Ni huyu Priscilla, mpenzi mpya wa Jux kutoka Nigeria

STAA wa Nigeria, Priscilla Ojo, 23, ndiye ameushikilia moyo wa Mtanzania Jux, 34, kwa sasa baada ya mwanamuziki huyo kuachana na aliyekuwa mpenzi wake Karen Bujulu ambaye walidumu kwa takribani mwaka mmoja kuanzia Januari 2023.

Ukiachana na Karen, Jux alishawahi kuwa na warembo wengine kama Jacqueline Wolper, Jackie Cliff, Vanessa Mdee na Nayika Thongom kutoka Thailand ambaye waliachana kutokana na umbali baina yao.

Na sasa swali la wengi ni uhusiano huu mpya utadumu kwa muda gani ukizingatia historia ya staa huyo? Uhusiano wa Jux uliodumu kwa muda mrefu ni ule wake na Vanessa ambaye walikuwa pamoja kwa takribani miaka mitano.

Je, mpenzi huyo mpya wa Jux ni nani hasa? Priscilla Ajoke Ojo anayejulikana zaidi mtandaoni kama Priscy alizaliwa Lagos, Nigeria Machi 13, 2001, mama yake mzazi akiwa ni mwigizaji maarufu wa Nollywood, Iyabo Ojo.

Kwao walizaliwa wawili yeye na kaka yake mkubwa Festus. Wazazi wao waliachana walipokuwa wadogo na baba yao kwa sasa anaishi Marekani, hivyo kwa sehemu kubwa walilelewa na mama pekee. 

Elimu ya msingi na sekondari aliipata huko Lagos  alikohitimu 2017 kisha kujiunga na Chuo Kikuu cha Babcock kilichopo Ilishanremo, jimbo la Ogun kwa lengo la kusomea taaluma ya vyombo vya habari na sanaa za maonyesho.

Akiwa mdogo, Priscilla aliigiza katika filamu nyingi za Nigeria na nyingi zilitayarishwa na mama yake. Kwa kifupi ni mwigizaji mwenye talanta kubwa anayeweza kucheza nafasi yoyote anayopewa kwa ustadi na bidii.

Kutokana na uwezo wake, Priscilla alipokuwa na umri wa miaka 14 aliteuliwa kuwania Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike katika Tamasha la Filamu Nigeria 2015 baada ya kufanya vizuri katika filamu ya Beyond Disability (2014).

Mwaka 2014 alijiunga na mtandao wa Instagram, lakini  ilichukua miaka kadhaa mbele hadi kuanza kuchapisha picha ambazo zilivutia watu wengi kutokana na urembo na mtindo wake wa maisha, na kufika Juni 2022 akafanikiwa kufikisha wafuasi milioni mbili.

Kwa sasa Priscilla akiwa na wafuasi zaidi ya milioni 2.8 wanaomfuatilia Instagram, chapa nyingi kubwa nchini Nigeria zimeshirikiana naye kukuza huduma na biashara zao kupitia ushawishi wake mtandaoni.

Miongoni mwa chapa ambazo amefanya nazo ni kampuni ya cryptocurrency ChiJ14Exchange, kampuni ya utengenezaji wa filamu ya Viskit, chapa ya vipodozi Hegai and Esther na kampuni ya simu za Itel Nigeria.

Zaidi amefanya kazi na chapa za urembo na mitindo kama House Of Sweeter Things, Sunglasses and Moore, Cassie Hair, Top Posh Collections, Beautiful Body Nigeria, St. Nalex Wears, Houz. Of Tee, Gattyz Makeovers, DMC Luxury, Official Lady Bug Cosmetics na kadhalika.

Mrembo huyo mwenye chapa yake ya mavazi, Priscy Closet, anaishi katika nyumba ya kifahari huko Lekki, Lagos pamoja na mama na kaka’ke huku akiwa na urafiki na watu maarufu mitandaoni Nigeria kama Diana Eneje na Rachel Doll.

Priscilla anayetajwa aliwahi kuwa na uhusiano na wanamuziki kama Korede Bello na Lil Kesh, anapata fedha nyingi kutokana na kazi yake ushawishi wa chapa mtandaoni (influencer) na sasa anamiliki gari aina ya Mercedes Benz.

“Anatengeneza fedha kwa hiyo inanipunguzia msongo wa mawazo. Niliruhusiwa kufanya nilichotaka, hivyo nilitarajia hilo pia kwa watoto wangu. Ninapenda kwamba anafanya mambo mengi ambayo ninafanya,” anasema mama’ke, Priscilla, Ojo.

Oktoba 2022 ulizuka uvumi Nigeria kuwa moja ya video za ngono iliyosambaa zaidi mtandaoni ilikuwa ya Priscilla kitu kilichomlazimu kujitokeza na kukanusha vikali.

“Nimesikia blog moja ina mkanda wangu wa ngono. Kwa nini huonyeshi uso wangu? Onyesha uso wangu kwenye video tuone. Pili, nina alama kubwa ya kuzaliwa nyuma ya miguu yangu, mbona nayo hatuioni? Kwa hiyo, jaribu tena,” aliandika Instagram.

Akizungumzia mwenendo wa binti yake, Ojo anasema alimuondoa Priscilla katika uigizaji ili kumpa nafasi ya kusoma na hakutaka yeye na kaka’ke wawepo katika mitandao ya kijamii hadi pale walipofika sekondari.

“Walikuwa na mipaka ya mambo ambayo wangeweza kufanya kwenye mitandao na nilifuatilia kila kitu walichokuwa wakifanya, na ni muhimu sana kwa kinamama wote kufanya hivyo,” alisema Ojo, Septemba 2023.

“Sikumruhusu kuwa na habari nyingi za mambo mengi. Alipokuwa akienda chuo kikuu nilijua wazi sitakuwa naye hivyo nilihitaji kumruhusu kuwa mtandaoni, lakini misingi tayari ilikuwepo. Sasa amemaliza chuo na amerudi Nollywood kuigiza tena.”

Ikumbukwe Ojo alianza kuigiza 1998 akijiunga na Chama cha Waigizaji Nigeria (AGN) na hadi sasa ameshiriki katika filamu zaidi ya 150 na kutoa zaidi ya 14 zake binafsi. Alipokuwa na umri wa miaka 21 alisimama kazi baada ya kujaliwa watoto wawili, Festus (1999) na Priscilla (2021). 

Related Posts