NIKWAMBIE MAMA: Anguko letu ndiyo fursa yao, tusikubali

Nianze kwa kukupa pongezi kwa kuhimiza uhifadhi wa mazingira pamoja na kupanda miti. Usemi wako wa “Turekebishe pale tulipopaharibu” umekuwa na maana kubwa kwa Watanzania na wengi wetu tunaunga mkono jitihada hizi kwa moyo mmoja.

Vijana kwa wazee sasa wameamshwa na maendeleo ya matumizi ya nishati salama na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa. Hili ni jambo kubwa katika kulinda afya zao, lakini pia kutunza mazingira. Athari za moshi na hewa ya ukaa ni mbaya sana kiafya, lakini pia miti inayokatwa kwa siku moja inagharimu miongo tangu kupandwa hadi kukomaa. Hapa tunaongeza athari za mabadiliko ya tabianchi yanayotishia ulimwengu hivi sasa.

Kwenye matumizi ya nishati salama kuna ufumbuzi wa mambo mengi, japokuwa changamoto zake ni nyingi pia. Kwa haraka naweza kusema gharama za gesi na umeme si rafiki kwa Mtanzania wa kawaida, hasa mama wa nyumbani. Iwapo jitihada za kushusha gharama hizo zitafanywa vema kuanzia kwenye uzalishaji wake, naamini tutafikia malengo na kupiga hatua mbele.

Leo sitakaa sana humo kwa sababu nagusa kwenye kona nyingine inayogusa humohumo kwenye utunzaji wa afya zetu na uhifadhi wa mazingira. Hivi vitu viwili vinashikana kama ngozi na mwili. Huwezi kuwa na afya timamu kwa kula mazao yanayotoka kwenye mazingira mabovu, pia huwezi kuhifadhi mazingira ukiwa na mgogoro wa afya. Hili ni jambo mtambuka, lakini nitafafanua.

Watanzania wengi hivi sasa wana matatizo ya afya ya akili. Hivi tunavyoongea, mambo yanayoendelea huku uswahilini yanatisha. Mtu analipia taxi Sh3,000 kumkimbia mwenzake anayemdai Sh5,000. Mwingine anakodi ngoma kwa Sh30,000 kwenda kumsuta mtu aliyemsema kwa kutompeleka mwanaye shuleni. Tena kuna aliyefunga genge la chakula akaenda kukesha kwenye maombi ili apate hela.

Kuna matatizo yasiyohesabika yanayosababishwa na udumavu wa afya ya akili. Baadhi yake ni uamuzi wa kiwendawazimu, kuongezeka uzito kusikostahili, maradhi yasiyoambukizwa na mengi mengineyo. Na haya yote ni tishio kubwa kwenye jamii yetu kwa hivi sasa. Lakini watu wengi tumejizoesha kulaumu jiwe tuliloangukia badala ya kisiki tulichojikwaa. Hivyo, kila siku matatizo huenda yakiongezeka kwa kuwa hatujashughulika na vyanzo vyake.

Ninachokiona cha kwanza ni ulaji. Watu wanasahau ulaji bora wa asili na wanahangaika na misosi ya kuigiza. Chakula cha kawaida huko maofisini na kwenye shughuli za watu ni chipsi kuku na mayai. Wanapokula chakula hicho, wengi hudhani kwamba wamekula vizuri, lakini wanasahau kuangalia aina ya mayai na kuku huyo, mbegu ya viazi iliyotumika na hata mafuta yaliyokaangiwa chakula hicho.

Mbegu bora ni kitu cha msingi kwenye chakula. Kwa mujibu wa wataalamu, mbegu asilia ndizo zinazoongoza kwa ubora duniani kote. Lakini watu wengi wanazikwepa kwa madai ya kuchelewa kupata mrejesho wa maokoto. Hata hivyo, ubora una gharama zake; huwezi kwenda bandani ukapata chakula bora cha asili, lazima utakutana na vya mchongo. Tukae tukielewa kuwa ukosefu wa chakula asilia husababisha kuyumba kwa afya ya mlaji.

Inatia moyo kuona watu makini wakihamasika na urejeshwaji wa mbegu za asili. Mbegu hizi zina uthabiti, uhimilivu na zinavumilia majanga kama ukame na magonjwa. Tofauti na mbegu za mchongo, mbegu asilia ni chanzo kikuu cha nasaba za mimea zinazotumiwa na watafiti. Kutokana na hali ya kimaisha ya wakulima wadogo, inawezesha watu binafsi, kaya au vikundi vya wakulima kumudu upatikanaji na matumizi yake.

Serikali ni lazima itilie mkazo uhamasishaji wa matumizi ya mbegu asilia kuanzia kwa wakulima. Tunaona wenzetu kama Rwanda, Ethiopia, Zimbabwe na Uganda walivyolitengenezea sheria suala hili. Hivi majuzi kwenye kumbukizi ya uhuru wa Mandela, Afrika Kusini ilihanikizwa kwa maonesho ya chakula cha asili. Kwenye shughuli hiyo hakukuonekana matufaa makubwa yanayodaiwa kuingizwa hapa kwetu kutoka huko. Hatuna budi kushtuka.

Pamoja na kukazia uhamasishaji wa matumizi ya mbegu asilia, kuwe na upunguzaji wa uingizwaji wa mazao yatokanayo na mbegu za mchongo. Mbegu zetu ni tiba ya magonjwa mengi, hivyo wadau mbalimbali, wakiwemo wakulima waelekezwe kujikita katika kilimo cha kutumia mbegu asili. Tunaweza kuokoa muda na fedha nyingi kwenye bajeti ya afya iwapo tutaondoa chanzo cha tatizo badala ya kusubiri tatizo litushughulishe.

Kule Brazil kwenye kijiji cha Caatinga, wakazi wameanzisha benki ya mbegu asilia zinazohimili mikiki ya mabadiliko ya tabianchi. Mbegu hizo ndizo zimekuwa tumaini la kipekee baada ya ardhi yao kupatwa na majanga yanayotokana na uharibifu wa mazingira. Wamekuwa mfano bora kiasi cha kuuvutia Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo Duniani (IFAD), hadi kuamua kuwashika mkono.

Hakika katika majanga yanayotuzunguka, mbegu asilia ndio suluhisho la kwanza. Tutapunguza madhara mengi baada ya kuimarisha afya ya mwili na akili, tutaboresha mazingira na hatutayumbishwa na mabadiliko ya tabianchi. Tukumbuke kuwa anguko letu linasubiriwa kwa hamu na adui zetu watakaoligeuza kuwa fursa yao.

Wa kujithamini zaidi ni sisi wenyewe.

Related Posts