Sh bilioni 7 zaing’arisha Kata ya Kivule

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Zaidi ya Sh bilioni 7 zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Kata ya Kivule iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi Juni 2024.

Fedha hizo zimetolewa na Serikali Kuu na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia mapato yake ya ndani.

Takwimu hizo zimetolewa na Diwani wa Kata ya Kivule, Nyansika Getama, wakati wa mkutano wa hadhara aliohitisha kwa lengo la kueleza umma kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi katika kata hiyo.

Amesema fedha hizo zimetumika kuboresha elimu ya msingi (Sh 1,648,400), elimu ya sekondari (Sh 1,891,200), sekta ya afya (Sh bilioni 2.2) na miundombinu ya barabara, madaraja, mitaro (Sh zaidi ya Sh bilioni 2).

“Nilipochaguliwa nilifanya ziara katika kata yote, nilisema haiwezekani Jiji la Dar es Salaam watoto wanakaa chini. Tulihakikisha tunaondoa upungufu wa madawati na sasa hivi watoto wa shule za msingi 14,925 hakuna anayekaa chini,” amesema Getama.

Amesema katika Shule za Msingi Kivule, Serengeti, Bombambili, Misitu na Magore wamenunua madawati 2,650 wamejenga vyumba vya madarasa 48, matundu ya vyoo 128 wakati katika Shule za Sekondari Abuu Jumaa, Misitu, Kerezange wamejenga vyumba 66, kununua viti na meza (1,420) pamoja na ujenzi wa matundu ya vyoo na ofisi za walimu.

Kwa upande wa sekta ya afya amesema wamejenga Hospitali ya Wilaya Kivule yenye majengo ya wodi ya wanawake (Sh milioni 240.2), wodi ya watoto (Sh milioni 316.5), jengo la macho na meno (Sh milioni 412), jengo la upasuaji (Sh milioni 191.2) na jengo la kuhifadhia maiti (Sh milioni 78.9).

Diwani huyo amesema ujenzi wa jengo la chuo cha uuguzi unaendelea na hadi sasa Sh bilioni 2.1 zimetumika kati ya Sh bilioni 5 zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo.

Kuhusu miundombinu amesema wamejenga barabara, madaraja, mifereji nak ingo za mto Magole A, Mkolemba, Kivule, Mto Mbonde na kwamba Barabara ya Banana – Kitunda – Kivule – Msongola itajengwa kupitia Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP) unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Akizungumzia kituo cha polisi kilichojengwa kwa ushirikiano wa nguvu za wananchi na halmashauri amesema mpaka sasa Sh milioni 97 zimetumika na kuahidi kuwa kitaanza kutoa huduma kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Wananchi wamempongeza diwani huyo kwa juhudi za kuleta maendeleo katika kata hiyo na kumuomba aharakishe kutatua changamoto za ubovu wa barabara, usafiri wa daladala katika baadhi ya maeneo, migogoro ya ardhi, urasimishaji wa makazi na Kivuko cha kwa Mbonde.

Mkazi wa Magole A, Jeremiah Chacha, amesema hakuna magari yanayofika Makonde – Mnarani hali iliyosababisha gharama za usafiri kuwa kubwa na kero zaidi kwa wanawake na watoto.

Idd Fundikira, amedai kuna utapeli wa viwanja, taarifa za mapato na matumizi hazisomwi na kuomba waliolipa Sh 120,000 kwa ajili ya urasimishaji warejeshewe fedha zao kama Serikali ilivyoelekeza.

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo ameahidi kuwa halmashauri itamalizia ujenzi wa kituo cha polisi na mwezi ujao watatangaza zabuni za ujenzi wa barabara ambapo Kata ya Kivule pia itanufaika.

“Hatutaki Rais Samia achafuke kwa watu wanaotumia nafasi zao kujinufaisha, fuatilieni wenyeviti waliotajwa kuhusika kuuza viwanja mara mbili na mkijiridhisha juu ya suala hilo likija kwetu tunamaliza,” amesema Kumbilamoto.

Related Posts