Dar es Salaam. Tanzania inatarajia kujifunza mbinu za kijeshi kutoka China kuanzia mwishoni mwa wiki baada ya kupokea meli tatu zenye wanajeshi kutoka Taifa hilo.
Wanajeshi hao wamekuja nchini kushiriki mazoezi ya pamoja kati ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Ukombozi la Watu wa China, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya ushirikiano kati ya nchi hizo na miaka 60 ya JWTZ inayoadhimishwa Septemba mosi.
Meli hizo zimetia nanga siku moja baada ya meli vita kutoka China iliyokuwa ikitoa matibabu kwa wagonjwa kwa siku saba kumaliza kazi. Ilitia nanga Julai 16, 2024.
Akizungumza na wanahabari, Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji Tanzania, Ameir Ramadhan Hassan amesema anaamini ujio wa wanajeshi hao kutoka China utawawezesha kujifunza vitu vingi kwa sababu wameendelea kijeshi na kiuchumi.
“Tunajifunza kutoka kwao, tunaamini na tuna imani mazoezi yatatuongeza uwezo wetu kijeshi,” amesema Hassan. Hii ni mara ya nne kufanyika mazoezi ya pamoja kati ya wanajeshi wa Tanzania na China.
Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2014, mazoezi yalifanyika Kigamboni jijini Dar es Salaam, mwaka 2019/2020 yalifanyika Mapinga mkoa wa Pwani, na ya tatu yalifanyika Septemba, mwaka jana.
Tofauti na miaka mingine, mazoezi ya mwaka huu yamebeba upekee ikielezwa ndani yake kutakuwa na maadhimisho ya miaka 60 ya JWTZ na miaka 60 ya ushirikiano kati yake na China.
“Pia mazoezi haya yatahusisha vikundi vyote vya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kuanzia vikosi vya anga, majini na wale wa nchi kavu, mazoezi yaliyopita yalikuwa ni vikundi maalumu pekee,” amesema Hassan.
Balozi wa China nchini, Chen Mingjian amesema ujio wa wanajeshi hao anaamini utaisaidia Tanzania kuongeza uwezo kijeshi.
Ujio huo amesema ni moja ya njia za kudumisha ushirikiano kati ya Tanzania na China ambao umedumu kwa miaka 60.
“China ni moja ya wawekezaji wakubwa nchini Tanzania, inatoa wakandarasi wakubwa wa miradi ya miundombinu, hata utalii. Mwaka huu tunatarajia watalii 50,000 watembelee Tanzania, uhusiano wetu umekuwa ukigusa sehemu mbalimbali,” amesema Mingjian.