Tanzania, Marekani kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki

Dar es Salaam. Tanzania na Marekani zimekubaliana kuendelea kuimarisha uhusiano katika masuala ya siasa na hasa katika uchaguzi ili kuhakikisha wananchi wanatumia haki yao kuapata viongozi wanaowataka.

Hayo yameelezwa leo Julai 24, 2024 na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anashughulikia masuala ya siasa wa Marekani, John Bass aliyekuwa na ziara ya siku tatu katika nchi za Tanzania na Chad.

Bass aliyezungumza na waandishi wa habari duniani kupitia mtandao wa Zoom, amesema katika mazungumzo yake na viongozi waandamizi wa Serikali ya Tanzania wamejadiliana jinsi ya kuimarisha uhusiano ambao tayari umekuwepo katika nyanja za siasa, uchumi na masuala ya afya.

“Kitu cha msingi nilichokuja kufanya ni kuelewa vipaumbele vya Tanzania, kama unavyojua katika miezi ijayo nchi zetu zinakwenda kwenye uchaguzi.

“Pamoja na kuimarisha uhusiano wa Serikali zetu, tunahakikisha watu katika nchi zetu wanakuwa na fursa wa kutoa sauti zao katika sanduku la kura,” amesema.  

Amesema pia wamejadiliana kuendelea kusaidia sekta ya afya hususani mapambano dhidi ya Ukimwi, uwekezaji katika miundombinu ya afya na mapambano ya ugonjwa wa malaria.

Katika uchumi, amesema wamejadiliana na viongozi wa Serikali kuimarisha ustawi wa Watanzania na kuimarisha uchumi wa kijani, unaolenga kupunguza athari za uharibifu wa mazingira na uwekezaji katika madini ya kimkakati.

 “Tumetathmini uwekezaji tuliouweka hapa Tanzania, hasa katika utawala huu wa sasa na kuangalia fursa za kuongeza ushirikiano wetu na kuimarisha uhusiano katika ulinzi na changamoto za kiuchumi na uwekezaji katika madini ya kimkakati na teknolojia katika uchumi wa kijani,” amesema. 

Alipoulizwa na Mwananchi kuhusu tatizo la uharamia katika Bahari ya Sham linavyokwamisha meli za mizigo kutoka Bara la Asia na Ulaya, Bass amesema Marekani imekuwa ikishirikiana na nchi nyingine kutoa ulinzi kusindikiza meli hizo.

“Tunajua kuna nchi nyingi ambazo uchumi wake unategemea meli hizo, hivyo tutaendelea kutoa ushirikiano kuzia uvamizi huo,” amesema.   

Kuhusu ziara yake nchini Chad amesema amejadiliana na viongozi wa nchi hiyo kuhusu namna ya kuimarisha uhusiano wa nchi hizo na kukabiliana na makundi ya uhalifu.

“Kwa Chad, kwa mfano, tulikuwa tunataka kuelewa nini kinaendelea kati ya Serikali ya Chad na wananchi wake kufuatia mgogoro uliokuwa ukiendelea katika nchi hiyo, na hali ya mizozo katika Sahara Magharibi kufuatia uwepo wa kundi la Boko Haram wanaosababisha migogoro na ongezeko la wakimbizi na hasa kwa nchi ya Afrika Magharibi,” amesema.  

Amesema migogoro katika nchi za Afrika Magharibi imekuwa ikisambaa kutokana na uwepo wa makundi yanayofanya kazi kwa zaidi ya nchi moja.

“Marekani imekuwa ikitoa misaada ya kibinadamu kwa watu wanakabiliwa na machafuko huko Dafur (Sudan) yanayosababishwa na migogoro na tutaendelea kushirikiana na nchi mbalimbali na wanachama wa Umoja wa Taifa.”

Related Posts