Tanzania, Nigeria kuvaana Kombe la Dunia Kriketi

UWANJA wa Dar es Salaam Gymkhana utashuhudia mechi ya ufunguzi ya kriketi kuwania kufuzu Kombe la Dunia kwa vijana wa chini ya umri wa miaka 19 kati ya Tanzania na Nigeria, Agosti 2, mwaka huu.

Hayo ni mashindano yanayoratibiwa na Chama cha Kriketi Duniani (ICC) na yatafanyika jijini Dar es Salaam ili kupata timu za Afrika zitakazofuzu kucheza fainali ya  kwa nchi za divisheni ya pili.

Mechi hiyo kwa mujibu wa msemaji na ofisa mawasiliano wa Chama cha Kriketi Tanzania (TCA), Ateef Salim itaanza ma saa 3:30 asubuhi.

“Tmu yetu iko imara baada ya mazoezi ya kutosha na imecheza mechi kadhaa za kujipima nguvu. Naamini tutashinda na kupata tiketi ya kucheza Kombe la Dunia kwa vijana walio chini ya miaka 19,” alisema Salim.

Siku hiyo hiyo, katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Ghana U19 itakwaana na Msumbiji U19 na kesho yake, Agosti 3,Sierra Leone itavaana na Rwanda katika mechi itakayopigwa saa 3:30 asubuhi wakati uwanja wa UDSM utashuhuda tena mechi kati ya Botswana na Malawi.

Agosti 4, mwaka huu, Nigeria itakuwa Gymkhana kupambana na Msumbiji wakati Tanzania itaumana na Ghana katika uwanja  wa UDSM.

Wakati huohuo, ligi ya mizunguko 20 ya Caravans T20  iliendelea katika viwanja mbalimbali jijini humo na waliong’ara ni pamoja na Aurobindo Agakhan ambao walipata ushindi wa mikimbio minane dhidi ya Alliance Caravans.

Aga Khan ndiyo waliopata kura ya kuanza na kufanikiwa kutengeneza mikimbio 166 ambayo vijana wa Alliance  walijitahidi kuifukizua, lakini mbio zao ziliishia kwa kupata mikimbio 158, hivyo kupoteza kwa mikimbio minane.

Ajith Kayyalakudi, aliyetengeneza mikimbio 61 na Abhik Patwa aliyecheza mikimbio 30 ndiyo walikuwa mashujaa wa mechi kwa upande wa washindi.

Katika mchezo mwingine, Lions waliwafunga Tamil Nadu kwa mikimbio 54. Lions walioanza kubeti walitengeneza mikimbio 152 huku wakipoteza wiketi tatu idadi ambayo Tamil Nadu walishindwa kuifikia baada ya wote kutolewa wakiwa wamefikisha mikimbio 98.

Rehaan Atif aliyecheza mikimbio 34, Daylan Manish aliyetengeneza mikimbio 33 na Karim Rashid aliyejazia kwa mikimbio 28, ndiyo walikuwa mashujaa kufunga upande wa washindi.

Vilevile, Jiji la Dar es Salaam lilishuhudia mechi za ligi ya mizunguko 20 kwa timu za divisheni C ambapo MCC  waliifunga Patel Titans kwa mikimbio minane. MCC walitengeneza mikimbio 113 ambayo Titans walishindwa kuifikia kwa kupata mikimbio 105.

Ali Asgar aliyetengeneza mikimbio 30 na Gokul Nair aliyeongezea 20 walikuwa nyota wa ufungaji kwa timu ya MCC

Related Posts