Afrika ina asilimia 65 ya ardhi yenye rutuba ambayo haijalimwa iliyosalia kote duniani. Licha ya ukweli huo, benki ya maeneleo ya Afrika inabainisha kuwa bara hilo linatumia karibu dola bilioni $60 kila mwaka kununua chakula kutoka nje.Wadau wajadili kilimo cha kulinda mazingira mjini Kampala
Matumizi hayo yanatarajiwa kuongezeka hadi kufikia dola bilioni $110 utakapofika mwaka 2025 kutokana na ongezeko la mahitaji pamoja na mabadiliko ya mwenendo wa watumiaji. Kulingana na Wizara ya Kilimo ya Kenya, karibu asilimia 63 ya ardhi yenye rutuba nchini humo ina tindikali.
Kwa upande wake Shirika la Chakula na Kilimo duniani linaripoti kuwa uzalishaji wa mahindi ulipungua kwa asilimia 4.4 mwaka 2022. Hata hivyo halikutaja sababu.
Benson Wanjala ni mkulima katika kijiji kimoja magharibi mwa Kenya. Anasimulia kuwa, alipoanza shughuli za kilimo zaidi ya miongo miwili iliyopita, shamba lake la ekari 10 lilikuwa na uwezo wa kuzalisha magunia 200 ya mahindi. Sasa anapata magunia 30 pekee.
Analalamika kuwa, ardhi yake iliyokuwa na rutuba haina uhai tena na haimsaidii kuendesha maisha kama hapo awali hivyo imempasa kuangalia namna nyingine ya kuishi.Afrika yashauriwa kukuza kilimo cha kisasa
“Nilishauriwa kutumia mbolea, lakini sikuwa nafuga ng’ombe wakati huo. Wakati nikiwa najiuliza ni kwanini uzalishaji wa mazao umepungua, niliamua kuhamia Nairobi na kuanza kulima mbogamboga,” alisema mmoja wa wakulima.
Wizara ya ardhi ya Kenya haikujibu maswali juu ya changamoto hii hasa mara baada ya kashfa ya mwezi Aprili kuhusu uwepo wa mbolea ya uwongo. Mbolea hiyo ilipatikana katika mifuko iliyoandikwa majina bandia na kugawanywa kwa wakulima kupitia programu maalumu ya ruzuku ya kitaifa.
Rais William Ruto alisema kuwa wakulima wasiopungua 7,000 walinunua mbolea hiyo na wangepewa fidia kwa kupatiwa mbolea sahihi. Mwezi Mei, nchi hiyo ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa afya ya udongo barani Afrika pamoja na masuala mengine yanayolenga kuongeza uzalishaji wa chakula.
Katka Mkutano huo Mkurugenzi mtendaji wa chama cha wakulima wa Afrika Mashariki Stephen Muchiri, alitoa wito kwa wakulima kurejea katika njia za asili za kilimo.
Kwa upande wake mwanaharakati wa masuala ya chakula katika shirika la Greenpeace Afrika Elizabeth Atieno Opolo, amesema wakulima hawana budi kujikita kwenye kilimo endelevu. Anaongeza kuwa licha ya kuwa kilimo cha aina hiyo kinachukua muda mrefu, manufaa yake ni ya muda mrefu pia. Ameongeza kuwa, matumizi ya mbolea za kemikali si tu kuwa yanaharibu ardhi bali pia yanaangamiza kabisa mazingira kwa ujumla.
Soma pia: Jukwaa la Mfumo wa Chakula Afrika lahitimishwa Tanzania
Kuporomoka kwa ubora wa ardhi ya kilimo si tatizo la Kenya pekee bali ni changamoto inayotia wasiwasi usalama wa chakula kote Afrika. Nchini Zimbabwe, asilimia 70% ya udongo una tindikali, kwa mujibu wa serikali. Kipindi cha nyuma, serikali ya taifa hilo ilileta mbolea za kemikali katika juhudi za kuimarisha udongo. Hata hivyo matumizi mabaya ya mbolea hizo yalikwamisha malengo.
Shirika linalopigia upatu mageuzi ya Kilimo barani Afrika la AGRA linapendekeza wakulima wapime tindikali katika udongo wao na watumie chokaa ili kupunguza kiwango kikubwa cha kemikali hiyo. Lakini wakulima wanasema gharama ni kubwa. Kupima udongo kunagharimu dola $20 hadi $40 za kimarekani.