Utapenda wadau wanavyojadili matumizi ya intaneti, faida zake kemkem

Dar es Salaam.  Wadau wa masuala ya teknolojia nchini Tanzania wamesema intaneti ina nafasi kubwa katika kuchochea maendeleo ya nchi, hivyo mamlaka zinazohusika zina wajibu wa kuhakikisha huduma hiyo inaboreshwa ili kumnufaisha kila mtu kwenye jamii.

Kutokana na fursa nyingi zinazopatikana kupitia mtandao huo, wadau hao wamesema ni nadra kwa mtu yeyote anayehitaji maendeleo kutoutumia kwani zipo fursa kemkem.

Wadau wametoa maoni hayo leo Jumatano, Julai 24, 2024, wakati wa kuchangia mada kwenye mjadala wa Mwananchi Space, ambao hufanyika kila Jumatano kwenye mtandao wa X,  mada ya leo ikihoji, ‘Ipi nafasi ya huduma za intaneti katika maendeleo ya nchi?’

Akichangia mjadala huo, mdau wa masuala ya mtandao, Kelvin Mmari, amesema huduma za intaneti zina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi, akitolea mfano mawasiliano ndani ya ofisi za Serikali ambapo intaneti kwa kiasi kikubwa ndiyo inatumika.

“Ukienda katika ofisi mbalimbali za Serikali, intaneti ndiyo inatumika kwa kiasi kikubwa na ikikwama, huduma nyingi zinasimama,” amesema.

Kuhusu matumizi ya mtandao huo, Mmari amesema hakuna mtu anayeweza kukwepa matumizi yake kwa maendeleo binafsi kwani zipo fursa nyingi kwenye intaneti.

Akizungumzia upatikanaji wa intaneti, Mkurugenzi wa Mipango na Uhandisi kampuni ya mawasiliano ya Tigo, Semvua Kissenge, amesema intaneti haitokei tyu kwa bahati. “Sisi watoa huduma tunatengeneza mazingira wezeshi ya kuhakikisha intaneti inamfikia mtu wa mwisho na kupata huduma au kitu kitakachomwezesha kutengeneza maendeleo yake.

“Tumefikia awamu nyingi za teknolojia ikiwemo 4G na 5G au hata kwenda kuunganisha mkongo nyumbani au ofisini kulingana na mahitaji ya mtu, hii inamsaidia mtu kurahisha mawasiliano yake ya kila siku,” amesema.

Kissenge amesema kwa miaka mitatu iliyopita, isingewezekana kukutana kupitia mjadala wa X (zamani Twitter), hivyo intaneti imefanya mambo kuwa rahisi katika nyanja zote za huduma.

Kama watoa huduma, Kissenge amesema wanachofanya ni kuwawezesha watu wapate huduma za intaneti kwa kuwawezesha kupata simu janja ili watumie na kurahisisha maendeleo ili watu wapate taarifa wanazohitaji popote walipo.

Pia, amesema wanashirikiana na Serikali kuhakikisha intaneti inafika kote nchini, hasa vijijini kwa kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa ubora wa mtandao ambao pia hupatikana mijini.

Amesema kwa sasa huduma za kifedha na kijamii zimerahisishwa na kila mtu anaweza kufanya jambo lake kwa kutumia mtandao wa intaneti.

Kissenge amewaomba watu wenye matumizi makubwa ya intaneti kujiunga na huduma bora zaidi zinazoweza kuwapa muunganiko kwa haraka zaidi.

Mapema,  Mhariri wa Uchumi wa Gazeti la Mwananchi, Ephrahim Bahemu amesema kutokana na umuhimu wa mtandao wa intaneti katika nyanja za uchumi, siasa, biashara na kijamii, huduma hiyo ni sehemu ya maisha na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

“Zamani miaka ya 1990 kulikuwa na mtandao wa 2G ambao tumeenda nao hadi sasa tupo 5G huku wengine wakitazamia 6G, mapinduzi yote haya yanaongeza kasi ya mawasiliano na kuongeza ufanisi katika shughuli mbalimbali.

“Umuhimu wake unakuja pale inaporahisisha shughuli za kibiashara, kilimo kupitia taarifa za hali ya hewa, uchumi na hata siasa. Mtandao wa intaneti umeongeza ukuaji wa biashara kwa kufanya utafiti sambamba na kupata ujuzi kupitia mtandao,” amesema Bahemu wakati akichokoza mada kwenye mjadala huo.

Hivyo, kutokana na kutoa fursa kubwa, amesema intaneti ni maisha na huduma hiyo ina umuhimu mkubwa na inahitajika kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya nchi kwa ujumla.

“Mtandao wa intaneti umesaidia ukuaji wa biashara kwa kuongeza vionjo vipya katika utoaji huduma, kupata ujuzi na ufanyaji wa tafiti. Intaneti imesaidia watu kufanya kazi nyingi kwa muda mfupi, hata kwenye siasa imerahisisha watu kufanya kampeni kupitia mitandao na kufikia watu wengi hivyo intaneti kwangu ni sehemu ya maisha ya binadamu,” amesema Bahemu.

Bahemu ameongeza kuwa nafasi ya intaneti katika jamii ni kukuza biashara, ujuzi, uzalishaji na kila kitu chenye tija kwenye Taifa.

Mbali na hayo, amebainisha kuwa kutokana na matumizi ya intaneti, watu wanapata ujuzi na wanafunzi wanafanya utafiti kupitia intaneti.

Hoja ya Bahemu imeungwa mkono na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Smart African Group, Edwin Bruno, ambaye amesema nafasi ya intaneti katika maendeleo ya nchi ni kubwa. Kutokana na ukubwa huo, amesisitiza mamlaka zote zinazoshughulika na mitandao zihakikishe zinaboresha huduma ili wananchi wafikie malengo yao.

“Ni lazima wananchi wapewe elimu waelewe namna sahihi ya kutumia teknolojia ya intaneti. Ukiuangalia utumiaji wa intaneti unaona kabisa kuna uwalakini, hivyo lazima tuwekeze kuwafundisha watu ili waweze kuitumia ipasavyo kwa sababu ina nafasi kubwa,” amesema.

Amebainisha kuwa Tanzania ina asilimia nane ya watumiaji wa mtandao, hivyo inapaswa kulifanya jukwaa hilo kuwa chombo cha habari na sehemu ya kukuza biashara.

Wingi huo wa watumiaji ndio Bruno amesema haupaswi kuwa sehemu ya kuongea umbea na majungu, bali kuwa sehemu ya kukuza biashara kwa kuwa unatoa nafasi kubwa ya kuwakutanisha na watu mbalimbali duniani.

Bruno amebainisha kuwa dunia imekuwa kijiji na mitandao inawakutanisha Watanzania na watu wa nje ya nchi, hivyo watu wanaweza kuuza bidhaa zao kupitia mitandao ya kijamii na kukuza uchumi.

“Hata biashara changa na bunifu (startups) zinapaswa kukuzwa kwa kupewa ushirikiano na Serikali na wadau kwa ajili ya kukua zaidi ya hapa zilipo,” amesema.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts