Waandishi wanolewa kuripoti habari za ukatili wa jinsia kwa wanawake mitandaoni

Dar es Salaam. Uchache wa uripotiji na ukandamizaji wa waathirika wa kesi za ukatili wa kijinsia kwa wanawake kwenye mitandao ya kijamii umetajwa kuwa changamoto kwa baadhi ya waandishi wa habari wanaoripoti kesi hizo.

Changamoto hiyo imebainika kupitia utafiti uliofanywa Afrika Mashariki na Shirika la (DW Akademie ambalo ni Shirika la Deutsche Welle (DW) Ujerumani, linaloshughulika na maendeleo ya vyombo vya habari na mafunzo ya uandishi wa habari duniani.

Hivyo, kutokana na hali hiyo, shirika hilo limeendesha mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) pamoja na wengine kutoka vyombo kadhaa vya habari jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kuhitimisha mafunzo hayo yaliyofanyikia ofisi za MCL, Tabata Relini, Dar es Salaam, leo Jumatano, Julai 24, 2024, mkufunzi wa mafunzo ya ukatili wa wanawake mtandaoni kutoka DW Akademie, Anwary Said amesema dhumuni la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo waandishi katika kuripoti kesi za namna hiyo.

“Kumekuwa na ukandamizaji wa waathirika wa ukatili mitandaoni kufanywa kama wahusika wakuu kuliko yule aliyesababisha ukatili huo. Pia hakuna namna nzuri ya kuripoti kesi hizi, hivyo tukaona tuanzie hapa,” amesema.

Amesema siku hizo tatu za mafunzo anaamini zimesaidia kuboresha uwezo wa waandishi hao huku wakitarajia mabadiliko chanya. Amesema mafunzo hayo ni ya tatu kufanyika kwa waandishi hapa nchini.

 Ofisa Mradi, Shirika la DW Akademie, Moses Mutente amesema DW Akademie inaamini vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kujenga jamii yenye usawa na kuzingatia haki za msingi za jamii.

“Kwa miaka mingi habari zinazohusu ukatili wa wanawake mtandaoni hazipewi uzito unaostahili hali iliyopelekea sauti za wanawake wengi kuzimwa kutokana na hofu ya kushambuliwa.

“Kupitia mafunzo haya, DW Akademie inaamini kwamba waandishi hawa watakuwa chachu ya mabadiliko kwenye vyumba vyetu vya habari kwa kuandika habari hizo kwa usahihi na kwa kuzingatia weledi.

“Kupitia mradi wetu wa Mind The Gap, DW Akademie imewajengea uwezo waandishi mbalimbali kutoka Mwananchi Communications, EFM/TVE, Channel Ten/ Magic FM, Dar24, TBC na Mjini FM. Mradi umejikita pia kwenye kuwajengea washiriki uwezo wa kuwa wakufunzi watakaoweza kupeleka kazi hii mbele,” amebainisha Mutente.

Amesema lengo kuu ni kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari na kusaidia waandishi wa habari na watangazaji kujenga ujuzi wa kitaaluma na maadili ya juu.

Mhariri wa Mafunzo wa MCL, Rashid Kejo amesema dhima ya kampuni hiyo ni kuliwezesha taifa.

Hivyo mafunzo hayo yatawezesha taifa kwa namna ya kuhakikisha wanawake wanapata haki katika jamii kwa mujibu wa sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kampuni yetu ya Mwananchi inafurahi kuwa sehemu ya mafunzo haya, kila mmoja anahaki sawa na mwingine, ana haki ya kufurahia maisha, matunda na keki ya taifa. Kwahivyo tunafundishana ili twende tukayatekeleze yale yanayopaswa kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi,” amesema Kejo.

Aidha, amewataka waandishi waliopata mafunzo hayo wakayafanyie kazi kwa kutafuta habari zenye matokeo katika jamii.

Omari Mwaisumo mwandishi wa habari kutoka DFM radio amesema mafunzo hayi ya siku tatu yamempa uelewa wa namna ya kuripoti habari hizo kwa usahihi kama inavyotakiwa.

Pia, Grolian Sulle wa Mwananchi amesema mafunzo hayo yatamsaidia katika kuripoti kwa weledi kwakuwa amezidi kuelewa kwamba ukatili unarudisha nyuma watendewa, hivyo ni jambo la kutiliwa mkazo. 

Mkufunzi wa mafunzo hayo, Salome Gregory amesema mafunzo ya unyanyasaji wa wanawake mtandanoni yanatoa  fursa kwa waandishi wa habari kujifunza namna tofauti ya kuandika habari hizo ili kuleta mabadiliko ya matumizi ya mitandao ya kijamii na kuifanya kua sehemu salama kwa watu wote.

Related Posts