Wakili Kitale aikomalia TLS, afungua kesi nyingine

Mwanza. Zikiwa zimepita siku tisa tangu Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza itoe ruhusa kwa Wakili Steven Kitale kuwasilisha maombi ya mapitio ya kisheria dhidi ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), hatimaye wakili huyo amefungua shauri hilo.

Shauri hilo namba 17558/2024 lililofunguliwa Julai 22, mwaka huu liko mbele ya Jaji Wilbert Chuma na tayari wito wa mahakama umekwishatolewa kwa wajibu maombi, kwa mujibu wa wakili huyo.

Wajibu maombi katika shauri hilo linaloanza kusikilizwa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza Julai 26, 2024, ni TLS, Mkurugenzi Mtendaji wa TLS, Baraza la Uongozi la TLS, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Katika shauri hilo, Kitale ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la Uongozi la TLS, anahoji uamuzi wa chama hicho kupandisha ada za wanachama wake kuhudhuria Mkutano Mkuu wa mwaka (AGM) kutoka Sh118,000 hadi Sh200,000  bila yeye kuwa na taarifa.

Wakili huyo anadai anapoomba mihtasari ya vikao vilivyopitisha ongezeko hilo amekuwa akipigwa danadana, jambo lililomkwamisha asitekeleze wajibu wake kwa wanachama.

“Tunaomba tupate taarifa kamili za ongezeko la ada ya mawakili wanaohudhuria kwenye mikutano ya AGM.

Awali, anasema gharama iliyopendekezwa na Baraza la Uongozi la TLS ilikuwa Sh118, 767 na ndiyo iliyopitishwa kwenye bajeti lakini baada ya muda kukawa na ongezeko hadi Sh200,000 na wame wanahoji bila kupata majibu.

Hoja nyingine katika shauri hilo ni kuiomba mahakama kutoa amri kwa Mkurugenzi Mtendaji wa TLS na Baraza la Uongozi TLS kutoa mihtasari ya vikao vilivyopitisha gharama hizo, kikao kilichoipitisha Kamati ya Uchaguzi ya TLS na Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi, jambo analodai lina ukiukwaji wa sheria, taratibu na kanuni za uchaguzi.

“Kwenye chama ambacho kina uwazi na kinafuata rule of law (utawala wa sheria) na kinachotakiwa kuonyesha utawala bora kimekosa hizo sifa kwa kushindwa kusimamia utawala wa sheria, ndiyo maana tumeamua kwenda mahakamani ambako haki inapatikana,” amesema Kitale.

Awali, Wakili wa Kitale, Godfrey Basasingohe amesema baada ya kukamilisha ufunguaji wa shauri hilo na kupangwa kuanza kusikilizwa Ijumaa Julai 26, mwaka huu, mawakili zaidi ya 20 wanatarajiwa kuungana naye katika shauri hilo.

“Maombi hayo mawili ya mteja wangu yamefikishwa mahakamani baada ya mbinu zote za kisheria na hatua za awali alizoelekezwa, kwa hiyo ameamua kuiomba mahakama iwalazimishe kutoa hizo nyaraka alizoomba.”

Related Posts