Dar es Salaam. Hatimaye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Z. H. Poppe Limited, Caeser Hans Poppe na mwanae Adam Caeser HansPoppe, wamejisalimisha Mahakama Kuu iliyopo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia (IJC) Temeke, jijini Dar es Salaam.
Hatua ya Caeser na Adam kujisalimisha, inatokana na Mahakama hiyo kutoa amri ya kukamatwa kwao kwa kosa la kuidharau Mahakama.
Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo, baada ya Caeser na Adam, kushindwa kufika mahakamani hapo kutoa orodha ya mali iliyokusanywa na kampuni hiyo, pamoja na nyingine, katika kesi ya mirathi ya namba 177/2022 ya marehemu Zacharia Hans Poppe.
Julai 5, 2024 Mahakama hiyo, chini ya Jaji Glady’s Nancy iliamuru Caeser na Adam, wakamatwe na wapelekwe mahakamani hapo ili washtakiwe kwa kuidharau Mahakama.
Wawili hao ni wakurugenzi wenza katika kampuni za marehemu Zacharia Hans Poppe, walitakiwa kuieleza mahakamani hali ya mali za marehemu Zacharia zilizopo katika kampuni zake ikiwemo taarifa ya mapato na matumizi, lakini hawakutokea siku hiyo.
Leo Jumatano, Julai 24, 2024, Caeser na Adam wamefika mahakamani hapo na kuomba mahakama isitekeleze amri ya kuwashtaki kama ilivyokuwa imelekeza kwa sababu wametii amri ya kufika wenyewe.
Wakurugenzi hao kupitia wakili wao kutoka kampuni ya Tan Law Africa, Peter Kibatala akisaidiana na Alphonce Nachipiangu, Gloria Ulomi na Rebecca Lyaka, wameomba mahakama hiyo iondoe amri iliyokuwa imeitoa na isitekeleze amri ya kuwashtaki kwa sababu wamefika wenyewe bila kukamatwa.
Jaji Barthy anayesikiliza shauri hilo alikubaliana na ombi la Kibatala na kuondoa amri ya kuwakamata na kuelekeza tarehe itakayopangwa na mahakama hiyo wakurugenzi hao na pamoja na wasimamizi wa mirathi siku hiyo wafike mahakamani hapo, bila kukosa.
“Naelekeza, wakurugenzi hawa na wasimamizi wa mirathi tarehe itakayopangwa na mahakama hii (Agosti 20, 2024) mfike bila kukosa,” amesema Jaji Barthy.
Shauri hilo liliitwa kwa ajili ya kujua iwapo amri iliyotolewa na mahakama imefanyiwa kazi ya kukamatwa kwa wakurugenzi hao.
Chumbuko la wakurugenzi hao kuitwa mahakamani hapo linatokana na watoto wa marehemu Zacharia HansPoppe, Angel na Abel, ambao ni wasimamizi wa miratji ya baba yao, kuiomba mahakama iwaite watoe taarifa ya fedha ikiwemo mapato na matumizi yaliyopo katika kampuni ya baba yao, Z. H. Poppe Ltd ambayo kwa sasa inasimamiwa na Caeser na Adam.
Katika maombi hayo Wakili Regina Helman, anayemwakilisha mtoto mkubwa wa marehemu Zacharia, Analisa Zacharia Poppe aliomba mahakama hiyo Caeser na Adam waitwe kwa sababu wao ndio waliyeshikilia hisa na mali za Zacharia HansPoppe katika kampuni zake na pia wanadaiwa kuendesha kampuni hiyo bila kuwashirikisha warithi ambao ni watoto wa marehemu.
Ombi hili la kukamatwa kwa wakurugenzi hao liliungwa mkono na Wakili Emmanuel Msengezi anayewatetea wasimamizi wawili wa mirathi ya Zacharia, Angel Zacharia Poppe na Abel Zacharia Poppe.
Msengezi alidai katika kampuni hizo, Zacharia Hans Poppe anamiliki hisa kwa asilimia 90 wakati Caeser ana hisa asilimia 10 pekee.
Zacharia HansPoppe alifariki dunia Septemba 10, 2021 katika Hospitali ya Aga Khan alikokuwa akipatiwa matibabu na mazishi yake yalifanyika Septemba 15, 2021 mkoani Iringa.
Hans Poppe alikuwa wanachama wa Simba na anayekumbukwa kwa kuiletea klabu hiyo mafanikio, kwa uhamasishaji aliofanya baada ya kuteuliwa pia kuwa mwenyekiti wa kundi la marafiki wa Simba ‘ Friend of Simba’ huku akiongoza kamati ya usajili.