Waraibu wa dawa za kulevya washituka, waomba Serikali ifanye oparesheni mpakani

Songwe. Waraibu wa dawa za kulevya waanoishi katika Mji wa Tunduma mkoani Songwe, wameiomba Serikali kuendesha oparesheni kwa kushirikiana na nchi jirani ya Zambia ya kudhibiti uuzwaji holela wa dawa za kulevya katika eneo la mpakani.

Wamesema kukithiri kwa biashara hiyo kumekuwa changamoto kubwa kwa nguvu kazi ya taifa na kusababisha waraibu walioanzishiwa tiba kuiacha na kurejea kwenye matumizi ya dawa hizo upya.

Aliyekuwa mraibu wa dawa za kulevya na kuhitimu matumizi ya tiba ya Methadone, Eleutherius Mbulingwe kwa niaba ya wenzake, ametoa ombi hilo leo Jumatano Julai 24, 2024, kwenye mkutano na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo.

Mkutano huo uliofanyikia mjini Tunduma, ulihusisha pia kamati za ulinzi na usalama zikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, wadau wa afya na waraibu wa dawa za kulevya walioanza tiba na waliohitimu kupitia mradi unaotekelezwa na Shirika la HJFMRI katika mikoa ya Mbeya na Songwe.

“Kamishna tunakuomba hapa mpakani fanya kama ulivyofanya maeneo mengine kuwakamata wauzaji wa dawa za kulevya, kwa sababu zinauzwa wazi wazi hata ukivuka upande wa Zambia, hali hii inawafanya baadhi ya waraibu walioanza tiba kurejea kwenye matumizi,” amesema Mbulingwe.

Amesema taifa linapoteza nguvu kazi licha ya jitihada za wadau kama Shirika la HJFMRI za kutaka kuhakikisha waraibu wanapewa elimu na kuanza tiba, kama hatua haitachukuliwa itakuwa kazi bure.

Amesema biashara ya dawa za kulevya imeshamiri mpakani hapo na kusababisha vijana kushindwa kujizuia kujidunga.

Ametolea mfano wa kliniki yao ya tiba ya methadone iliyokuwa na watu 900, lakini 200 tayari wameiacha.

“Tulianza tiba tukiwa 900, tayari 200 wameshaacha na wengine wako magerezani kwa makosa mbalimbali, sita wamepoteza maisha baada ya kurejea kwenye matumizi ya dawa za kulevya,” amesema mrahibu huyo.

Mraibu mwingine wa dawa hizo aliyeomba hifadhi ya jina lake, amesema mtandao wa biashara ya dawa za kulevya ni mkubwa mjini Tunduma na ameiomba Serikali kushirikiana na Zambia kukabiliana nao.

Akijibu maombi hayo, Kamishna Jenerali, Lyimo amesema tayari wamefanya mazungumzo na wenzao wa Zambia kwa ajili ya kushirikiana kudhibiti uingizwaji wa dawa za kulevya kupitia mpaka wa Tunduma.

“Mpaka wa Tunduma unatumika kuvusha na kusafirisha dawa za kulevya kwenye mabasi ya masafa marefu na magari ya mizigo kupeleka mikoa mbalimbali na mataifa mengine, dawa hizo ni pamoja na bangi iliyosindikwa (skanka) ambayo ina kiwango kikubwa cha kemikali,” amesema Lyimo.

Amevitaka vyombo vya dola mkoani Songwe na hususan katika mpaka wa Tunduma, kuweka mikakati ya pamoja kuongeza nguvu ya udhibiti. “Kwenye baadhi ya maeneo yenu kuna kilimo cha bangi kinaendelea huko, sasa niseme ikibainika kilimo kimefanyika, askari wa eneo husika watachukuliwa hatua kwa sababu vita ya mapambano ya dawa za kulevya inahitaji ushirikishwaji,” amesema Lyimo.

Kuhusu shuleni, Kamishna Jenerali Lyimo amesema wataanza utaratibu wa kuchukua sampuli za vipimo vya mikojo kwa wanafunzi kuanzia na wale wanaosoma shule za msingi kwa lengo la kubaini wanaotumia dawa hizo ili wawaanzishie tiba ya methadone.

“Kazi hii itahusisha halmashauri zote nchini tunalenga kupata idadi ya shule ili kuruhusu wataalamu wa maabara kuanza kazi ya  uchukuaji sampuli, tunataka kuokoa vijana ambao ni taifa la kesho,” amesema Lyimo.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo amepongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali kudhibiti biashara hiyo.

Chongolo amesema biashara ya dawa za kulevya inajenga taswira mbaya ya nchi na kuvitaka vyombo vya dola kutambua vina dhamana kubwa ya kushirikiana kuidhibiti.

“Kipindi cha miaka 11 iliyopita kilo 600,000 zilikamatwa, hatua hizo ni kutokana na jitihada mbalimbali za serikali kudhibiti uingizwaji na usafirishaji,” alisema.

Mkurugenzi wa mradi wa Shirika la HJFMRI Nyanda za Juu Kusini, Dk Emmanuel Behamana amesema kupitia mradi huo, wanaboresha upatikanaji wa huduma mbalimbali za tiba na matunzo kwa waraibu wa dawa za kulevya.

“Pia tuna wawezesha kuwa na miradi mbalimbali ya kiuchumi ili kuwaondoa kwenye dhana ya matumizi ya dawa za kulevya wanapohitimu tiba ya Methadone,” amesema.

Related Posts