AKILI ZA KIJIWENI: Labda nyie mnamwelewa Kibu Denis

NIMEJARIBU kumwelewa rasta Kibu Denis Prosper ambaye wiki chache zilizopita alisaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Simba, maana yake hajaanza hata kuutumikia.

Jamaa baada ya kusaini mkataba mpya na msimu wa 2023/2024 kumalizika akaiomba ruhusa klabu yake kuwa anaenda mapumzikoni Marekani ambako pia inaishi.

Uongozi wa Simba kiungwana ukamruhusu ukizingatia ni haki na lazima kwa mchezaji kupata mapumziko baada ya msimu kumalizika ili aweke sawa mwili na akili kabla ya kujiandaa na msimu mpya.

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, baada ya muda wa kupumzika aliopewa na klabu yake kumalizika, Kibu hakuungana na kikosi cha Simba katika kambi ambayo inaendelea Ismailia, Misri pasipo kutoa taarifa yoyote kwa uongozi.

Ikabaki kutupiana mpira tu, Simba wanasema wanaotaka kujua Kibu alipo waulize maswali upande wa mchezaji aseme yuko wapi na upande wa winga huyo nao ukahamishia kesi kwa Simba kuwa watafutwe wao waseme.

Hata hivyo, juzi msimamizi wa mchezaji huyo, Carlos Sylivester alikata mzizi wa fitna baada ya kufichua, Kibu amekimbilia Norway ambako amepata ofa ya kujiunga na timu moja ya huko huku Simba wakiwa hawafahamu lolote.

Mimi Kibu amenishangaza kwa sababu vyovyote itakavyokuwa hawezi kucheza ligi ya huko alikokwenda pasipo Simba kumuidhinisha maana ni mchezaji wao halali na hakuna mwanya wowote ambao mchezaji huyo anaweza kuutumia na akajiunga na timu ya huko bila Simba kuridhia.

Alipaswa kuwa mweledi tu kwa kuijulisha Simba kama utaratibu unavyotaka ili mambo yake yasije kukwama mbele ya safari.

Mwishowe ili acheze huko klabu ambayo ina mkataba naye itapaswa kuridhia kumwachia ili atumikie timu mpya ndio maana mimi sijamuelewa kwa hiki anachokifanya.

Related Posts