AKILI ZA KIJIWENI: Saluti nyingi kwa Maxi Nzengeli

SIKU moja kwenye ukurasa huu wa akili za kijiweni niliandika kitu kuhusu Maxi Mpia Nzengeli jinsi nilivyomuona kama usajili muhimu kwa Yanga tangu ilipomnasa.

Muonekano wake akiwa hajavaa jezi unaweza kukufanya ukamdharau na kudhani hana uwezo na kipaji cha soka lakini anapokuwa uwanjani huwa ni mwanadamu mwingine.

Ni mchezaji ambaye ana nishati ya kutosha inayomfanya awe na uwezo wa kukimbia kilomita nyingi ndani ya uwanja, pia ana uamuzi wa haraka na sahihi wa kujua aufanyie nini mpira kwa wakati gani.

Sio aina ya mchezaji ambaye anafanya vitu vingi vya kufurahisha jukwaa lakini ni mtekelezaji mzuri wa mipango ya benchi la ufundi pindi anapokuwa uwanjani.

Ndiyo maana sio jambo la kushangaza kuona amekuwa tegemeo kwa makocha wawili tofauti ambao wameinoa Yanga ambao ni Nasreddine Nabi na baadaye Miguel Gamondi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika viwanja vya mazoezi, Maxi anatajwa kuwa mchezaji ambaye ana kiwango cha juu cha ufanisi katika programu mbalimbali ambazo benchi la ufundi la timu hiyo limekuwa likiwapa wachezaji.

Katika soka la kisasa makocha wengi huwa wanahitaji kuwa na wachezaji wanaovuja jasho na kucheza kwa kujitolea kama alivyo Maxi ambaye amekuwa tegemeo katika kikosi cha Yanga.

Wiki iliyopita, Yanga ilicheza mechi ya kirafiki na Augsburg inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani na Maxi alianza kikosini na kumaliza dakika zote za mchezo huo ambao yeye ndio alipiga pasi ya bao moja ambalo Yanga ilipata.

Jambo la kushangaza, mmoja wa wachezaji wa Augsburg mpira ulipoisha alienda katika chumba cha kubadilishia nguo cha Yanga na kumpa jezi yake Maxi.

Related Posts