Aliyefungwa maisha kwa kumlawiti mtoto akwaa kisiki mahakamani

Arusha. Mahakama Kuu Masijala ndogo ya Mtwara, imebariki adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa mkazi wa Masasi mkoani Mtwara, Justine Alex aliyohukumiwa kwa kosa la kumlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka minane.

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo katika hukumu iliyotolewa na Jaji Martha Mpaze, Julai 22, 2024 baada ya kutupilia mbali rufaa ya Justine aliyoikata kupinga hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Masasi.

Jaji amefikia uamuzi huo baada ya kupitia hoja za pande zote na kuwa kesi upande wa mashtaka ilithibitishwa bila kuacha shaka, hivyo rufaa hiyo haina mashiko na kuitupilia mbali.

Mahakama ya Wilaya ya Masasi ilimtia hatiani Justine katika kesi ya jinai namba 81/ 2023, baada ya kushawishika na ushahidi wa mashahidi sita wa upande wa mashtaka.

Ushahidi huo ni pamoja na wa mtoto huyo aliyekuwa akisoma darasa la pili katika Shule ya Msingi Mpowoea, akieleza namna Justine alivyomlawiti.

Katika kesi ya msingi, Justine alidaiwa kumwingilia kinyume na maumbile mtoto huyo Julai mosi, 2023 kinyume na kifungu cha 154(1)(a) na (2) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Akitoa ushahidi mahakamani hapo, mama wa mtoto huyo alidai siku ya tukio alimuona mwanaye akitembea kwa shida na alipomuuliza kama anaumwa alikataa, lakini hakuridhika na majibu hayo na ndipo alimjulisha baba wa mtoto kumchunguza.

Ilidaiwa baada ya baba kumchunguza mtoto huyo, alimjulisha mkewe kuwa mtoto wao ameingiliwa kinyume na maumbile na kulikuwa na michubuko.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mtoto huyo alimtaja Justine na ushahidi wa daktari aliyemchunguza alibaini kukuta michubuko na uvimbe katika sehemu ya haja kubwa.

Ilidaiwa siku ya tukio, mtoto huyo alikuwa akicheza mchezo wa bao na marafiki zake wawili na Justine alipofika aliwataka watoto hao waongozane naye wakakate kuni, lakini watoto hao walikataa.

Mtoto huyo alidai alikubali kuongozana naye na wakiwa njiani alimfunga mikono kwa kamba akamsukuma chini, akamvua suruali na kumfanyia kitendo hicho na alipomaliza alimwachia na kumtaka aende nyumbani.

Kutokana na maelezo ya mtoto huyo, baada ya kukaguliwa na baba yake, alipelekewa kituo cha polisi, kisha hospitali alikofanyiwa uchunguzi na kubainika amelawitiwa.

Katika utetezi wake, Justine alidai alishangaa kukamatwa Julai 2, 2024 na watu wawili waliofika nyumbani kwake wakimweleza anahitajika kituo cha polisi Ndanda, lakini alipouliza kwanini alielezwa atajulishwa akifika kituoni.

Alidai akiwa kituo cha polisi alikumbana na mateso na kulazimishwa kukiri kosa hilo na kuwa alifikishwa mahakamani kwa kosa ambalo hakutenda.

Hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili alihitimisha kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kesi bila kuacha shaka, kumtia hatiani Justine na kumhukumu kifungo cha maisha jela.

Katika rufaa hiyo ya jinai namba 12409/2024, Justine aliwasilisha hoja nne za rufaa zilizotengeneza misingi miwili ya rufaa ambazo ni upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi yao bila kuacha shaka yoyote na Mahakama ilishindwa kuzingatia utetezi wake.

Katika rufaa hiyo, Justine alijitetea mwenyewe, huku upande wa mjibu rufaa ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Florence Mbamba aliyepinga vikali hoja ya kesi ya mashtaka kushindwa kuthibitisha kesi na kuwa kesi ilithibitishwa.

Wakili huyo alidai ushahidi wa shahidi wa pili ambaye ni mtoto huyo ulieleza wazi kilichojiri kati yake na Justine walipokuwa msituni.

Alieleza ushahidi bora na muhimu katika kesi za makosa ya kujamiiana ni kutoka kwa mwathirika wa tukio husika ambaye katika kesi hiyo uliungwa mkono na daktari aliyemchunguza.

Kuhusu kutozingatiwa utetezi, wakili huyo alieleza Mahakama ya awali ilizingatia utetezi wa Justine, akielekeza kwenye ukurasa wa nne na tano wa hukumu, hivyo kuiomba Mahakama kufuta rufaa hiyo kwani haina mashiko.

Katika majibu yake, Justine alieleza kesi haikuthibitishwa bila kuacha shaka, akirejea ushahidi wa mwathirika huyo aliyeeleza kumjulisha dada yake na baba yake kuhusu aliyemfanyia kitendo hicho, lakini hawakufika mahakamani kutoa ushahidi.

Jaji Martha baada ya kusikiliza hoja za pande zote huku akinukuu mashauri mbalimbali yaliyowahi kutolewa uamuzi na Mahakama ya Rufani, alieleza ushahidi unatosha kuwa mwathirika huyo alilawitiwa na alieleza namna Justine alivyomlawiti msituni.

“Kulingana na ushahidi kuhusu nani alitenda kosa lisilo la kawaida dhidi ya mwathirika, ni wazi Justine ndiye mhusika, hakuna dalili au dalili zinazoonyesha huenda kesi hiyo ilitungwa dhidi yake,” alieleza Jaji.

Jaji Martha alieleza kutokana na hayo, haoni kushindwa kuitwa kwa baba na dada wa mwathirika huyo kunadhoofisha kesi, hivyo anaona malalamiko hayo hayana msingi na kukubaliana na hoja ya wakili wa Serikali kuwa mashtaka walithibitishwa.

Kuhusu hoja ya  kushindwa kuzingatiwa utetezi wa Justine, Jaji alieleza mbali na muhtasari wa ushahidi wa pande zote mbili, ameona kuwa wakati akichambua masuala hayo kwa ajili ya uamuzi, hakimu aliegemea ushahidi wa upande wa mashtaka tu.

“Hata hivyo, katika kujadili kama Justine alitenda kosa nilizingatia utetezi wake na baada ya tathmini ya kina, niligundua hauleti shaka yoyote kuhusu kesi ya mashtaka ambayo ingenifanya nifikie uamuzi tofauti.

 “Kwa sababu zilizoainishwa, naona rufaa haina mashiko na hivyo naitupilia mbali kwa ujumla wake,” alieleza.

Related Posts