Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeamuru mshtakiwa Hamisi Luongo, anayetuhumiwa kumuua mkewe kisha kuteketeza mwili kwa moto kwa kutumia gunia zima la mkaa, akafanyiwe uchunguzi wa afya ya akili.
Awali, kabla Mahakama haijatoa amri hiyo, mshtakiwa alipinga hoja ya upande wa mashtaka ya kufanyiwa uchunguzi, akidai hayuko tayari kwenda huko kwa kuwa ana akili timamu na hana rekodi ya matatizo ya akili.
Ameieleza Mahakama kuwa, anashangaa kushtakiwa kwa tuhuma za kumuua mkewe ambaye yuko hai, hata hivyo, hakueleza ni wapi alipo.
Jaji Elizabeth Mkwizu jana Jumatano Julai 24, 2024 alitoa amri mshtakiwa akapimwe afya ya akili kutokana na maombi ya wakili wa mshtakiwa, Mohamed Majaliwa ambaye yaliungwa mkono na waendesha mashtaka kesi ilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji.
Luwongo, mkazi wa Gezaulole wilayani Kigamboni, Dar es Salaam anakabiliwa na kesi ya mauaji ya mkewe Naomi Marijan, kinyume cha vifungu vya 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kana ilivyorejewa mwaka 2019, akidaiwa kutenda kosa hilo Mei 15, 2019.
Aliposhikiliwa na Jeshi la Polisi alituhumiwa kumuua mkewe na kuteketeza mwili wake akitumia gunia zima la mkaa, kisha akazika majivu shambani na kupanda mgomba mahali alipoyazika.
Wakili Majaliwa Septemba 6, 2023, alitoa ombi mshtakiwa akapimwe afya ya akili aliposomewa maelezo ya awali ya kesi inayomkabili mbele ya Jaji Mussa Pomo.
Aliwasilisha ombi hilo la uchunguzi akidai mteja wake anatarajiwa kujitetea, akili yake haikuwa sawa alipotenda kosa hilo.
Jaji Pomo hakutoa amri hiyo. Kesi baadaye ilihamishiwa kwa Jaji Mkwizu.
Kesi ilipangwa Julai 24, kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa Mahakama kupokea ushahidi wa upande wa mashtaka.
Baada ya utambulisho wa mawakili wa pande zote, mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali, Mwasiti Ally alieleza walikuwa tayari kuendelea na ushahidi.
Pia, alikumbusha kuhusu ombi la upande wa utetezi la mshtakiwa kufanyiwa uchunguzi wa akili akieleza wanaliunga mkono.
“Tunaomba Mahakama iridhie ombi la kufanya uchunguzi wa akili ya mshtakiwa wakati wa tukio ili kutenda haki,” ameomba.
Wakili Majaliwa aliunga mkono akieleza kulingana na mazingira usikilizaji wa shauri hilo hauwezi kuendelea mpaka ombi hilo litakapotekelezwa na matokeo ya uchunguzi kuwasilishwa mahakamani.
Kabla ya Mahakama kutoa uamuzi, mshtakiwa aliomba kuzungumza pasipo kupitia kwa wakili.
Jaji alipomuhoji Wakili Majaliwa, aliridhia apewe fursa.
Mshtakiwa alipinga hoja ya kwenda kupimwa akili akieleza hata mkewe anayedaiwa kumuua yuko hai.
“Mheshimwa Jaji niko timamu, nina akili timamu kwa asilimia 100. Sina tatizo la akili na haya yanayoendelea hapa mimi siyaelewi. Siko tayari kupelekwa huko wanakosema,” amesema mshtakiwa na kusisitiza:
“Siko tayari kabisa kwani sina rekodi zozote za tatizo la akili. Wakili wangu namkubali sana lakini katika hili namuomba akae pembeni katika kesi yangu.”
Jaji Mkwizu alilazimika kumtuliza na kumfafanulia kwa upole kuhusu hoja hiyo, akimtoa wasiwasi kuwa mahakamani ndiko mahali salama na pa haki.
“Mshtakiwa unaweza kunisikiliza na mimi kidogo?” Jaji Mkwizu alimuuliza mshtakiwa, ambaye alikubali kumsikiliza.
“Relax (tulia), mahakamani ndiyo sehemu salama na sehemu ya kutenda haki. Sheria aliyoizungumzia wakili wa Serikali ni kwa sababu kuna ombi la kwenda kuchunguzwa akili yako, si kwa wakati huu bali kwa wakati wa kutenda tukio hilo kama ulikuwa na akili sawasawa, si kwa sasa,” amesema Jaji Mkwizu.
Alimweleza madakatari ndio pekee wanaoweza kujua kama wakati huo alikuwa katika akili yake ya kawaida au haikuwa sawa.
“Kwa hiyo hatukuangalii kwa leo bali wakati ule wa kutenda kosa hilo,” amesisitiza Jaji Mkwizu akimpa mfano kuwa hata sasa akivua nguo (mshtakiwa) akatembea uchi ikiwa wakati wa kutenda kosa hilo alikuwa na akili timamu basi sheria itachukua tu mkondo wake.
Jaji Mkwizu amesema Mahakama haiwezi kumpeleka tu huko mtu bila sababu ya msingi na kuwa, hiyo ni kwa ajili ya ulinzi wake.
Baada ya maelezo ya Jaji Mkwizu, mshtakiwa akaanza kutoa utetezi kuhusu madai ya kukiri kutenda kosa hilo, akidai hata yeye kosa analotuhumiwa halikutendeka kwa kuwa mkewe anayetuhumiwa kumuua hajafa.
“Mheshimiwa kuna jambo kwamba si kila mtu anayekiri kosa ametenda kosa, wengine wanaamua tu kukiri kwa sababu fulanifulani ama kwa kuteswa. Mfano kosa ambalo ninatuhumiwa, kama ingekuwa limetendeka…”
Kabla hajamaliza sentensi hiyo, Jaji Mkwizu alimkatiza na kumweleza anakoelekea kwa sasa si wakati wake na kwamba, hayo yataangaliwa wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa mashtaka wataeleza ni kwa nini wanasema kuwa ametenda kosa hilo.
Hata hivyo, mshtakiwa aliendelea kukana kosa akidai:
“Hata huyo mke wangu anayedaiwa kuwa amefariki, hajafa, sasa hili ni jambo la kushangaza kabisa kuwa ninashtakiwa kwa kumuua mke wangu.”
Baada ya mshtakiwa kutoa maelezo hayo, Jaji Mkwizu alitoa amri akieleza amepitia ombi linalotokana na hoja iliyotolewa Septemba 6, 2023 wakati wa usikilizwaji wa awali, kuwa mshtakiwa achunguzwe kuhusu utimamu wa akili wakati wa kutenda tukio hilo.
Amesema kwa kuwa hilo ni jambo la kisheria na wasiwasi huo umeonyeshwa pia na upande wa mashtaka hakuna namna ambayo Mahakama inaweza kujiridhisha na hali ya akili ya mshtakiwa isipokuwa tu, kwa kufanyiwa uchunguzi wa vipimo vya madaktari.
“Kwa mazingira hayo, Mahakama inaridhika na kutoa amri kuwa mshtakiwa atakuwa chini ya uangalizi katika Taasisi ya Afya ya Akili Isanga kwa ajili ya uchunguzi wa akili yake, chini ya kifungu cha 219 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai,” amesema Jaji Mkwizu.
Pia, ametoa maelekezo kwa ofisa afya wa taasisi hiyo kutekeleza wajibu huo kama ilivyoelekezwa.
Ameahirisha kesi hiyo hadi tarehe itakayopangwa na Msajili wa Mahakama kwa ajili ya kuendelea na taratibu nyingine kulingana na matokeo ya uchunguzi yatakayowasilishwa mahakamani.
Jaji Mkwizu ameamuru mshtakiwa kuendelea kuhifadhiwa mahabusu kusubiri kukamilika kwa taratibu hizo.
Kwa mujibu wa maelezo ya awali ya kesi aliyosomewa mshtakiwa, katika ndoa yao yeye na mkewe walipata mtoto mmoja, Grecious.
Mei 19, 2019 mshtakiwa alitoa taarifa Kituo cha Polisi Mji Mwema na maeneo mbalimbali ikiwamo kwa ndugu wa marehemu kuwa, mkewe alikuwa ameondoka kwenda kusikojulikana na kumwacha mtoto kuanzia Mei 15, 2019.
Julai 16, katika Kituo Kikuu cha Polisi, akihojiwa mshtakiwa alikiri kumshambulia na kumuua mkewe Mei 15, 2019 ndani ya nyumba yao kisha akauchukua mwili wake na kwenda kuuchoma moto katika banda lililikuwa limeandaliwa kwa kutumia mkaa na vitu vingine alivyokuwa ameviandaa.
Alidai majivu na masalia mengine aliyachukua kwa kutumia gari lake aina ya Subaru Forester lenye namba za usajili T 206 CEJ mpaka shambani kwake Kijiji cha Marogoro, wilayani Mkuranga mkoani Pwani.
Huko aliyazika kwenye mashimo yaliyokuwa yameandaliwa na kapanda migomba.
Siku hiyohiyo, aliongozana na maofisa wa polisi na wengine mpaka eneo la tukio (nyumbani) na shambani ambako ofisa kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali alichukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba (DNA).
Matokeo ya uchunguzi wa sampuli hizo yalionyesha majivu yalikuwa ya binadamu ambayo yalioana na baadhi ya ndugu wa marehemu Naomi.
Maelezo ya ziada yalichukuliwa kutoka kwa mshtakiwa na mlinzi wa amani (Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo), baadaye mshtakiwa alipandishwa kizimbani na kusomewa kosa la mauaji.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.