Unguja. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi linamshikilia mtuhumiwa Marco Daud Zagamba (32) mkazi wa Mbweni kisiwani humo kwa tuhuma za kujipatia Sh6 milioni kwa njia za udanganyifu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 25, 2024 ofisini kwake Madema, Kaimu Kamanda wa mkoa huo, Abubakar Khamis Ally amedai kuwa mtuhumiwa huyo amewatapeli watu watano akidai ni mtumishi wa umma na atawapatia ajira katika vikosi vya maalumu vya SMZ.
“Katika hatua nyingine Julai 22, 2024 katika eneo la Maisara Zanzibar, mtuhumiwa huyo alimtapeli mtu mmoja Sh1.4 milioni akidai yeye ni mtumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) na atamsaidia kumpatia ajira kwenye idara hiyo,” amesema Abubakar.
Amesema kuwa mtuhumiwa huyo amefanya matukio ya utapeli kwa muda mrefu akitumia mbinu ya kuwa karibu na ofisi za Serikali ili kuwaaminisha anaowatapeli ni mtumishi wa taasisi hizo na akifanikiwa hutoweka.
Pia, amewataka wananchi wote waliopatwa na kadhia ya kutapeliwa, wafike kituo cha Polisi Madema ili kumtambua mtuhumiwa huyo.
Sambamba na hilo, Kamanda Abubakar amesema matukio ya wizi wa pikipiki yamekuwa yakiripotiwa katika vituo vya Polisi ambalo limefanya ufuatiliaji na kuwakamata watuhumiwa watatu ambao wamekiri kuiba pikipiki 21 kwa kipindi cha miezi sita mwaka huu.
“Baada ya kufanya mahojiano na watuhumiwa hao tulifanikiwa kuzipata pikipiki nne na walieleza kuwa wanapoiba husafirisha kupeleka jijini Dar es salaam na tulimfuatilia mpokeaji wa mali hizo na kufanikiwa kumkamata maeneo ya Mbagala,” amesema Abubakar.
Amewataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Rashid Cosmas John (21), Idd Abdallah Suleiman (20) wote wakazi wa Kidimni, Mussa Khamis Maroda (24) mkazi wa Mwera na Suleiman Ramadhan Mwinyi (24) ambaye anapokea pikipiki hizo kutoka Zanzibar.
Amewataka wamiliki wa vyombo vya moto kuwa waangalifu kwa kuhakikisha vyombo hivyo vinakuwa sehemu salama, kwani baadhi ya wamiliki huviacha bila uangalizi.
Amesema Jeshi la Polisi limeendelea kufanya operesheni na misako mbalimbali ili kuzuia na kupambana na uhalifu ambapo jumla ya kesi 180 wahusika wamekutwa na hatia na kuhukumiwa kutumikia adhabu kama vile vifungo, kulipa fidia na faini.
Katika hatua nyingine Kamanda Abubakar amesema kipindi hiki ambacho Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Camillus Wambura ametangaza usaili kwa vijana walioomba ajira za Jeshi la Polisi, watu wanapaswa kuchukua tahadhari dhidi ya matapeli ambao wanatumia fursa hiyo ili kujipatia kipato kwa njia isiyo halali.