Askofu Kasala ataka INEC kuongeza siku za uandikishaji wapigakura

Geita. Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Flavian Kasala ameonyesha wasiwasi kwa siku saba zilizotengwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuboresha daftari la wapigakura katika mikoa ya Geita na Kagera kama zitatosha kuwaandikisha wananchi wote wenye sifa.

INEC itaanza mzunguko wa pili wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura itakayojumuisha mikoa ya Geita na Kagera kuanzia Agosti 5 hadi 11, 2024.

Akizungumza kwenye mkutano wa INEC na wadau kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura uliofanyika jana Julai 24, 2025 mjini Geita, Askofu Kassala ameshauri siku hizo ziongezwe, ili wote wenye sifa wafikiwe.

“Tumeona hapa kusajili mtu inachukua muda na watu wanaweza kuwa wengi na mmetoa siku saba ambazo zinaweza kumalizika kabla ya watu wote kufikiwa je, kuna mbadala wake ili watu watakaokosa haki hiyo ya kujiandikisha na kuboresha taarifa zao?”amehoji Askofu Kassala.

Amesema lipo kundi kubwa la vijana ambao uandikishaji wa daftari mwaka 2020 hawakuwa na sifa kutokana na umri na kuwa kama viongozi wa dini, ni wakati wao kuhamasisha kundi hilo kujitokeza kwa wingi kujiandikisha pamoja na wananchi wengine, ili wawe na sifa ya kupiga kura kwenye chaguzi zijazo.

Akizungumzia jambo hilo, Tausi Salehe, mkazi wa Geita amesema siku zilizotolewa na INEC zitatosha endapo waliopewa kazi ya kuandikisha wataifanya kwa haraka na weledi kulingana na idadi ya wanaofika kujiandikisha.

Akizungumzia hoja ya Askofu Kassala, Mwenyekiti wa Tume, Jaji Jacobs Mwambegele amesema kwa uzoefu walionao katika uandikishaji wapigakura, siku hizo zinatosha kutokana na vituo vilivyopo na kwamba uandikishaji huo ni kwa wale ambao hawakuandikishwa kwenye daftari mwaka 2020 na wale wanaoboresha taarifa zao.

Mkurugenzi wa Tume, Ramadhani Kailima amesema ipo timu ya kutosha ya waandikishaji na ikibainika kuna kituo kimeelemewa na siku zimebaki chache, kitaongezewa nguvu ya waandikishaji, ili kuhakikisha wote wenye sifa wanapata nafasi ya kuijiandikisha.

Akizungumzia idadi ya wapigakura, mkurugenzi huyo ameeleza kwa Mkoa wa Geita wanatarajia kuandikisha wapigakura wapya 299,672 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 24.7 ya wapigakura milioni 1.2 waliopo kwenye daftari hilo.

Kuongezeka kwa idadi hiyo kunauwezesha mkoa huo kuwa na wapigakura zaidi ya milioni 1.5.

Kailima amesema idadi hiyo inaweza kuongezeka endapo kutakuwa na watu waliokuwa na sifa za kuandikishwa mwaka 2019/20 na hawakujiandikisha.

Amesema tayari tume imefanya maandalizi kwa kutambua vituo 1,637 vitakavyotumika kwenye uboreshaji na kwa mwaka huu  vituo vipya 68 vimeongezeka  kutoka vituo 1,569 zilivyotumika kwenye uboreshaji wa mwaka 2019/20.

“Kwa nchi nzima tuna vituo 40,126 vya kuandikisha wapigakura ambavyo vitatumika katika uboreshaji wa daftari 2024 na vituo hivi 39,709 vipo Tanzania Bara na 417 vipo Zanzibar. Hili ni ongezeko la vituo 2,312 ikilinganishwa na vituo 37,814 vilivyotumika 2019/2020,” amesema Kailima.

Pamoja na hilo, amesema vyama vya siasa vina nafasi kubwa ya kuhamasisha watu kujitokeza kujiandikisha na kuwataka viongozi wa vyama hivyo kutumia muda huu kufanya hivyo.

Katika hatua nyingine, Kailima ameyataka makundi ya vijana kujitoa kujiandikisha pamoja na kutoa hamasa kwa vijana wenzao kwa kutumia mitandao ya kijamii, vikundi na majukwaa yao.

Pia ametoa wito kwa viongozi wa dini kutumia siku za ibada kuhamasisha waumini wao kujiandikisha kwenye daftari la wapigakura sasa badala ya kusubiri awamu nyingine itakayofanyika Aprili 2025.

Related Posts