Dar es Salaam. Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson amemuapisha Balozi Mahmoud Thabit Kombo kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku akieleza kwa nini ameapishiwa jijini Dar es Salaam.
Balozi Kombo ameapishwa leo Alhamisi Julai 25, 2024, Ofisi Ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku tano zimepita tangu alipoteuliwa kuwa Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Rais Samia Suluhu Hassan Julai 21, 2024.
Akizungumza baada ya kumuapisha, Dk Tulia amempongeza kwa kuaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kupewa nafasi ya ubunge, huku akisema zipo chache hivyo yeye kuwa miongoni mwao ni heshima kubwa.
“Tukio hili ambalo tumelikamilisha hapa ni kiapo cha uaminifu ambacho kinamfanya Balozi Kombo kuwa mbunge kwa matakwa ya ibara ya 68 ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na kwa mujibu wa kanuni za Bunge za kudumu.
Kanuni ya 30 fasili ya kwanza ambayo inaeleza kabla ya mbunge kuanza kushiriki kanuni za Bunge lazima ale kiapo cha uaminifu mbele ya Spika,” amesema Dk Tulia.
Amesema fasili ndogo ya 2(b) inaleza mbunge ataapishwa na Spika kwa mujibu wa eneo ambalo litapangwa na Spika huku akisema awali kulikuwa na changamoto jambo ambalo lilifanya kanuni zibadilishwe.
“Tulilazimika kutoa ufafanuzi huu kila wakati ili watu wasione kwa nini wabunge wengine wanaapishwa bungeni wengine nje ya Bunge, kanuni zetu zinaruhusu hayo mazingira na Spika akiagiza wapi kiapo kitafanyika hapo, leo tumefanyia ofisi ndogo za Bunge hapa Dar es Salaam lakini ingeweza kufanyika sehemu nyingine yoyote,” amesema Dk Tulia.
Dk Tulia amesema anaamini Balozi Kombo na wengine walioteuliwa watakwenda kufanya kazi na kuendeleza mipango ambayo imewekwa wazi na Rais ikiwemo uhusiano wa kimataifa na Afrika Mashariki.
“Tumeona familia ipo hapo nyuma tunaamini wapo tayari kukuunga mkono katika majukumu haya mapya,” amesema Dk Tulia.
Mbali na kuwa Mbunge, Rais Samia alimteua Balozi Kombo kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kabla ya uteuzi huo, Balozi Kombo alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia.
Kombo aliteuliwa kuchukua nafasi ya January Makamba ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.
Pia Balozi Kombo aliteuliwa kuwa Mbunge ikiwa ni saa chache tangu aliyekuwa Mbunge wa kuteuliwa na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amuandikie Spika barua ya kujiuzulu ubunge.
Kwa mujibu wa barua hiyo, Balozi Mbarouk alisema sababu ya uamuzi huo ni changamoto za kijamii zinazomkabili.
“Ninalazimika kuchukua uamuzi wa kujiuzulu, ili nipate nafasi ya kushughulikia changamoto hizo,” inaleza sehemu ya taarifa ya Bunge kwa umma iliyotolewa Jumapili ya Julai 21, 2024, ikinukuu barua ya Balozi Mbarouk.
Balozi Mbarouk ambaye pia alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki aliteuliwa Aprili, 2021 kuwa mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kwa sasa nafasi yake imechukuliwa na Cosato Chumi aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.