Dabo atangaza vita mpya | Mwanaspoti

Azam FC kesho inatarajiwa kushuka tena uwanjani kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Union Touarga ya Morocco, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Youssouph Dabo akisema licha kuendelea kuwepo nchini wakati kikosi hicho kikiwa kambini nchini huko kwa ajili ya maandalizi ya msimu (Pre season), bado haitoathiri programu walizoziandaa akishirikiana na wenzake.

Azam imeweka kambi Morocco baada ya kuanza jijini Dar es Salaam kisha Zanzibar ilipocheza mechi moja dhidi ya Zimamoto na kushinda mabao 4-0 kabla ya kucheza ikiwa ughaibuni na US Yacoub Mansour na kuilaza mabao 3-0 na kesho itamalizana na Touarga na kuiaga kambi kwa kucheza na Wydad AC Jumatatu.

Kocha Dabo yupo jijini Tanga kwa ajili ya kuendelea na kozi ya ukocha wa CAF ‘A’ Diploma iliyoanza Julai 23, itakayomalizika Agosti Mosi mwaka huu, ambayo itampa nafasi ya kutambulika rasmi kama kocha mkuu na sio msaidizi na alizungumza na Mwanaspoti alisema kutokuwepo kwake Morocco sio ishu sana.

“Benchi letu la ufundi linaendelea na maandalizi ya msimu na licha ya kukosekana kwangu ila tulishapanga taratibu zote na makocha wenzangu za kuhakikisha hakuna kitakachoharibika wakati wote wanapoendelea na kambi yetu Morocco,” alisema Dabo.

Kocha huyu aliongeza, hata kama itashindikana kurudi tena Morocco kuungana na kikosi hicho, ila ataisubiria Dar es Salaam huku akiamini kambi hiyo itakuwa na tija kubwa, wakati huu wakijipanga kwa ajili ya mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii.

“Sioni tatizo kama itashindikana kuungana na timu Morocco kwa sababu kama nilivyosema awali, tulishapanga kila kitu na kipo katika mstari mzuri, malengo yetu makubwa ni kufanya vizuri zaidi msimu ujao hivyo hilo ndilo jambo kubwa kwetu.”

Azam itakaporejea nchini itakuwa na kibarua kigumu cha kupambana na Coastal Union, katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii, utakaopigwa Agosti 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar kuanzia saa 10:00 jioni.

Related Posts