Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Iran Nasser Kanani ameandika kwenye mtandao wa X :
” Watoto wa Kipalestina wanauawa kila siku na muuaji wa Tel Aviv, na baada ya uhalifu wote huu, serikali na Bunge la Marekani wanamkaribisha muuaji huyu kwa kumshangilia. Waziri mkuu wa uhalifu na wa utawala feki anakumbatiwa na wafuasi wake baada ya miezi tisa ya mauaji ya halaiki na mauaji ya watoto wachanga.”
Matamshi hayo yametolewa baada ya Netanyahu kuitolewa wito Marekani kuungana na Israel ili kukabiliana na kile alichokitaja kuwa “mhimili wa ugaidi” wa Iran, akidai kuwa Tehran inahusika na karibu mauaji yote yanayochechewa na imani za kidini katika eneo la Mashariki ya Kati.
Mashambulizi yaendelea kuripotiwa Gaza
Watu kadhaa wameripotiwa kuuawa leo Alhamisi huku wengine wakijeruhiwa kufuatia mashambulizi ya Israel huko Gaza. Hayo yanajiri wakati Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu bado yuko nchini Marekani, katika ziara ambayo imelaaniwa vikali na Iran.
Maeneo mbalimbali hasa ya kusini mwa Ukanda wa Gaza katika miji ya Rafah na vitongoji vya al-Qarara karibu na Khan Younis, yameshuhudia mashambulizi makali ya Israel.
Soma pia:Vita vyaendelea Gaza, mchakato wa mazungumzo wakwama
Watu wasiopungua 30 wameripotiwa kuuawakatika kipindi cha saa 24 zilizopita, na hivyo kupelekea idadi ya vifo kufikia watu 39,175, hii ikiwa ni kulingana na taarifa za Wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas. Areej Abu Alyan, ni mkimbizi wa ndani:
“Tuliyakimbia makombora waliyotufyetulia, miili ya mashahidi na majeruhi ilikuwa imetapakaa kila mahali. Kwa sasa tuko mitaani bila makazi na hatujui pa kwenda. Hatukuweza hata kuchukua nguo za watoto.”
Netanyahu aapa kuendelea na vita Gaza
Kuendelea kwa mashambulizi hayo kunajiri wakati hapo jana waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alipolihutubia Bunge la Marekani, aliahidi kuviendeleza vita hivyo hadi atakapo litokomeza kabisa kundi hilo la wanamgambo wa Kipalestina linalozingatiwa na Umoja wa Ulaya, Marekani, Ujerumani na mataifa kadhaa ya magharibi kama kundi la kigaidi.
Hayo yakijiri, kundi la kuwatetea mateka wa Israel ambao bado wanashikiliwa huko Gaza, limetaja kuridhishwa na hatua ya serikali ya Israel kupata miili ya mateka watano lakini likadai kuwa kuna “hujuma” zinazofanyika ili kukwamisha juhudi za kuwakomboa mateka wengine waliosalia.
Soma pia: Netanyahu aapa kuendelea na vita Gaza
Katika hatua nyingine, Netanyahu aliyeapa kuendelea na vita vya Gaza, atakutana na rais Joe Biden na makamu wake Kamala Harris, huku akisisitiza umuhimu wa Washington kuendelea kuisaidia kijeshi ili kukabiliana na Hamas na kusisitiza kuwa ushindi wa Israel ni wa Marekani pia.
Ziara ya Netanyahu nchini Marekani imekosolewa na baadhi ya wabunge wa chama cha Democratic lakini pia mamia ya waandamanaji walikusanyika nje ya Bunge la Marekani huku wakiwa na mabango yaliyosomeka kuwa “Netanyahu ni mhalifu wa kivita.”
Vyanzo: (AP, RTRE, DPAE, AFP)