Geita Gold imethibitisha kumalizana na Amani Josiah kuwa kocha mkuu wa timu hiyo kwa mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuendelea kama ataipandisha Ligi Kuu, huku Choki Abeid akiwa msaidizi wake.
Geita inayojiandaa na Ligi ya Championship baada ya kushuka daraja imeshinda vita ya kumpata Amani Josiah aliyekuwa anawaniwa na Stand United, Biashara na Songea United na atasaidiana na Choki Abeid aliyekuwa kocha wa U-20.
Josiah kwa sasa anaendelea na masomo ya leseni ya Diploma A ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) jijini Tanga pamoja na aliyekuwa kocha msaidizi, Lucas Mlingwa chini ya Denis Kitambi, ambaye atapangiwa majukumu mengine na klabu hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mkurugenzi wa Mashindano Geita Gold, Liberatus Pastory alisema ofa nzuri waliyompa Josiah imemshawishi na kuungana nao kuirejesha timu hiyo Ligi Kuu, huku mipango ya usajili ikiendelea kwa usiri mkubwa.
“Tumemleta Amani Josiah kwa mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuendelea endapo tutafikia malengo ya kupanda daraja kwahiyo atasaidiana na Choki Abeid. Usajili unakwenda vizuri asilimia 85 umekamilika bado 15,†alisema Pastory.
“Kocha ana mapendekezo yake ana wachezaji wengi anawafahamu na sisi tuna ya kwetu tunamshirikisha tunashauriana, tulimtambulisha Yusuph Mhilu pekee kwa sababu tumekubaliana tukianza kutambulisha tutambulishe wote kwa pamoja.
“Mwishoni mwa wiki hii ama wiki ijayo tutaweka wazi usajili wetu, tunawaomba mashabiki waendelee na utulivu walionao kilichotokea ni bahati mbaya hakuna aliyetarajia, tumejipanga kama tulivyofanya wakati ule tunapanda daraja,†alisema Pastory.