Kilichowang’oa vigogo wa taasisi Wizara ya Habari

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutengua uteuzi wa wenyeviti na watendaji wakuu wa taasisi tatu zilizo chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, inadaiwa huenda wameponzwa na salamu za shukurani zilizotolewa.

Julai 21, 2024 Rais Samia Suluhu Hassan alipotengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, Nape Nnauye na kumteua Jerry Silaa kujaza nafasi hiyo, saa chache baadaye taasisi hizo zilitoa salamu za shukuran kwa Nape na kumtakia kila la heri katika majukumu yake.

Taasisi hizo ni Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Shirika la Posta Tanzania na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).

Jioni ya Julai 23, Rais Samia kupitia taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka alitengua uteuzi wa Zuhura Muro aliyekuwa Mwenyekiti wa bodi ya TTCL na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Peter Ulanga.

Wengine ambao uteuzi wao ulitenguliwa ni aliyekuwa Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi Shirika la Posta, Brigedia Jenerali mstaafu Yohana Ocholla na Postamasta Mkuu wa shirika hilo, Maharage Chande.

Dk John Nkoma, aliyekuwa Mwenyekiti wa bodi ya UCSAF na aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Justina Mashiba nao uteuzi wao ulitenguliwa.

Kwa mujibu wa wadau waliozungumza na Mwananchi jana, salamu za shukurani zilizotolewa hata kama ni kwa nia njema, ziliashiria kudharau mamlaka ya Rais au kutoridhishwa na uamuzi uliofanyika.

Mwanataaluma wa sheria ambaye ni wakili wa kujitegemea, Bashir Yakub amesema huenda uamuzi wa Rais kuwaondoa kwenye nafasi zao wenyeviti na watendaji hao wa taasisi unatokana na salamu za shukurani zilizotolewa kwa aliyekuwa waziri wao.

“Inawezekana ikaonekana ni jambo la kawaida ila kiutawala na utumishi wa umma ujumbe waliotoa ni kama walitaka kuonyesha Rais amekosea kutengua uteuzi wa waziri. Ni kama walitaka kuonyesha ameondolewa mtu sahihi,” amesema.

Mwanasheria huyo amesema, “tukio la aina hii halijawahi kutokea, haiwezekani Rais atengue uteuzi wa kiongozi halafu taasisi iandike salamu za shukurani kwa kiongozi huyo na kumtakia heri katika majukumu yake mengine. Ni kama hawajaridhishwa na uamuzi wa kumuondoa.”

Hata hivyo, amesema upo uwezekano wenyeviti na watendaji hao si wahusika wa moja kwa moja wa salamu hizo, lakini kwa kuwa wao ndio viongozi wanapaswa kuwajibika.

“Utenguzi wa waziri ulitokea saa tano usiku, kesho yake asubuhi taasisi inatoa salamu za shukurani siamini hata kama bodi au menejimenti zilikaa kuamua watoe salamu hizo, inawezekana hayo yamefanywa na vitengo vya habari lakini kwa kuwa wao ndio watendaji wakuu hakuna namna watakwepa kuwajibika,” amesema.

Maoni hayo hayatofautiani na kilichoelezwa na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Kristomus anayesema taasisi hizo kumshukuru waziri ambaye uteuzi wake umetenguliwa ni dhihaka kwa mamlaka ya juu.

Amesema, “kwenye utumishi bosi wako akifanya uamuzi hutakiwi kupingana nao, sasa kitendo cha taasisi kumshukuru waziri aliyetenguliwa ni kama ujumbe wa kumdhihaki Rais kwa kumuondoa mtu ambaye wao wanamuona anafaa.”

“Walichokifanya ni kama kuonyesha waziri alionewa ingawa inawezekana kuna mengine yanaendelea chini kwa chini. Kwa kilichotokea inaweza kuchukua muda kwao kurudi kwenye mfumo au labda hadi pale kiongozi aliye madarakani atakavyoamua,” amesema.

Mtaalamu wa masuala ya rasilimali watu na utawala aliyeomba hifadhi ya jina lake, amesema taasisi hizo zilifanya kosa kutoa salamu kwa waziri kwa sababu huenda zinahusika katika kilichosababisha aondolewe kwenye nafasi hiyo.

“Inaonekana kizazi cha sasa hakifahamu mamlaka ya Rais. Yeye ndiye anayeteua na kutengua, maamuzi yake yanapaswa kuheshimiwa. Kama ametumia mamlaka hayo kumtengua mtu taasisi inapata wapi ujasiri wa kumpongeza mtu huyo.”

“Rais hajaweka wazi sababu ya mabadiliko, huenda haridhishwi na utendaji wa taasisi hizo ndiyo maana akamtoa waziri halafu wao wanakuja kumpongeza, tena bila hata ya kusubiri muda upite. Hii inatafsiriwa kama kejeli kwa kiongozi mkuu wa nchi,” amesema.

Mwanataaluma huyo ambaye ameshuhudia utawala katika awamu zote sita za uongozi nchini, amesema kitendo kama hicho hakijawahi kutokea na imekuwa mara ya kwanza kwa kiongozi aliyeondolewa kwenye mamlaka kupewa salamu za shukurani hadharani.

Amesema hata kama salamu hizo zimetolewa kwa nia njema, hazikutolewa wakati sahihi. Pia amesema kwa utamaduni uliozoeleka mkubwa anapotoa uamuzi huwezi kuhoji.

Related Posts