KONA YA MALOTO: January, Nape: Ilianza kwa Magufuli sasa kwa Samia

Catherine Haddon, raia wa United Kingdom (UK), ni mtaalamu wa uendeshaji wa Serikali. Catherine aliwahi kusema: “Some reshuffles are planned well in advance and some are sudden but, they all have the potential to go off-course.”

Tafsiri yake ni kuwa; “baadhi ya mabadiliko ya baraza la mawaziri hupangiliwa vizuri mapema na mengine hutokea ghafla, lakini yote kwa namna moja au nyingine hufanana kwa Serikali kutoka nje ya mstari.” Yaani, mabadiliko yoyote ya baraza la mawaziri yana athari hasi kwa Serikali.

Nimeanza na nukuu ya Catherine, kuelekea kujenga tafakuri kufuatia Rais Samia Suluhu Hassan, kufanya mabadiliko mengine ya Baraza la Mawaziri. January Makamba, aliingia Baraza la Mawaziri la Rais Samia Septemba 2021, Agosti 2023, akawa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Hivi sasa January siyo waziri. Ametenguliwa.

Nape Nnauye, aliingia Baraza la Mawaziri la Rais Samia Januari 2022, akiwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Baada ya huduma yake ya miaka miwili na miezi sita iliyotimia, ametenguliwa. Nape siyo waziri tena. Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Julai 21, 2024.

Sura namba moja ya kuondoka kwa January na Nape kwenye Baraza la Mawaziri ni kuwa sasa, Rais Samia amejipangusa dhidi ya waliotengwa na mtangulizi wake, Dk John Magufuli. January na Nape, waliondolewa na Magufuli kwenye Baraza la Mawaziri katika nyakati za tamthiliya tata kisiasa.

Nape, alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuanzia Desemba 2015, aliondolewa na Magufuli Machi 23, 2017, baada ya kutofautiana mtazamo juu ya hatua zilizostahili dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Makonda, alituhumiwa kuvamia ofisi za Clouds Media Group (CMG), akiwa na askari wenye mitutu ya bunduki, kisha kulazimisha kurushwa hewani kwa maudhui yaliyokataliwa na uongozi wa Televisheni ya Clouds. Magufuli alitaka Makonda aachwe, Nape alisimama kidete kuhakikisha hatua zinachukuliwa. Akafukuzwa.

Nyakati za tamthiliya tata kisiasa, uliibuka mchezo wa kudukua mawasiliano ya watu, hasa wanasiasa. Sauti za Nape, January, Makamu Mwenyekiti CCM, Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu CCM mwaka 2006 mpaka 2011, Yusuf Makamba, Waziri wa Mambo ya Nje mwaka 2007 mpaka 2015, Bernard Membe, kwa nyakati tofauti walidukuliwa wakimteta Dk Magufuli.

Julai 21, 2019, Dk Magufuli alimweka pembeni January. Baadaye, Nape alionekana Ikulu, Dar es Salaam, ikaelezwa alikwenda kumwomba radhi Dk Magufuli.

Kisha, Dk Magufuli akatoka hadharani na kusema hata January alimwomba msamaha, akatangaza kuwasamehe wote. Pamoja na hivyo, baada ya Uchaguzi Mkuu 2020, Magufuli hakuwarudisha January na Nape kwenye Baraza la Mawaziri.

Hiyo ikaleta tafsiri kuwa January na Nape, walitengwa na Magufuli. Kitendo cha Rais Samia kuwarejesha Nape na January kwenye Baraza la Mawaziri, kilileta tafsiri ya watengwa wa Magufuli kukumbukwa na Mama (Rais Samia). Upo wakati ilielezwa kuwa “watengwa” ndio wenye zamu kwenye urais wa Mama. Mawaziri kadhaa kipindi cha Magufuli, waliwekwa kando. Sasa, watengwa wa Magufuli, wamekuwa watengwa wa Samia.

Kunani Wizara ya Mambo ya Nje?

Kila tafsiri inaweza kuwepo, swali moja litaendelea kutatiza wengi, ni kilichotokea ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Mapema, Julai 21, 2024, Ofisi ya Spika wa Bunge, ilieleza kupokea barua kutoka kwa aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Mbarouk Nassor Mbarouk, kuomba kujiuzulu ubunge, kutokana na matatizo ya kijamii.

Katiba ya Tanzania, ibara ya 55 (4), inatoa sharti kwa Rais kuteua mawaziri na naibu mawaziri miongoni mwa wabunge tu. Kwa mantiki hiyo, kitendo cha Mbarouk kujiuzulu ubunge kilijenga tafsiri ya kujing’oa unaibu waziri.

Siku hiyo hiyo, usiku wake taarifa ya Ikulu ikatoka, ilieleza kumwengua January pamoja na Naibu Waziri mwingine wa Wizara ya Mambo ya Nje, Stephen Byabato. Kwa maana hiyo, bosi wa wizara na wasaidizi wake wawili, wote wameng’oka.

Mbarouk alisema, aliamua kujiuzulu kwa sababu ana matatizo ya kijamii. Taarifa ya Ikulu ikasema, Mbarouk atapangiwa kituo cha kazi. Mbarouk ni balozi. Maneno atapangiwa kituo cha kazi, yanaeleweka kuwa anarejeshwa kwenye uwanja wa diplomasia. Mbarouk alisema ana matatizo ya kijamii.

Je, akipangiwa kituo hayo matatizo ndiyo yataisha?

Dhahiri, kuna jambo halipo sawa Wizara ya Mambo ya Nje. Rais Samia, ana wajibu wa kuueleza umma nini ambacho kimesababisha awaondoe mabosi watatu kwa mpigo, ingawa mmoja amesema atampangia kituo.

Rais Samia, alipoapa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Machi 19, 2021, alimteua Balozi Liberata Mulamula kuwa Waziri wa Mambo ya Nje. Mulamula aliapishwa Machi 31, 2021, lakini akaondolewa Oktoba 3, 2022. Akafuata Stergomena Tax, ambaye Agosti 31, 2023, alimpisha January, kisha yeye akahamia Wizara ya Ulinzi.

Kihistoria, Wizara ya Mambo ya Nje haina utamaduni wa mawaziri wake kubadilishwa mara kwa mara. Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa, alidumu na Waziri wa Mambo ya Nje mmoja kwa miaka 10, ambaye ni Dk Jakaya Kikwete. Kisha, Rais wa Nne, Kikwete, aliteua mawaziri wawili ndani ya miaka 10.

Januari 4, 2006, Kikwete alimwapisha Dk Asha-Rose Migiro, kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Januari 11, 2007, Migiro aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Uteuzi huo wa Migiro UN, ulisababisha nafasi ya uwaziri ibaki wazi. Kikwete alimteua Bernard Membe, ambaye alidumu kipindi chote kilichokuwa kimesalia katika urais wake.

Rais wa Tano, Dk Magufuli, alidumu na mawaziri wawili wa Mambo ya Nje, kwa miaka yake mitano na siku 132, ambayo alihudumia nchi, kabla ya mauti kumkuta. Rais Samia, ndani ya miaka mitatu na miezi minne, ameshafikisha mawaziri wanne, Wizara ya Mambo ya Nje. Je, kunani? Sasa waziri ni Balozi Mahmoud Thabit Kombo.

Hivi karibuni, Nape akiwa ziarani mkoani Kagera, alinukuliwa akitoa matamshi tata. Nape aliwaambia wakazi wa Bukoba Mjini kuwa yeye ni mzoefu wa uchaguzi, na kwamba angemsaidia mbunge wao Byabato kushinda uchaguzi.

Akasisitiza kuwa yeye kama Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, anasimamia kampuni za simu, hivyo angezishawishi zitoe fedha kusaidia maendeleo jimboni kwa Byabato.

Watu wengi wameelekeza lawama zao kwenye kauli ya Nape kuwa angemsaidia Byabato kutangazwa mshindi hata nje ya sanduku la kura. Hata hivyo, kwangu kauli mbaya zaidi ni ile aliyosema kuwa angeshawishi kampuni za simu zipeleke maendeleo jimboni kwa Byabato, kitu ambacho hakina tafsiri tofauti ya rushwa.

Kiongozi wa Serikali anayepaswa kuwa msingi wa maadili kwenye eneo lake, hakupaswa kutoa kauli zenye ukakasi.

Waziri kutamba kuwa angeshawishi kampuni binafsi kuchangia maendeleo ili kumsaidia Byabato, inajenga wasiwasi kuwa pengine ndiyo ulikuwa mchezo wake.

Tena kwa masilahi binafsi. Waziri badala ya kusimamia sheria na sera, kuhakikisha kampuni zinatoa huduma bora, yeye anawaza kuzishawishi zimchangie pesa.

Hii ni hadithi mbaya ya Nape.

Kutoka Nape hadi January, sasa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ni Jerry Silaa, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Deogratius Ndejembi, ndiye anakuwa Waziri wa Ardhi, akitokea Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu. Ndejembi amempisha Ridhiwani Kikwete.

Pitia mabadiliko yote, jambo moja hatuwezi kubishana ni kuwa Baraza la Mawaziri chini ya Rais Samia, limekuwa na mabadiliko ya mara kwa mara bila kuwa na maelezo ni kwa nini yanatokea.

Ndani ya miaka mitatu ya Rais Samia, ukimwondoa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mawaziri waliobaki wote walishafanyiwa mabadiliko.

Yupo mtu anaweza kulileta jina la Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, kuwa hajabadilishwa. Awali, wizara ilikuwa ikiitwa Fedha na Mipango, kisha ikagawanywa mara mbili. Mwigulu amebaki kuwa Waziri wa Fedha. Mipango ikaanzishiwa wizara mpya ya Uwekezaji na Mipango, ambayo waziri wake ni Profesa Kitila Mkumbo.

Mabadiliko ya mara kwa mara yanaleta maswali, je, mawaziri hawawezi kazi au hulka zao hazimfurahishi Rais Samia, kwa hiyo anawabadilisha kila baada ya miezi?

Je, ndani ya Serikali kuna usaliti mkubwa, ndiyo sababu hataki kutulia na wasaidizi wake kwa muda mrefu?

Katika historia, Tanzania chini ya Rais Samia imeweka rekodi ya kubadili wakurugenzi wakuu wanne wa Idara ya Usalama wa Taifa, ndani ya miaka mitatu.

Januari 2023, alimwondoa ofisini aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Diwani Athuman. Aliyempokea Diwani ni Said Massor.

Miezi saba ilitosha kwa Massor kufika tamati Tiss. Agosti 28, 2023, Balozi Ally Siwa, aliapishwa kuwa DGIS. Kisha, ilipofika Julai 11, 2024, Rais Samia alimwapisha Suleiman Abubakar Mombo kuwa Mkurugenzi Mkuu mpya wa Idara ya Usalama wa Taifa.

Kwa nini Serikali ya Rais Samia haitulii? Wapo watu wanadai shida kubwa ni Uchaguzi Mkuu 2025.

January ametajwa mara nyingi kuwa na mipango ya kuwania urais mwaka 2025. January mwenyewe alishajitokeza na kueleza kumuunga mkono Rais Samia. Je, ni mapambano dhidi ya adui asiyekuwepo?

Mabadiliko yafanyike. Iwe kwa nia njema ya kuhudumia nchi au hofu na visasi vya kutoaminiana, muhimu ibaki kichwani kwamba Serikali inapaswa kuonekana imetulia, ikitekeleza wajibu wake kwa wananchi.

Panga pangua ya mawaziri hadi wakurugenzi Tiss, ni kiashiria cha Serikali kutotulia. Zaidi, ni kama alivyosema Haddon, hakuna mabadiliko ya Baraza la Mawaziri ambayo hayaipeleki Serikali nje ya mstari.

Kuondolewa kwa mawaziri wawili, January Makamba, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Nape Nnauye, aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kumeibua mjadala, hasa mitandaoni.

Wananchi wamekuwa na maoni tofauti kuhusu kuondolewa kwa mawaziri hao, huku wengi wakihusisha kuondolewa kwa Makamba na mbio za urais, huku wengine wakieleza kwamba Nape amejimaliza mwenyewe kwa kauli yake aliyoitoa hivi karibuni.

Akizungumzia uamuzi wa kuondolewa kwa Nape, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe alisema pengine kauli yake ya Julai 15 ndiyo iliyomponza.

“Yalikuwa makosa makubwa kwa kiongozi mwandamizi kama Nape kutoa kauli kama hizo zenye kukichafua chama (CCM) na Serikali juu ya uchaguzi.

“Kauli yake inaweza kuwa imechukuliwa kama uthibitisho kwa wapinzani ambao mara zote wamekuwa wakilalamika kuibiwa kura,” ameeleza.

Dk Kabobe amehusisha kuondolewa kwa Nape na madai yaliyowahi kutolewa na mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde akimtuhumu kwa hujuma za uchaguzi ndani ya CCM wakati wanapiga kura za kuwachagua wabunge wa Afrika Mashariki.

Related Posts