M-Bet yakabidhi Sh100 milioni kwa Simba kwa ajili ya Simba Day

Na Mwandishi wetu

Mdhamini mkuu wa Simba, kampuni ya michezo ya kubashiri ya M-Bet Tanzania imeikabidhi timu hiyo Sh100 milioni kuelekea sherehe za miaka 88 tangu kuanzishwa kwa timu “Simba Day”.

Simba itanya maadhimisho ya miaka 88 tangu kuanzishwa kwake Agosti 3 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

 Afisa masoko wa M-Bet Tanzania, Victor Wilson, alikabidhi mfano wa hundi kwa Afisa  Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula, katika hafla fupi iliyofanyika Morogoro.

Wilson alisema kwamba pesa hizo ni sehemu ya makubaliano katika mkataba wao waliosaini na Simba wa miaka mitano Agosti 1, 2022.

Mkataba huo wa udhamini wa miaka mitano una thamani ya Sh26.1 bilioni. 

“Tunafurahi kuwa sehemu ya klabu kubwa Tanzania, Simba ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya soka nchini.

Nawaomba mashabiki na wanachama wa Simba kujitokeza kwa wingi katika hafla ya Simba Day,” alisema Wilson.

Kwa upande wake, Kajula aliishukuru M-Bet kwa msaada wao na akaahidi kwamba klabu haitawaangusha katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

 “M-Bet ni wadhamini wakuu wa klabu na wamechangia mengi kwa timu tangu tuliposaini mkataba mwaka 2022. Hadi sasa, tumetumia zaidi ya Sh13 bilioni kwa usajili wa wachezaji, ikiwemo mishahara. Tuna timu bora kwa msimu ujao wa ligi, na tuna uhakika tutafanya vizuri,” alisema Kajula.

Simba itapambana na vigogo wa Rwanda, APR katika mchezo huo uliopangwa kuanza saa 1.00 usiku.

Wakongwe hao wa soka nchini watakuwa wakicheza mchezo wao wa mwisho kabla ya kupambana na Yanga katika mechi ya nusu fainali ya ngao ya jamii Agosti 8 kwenye uwanja huo huo.

Afisa mtendaji mkuu wa Simba, Imani Kajula (mwenye jezi nyekundu)  akipozi na Afisa Masoko wa kampuni ya M-Bet Tanzania Victor Wilson (kushoto) and Afisa mwenzake, Seleman Mrisho mara baada ya kukabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya Sh100 millioni kuelekea maadhimisho ya Simba Day.

Related Posts