Dar es Salaam. Kampuni ya ZAS Investment Company Limited imekwaa kisiki baada ya mipango yake ya kujaribu kukwepa kulipa deni la mkopo wa mabilioni ya fedha kutoka Benki za Equity Tanzania Limited na Equity Kenya Limited kunasa kwenye mtego wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara.
Mahakama imesema kampuni hiyo ilikiuka mkataba wa mkopo wa kibenki uliosainiwa Oktoba 5, 2021, hivyo kuiamuru kuzilipa benki hizo deni la msingi la mkopo huo zaidi ya Dola milioni 8.06 za Marekani (sawa na zaidi ya Sh21 bilioni).
Pia imeamuriwa kulipa riba ya compound ya asilimia nane ya kiasi hicho, kama ilivyobainishwa katika mkataba wa Oktoba 5, 2021, kuanzia tarehe ya kufungua madai kinzani mpaka tarehe ya hukumu na riba ya asilimia saba kwa mwaka kuanzia tarehe ya hukumu mpaka tarehe ya kumaliza malipo yote.
Vilevile, Mahakama imewaamuru wakurugenzi hao na kampuni hizo nyingine mbili kuzilipa benki hizo zaidi ya Dola milioni 7.6 (sawa na zaidi ya Sh19.97 bilioni) kama kiasi cha dhamana waliyoitoa kwa ZAS katika mkopo huo kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao.
Mwisho kampuni hiyo na wadhamini wake wameamriwa kulipa gharama za shauri la madai kinzani.
Kampuni hiyo iliingia mikataba na benki hizo kwa nyakati tofauti katika ya Septemba 28, 2020 na Oktoba 5, 2021, ambapo benki hizo ziliiwekea udhamini wa mkopo kutoka kwa mkopeshaji wa nje ya nchi kwa ajili ya kulipa madeni yake mengine na kuendesha shughuli zake.
Mikataba hiyo iliiwezesha kampuni hiyo kupata mkopo wa Dola milioni 7 (zaidi ya Sh18.43 bilioni) kutoka kampuni ya Lamar Commodity Trading DMCC (Lamar) kutoka Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu kupitia wakala wake kampuni ya Numora Trading PTE Limited (Numora).
Kwa mujibu wa mkataba wa mkopo huo, benki hizo zilitakiwa kwanza kuwasilisha kwa kampuni hiyo hati ya muamana, yaani barua ya kibenki ya udhamini wa mkopo huo (Standby Letter of Credit/Letter of Credit – SBLC/LC) kama sharti la mkopo ambalo benki hizo zilitekeleza.
Ili kupata SBLC/LC hiyo, kampuni ya ZAS mbayo ilikuwa mteja wa benki hizo tangu mwaka 2014, pia iliweka hati za mali zake mbalimbali zinazohamishika na zisizohamishika zilizoko maeneo mbalimbali nchini kama dhamana.
Hata hivyo, baada ya muda wa kurejesha mkopo huo kufika, kampuni ya ZAS ilishindwa kuureresha na hivyo benki hizo kama mdhamini zikawajibika kuilipa mkopo huo na zenyewe zikaidai kampuni hiyo.
Badala ya kulipa mkopo huo, kampuni hiyo ilikimbilia mahakamani ambako ilifungua kesi kupinga kudaiwa na benki hizo kwa madai mkopo huo ilioupokea kutoka kwa mkopeshaji huyo wa nje, hakuwa na dhamana.
Katika kesi hiyo ya kibiashara namba 103/ 2022, kampuni ya ZAS ilidai mikataba iliyosainiwa na pande hizo mbili kuwezesha upatikanaji wa mkopo huo ni batili, ikidai benki hizo zilikiuka masharti kwa kushindwa kuitekeleza kwa kuwa hazikutoa SBLC/LC.
Kwa hiyo kampuni hiyo ilidai mkopo huo ilioupokea kutoka kampuni ya Lamar/Numora haukuwa na dhamana kutoka kwa benki hizo, huku ikizituhumu benki hizo kufanya udanganyifu na kuhusiana na upatikanaji mkopo huo na kusababisha kuilipa zaidi ya Dola 300,000 za Marekani isivyo halali.
Hivyo, iliiomba pamoja na mambo mengine Mahakama hiyo iamuru benki hizo zilizokiuka masharti ya mikataba hiyo, mali ilizoziweka kama dhamana ya kuwezesha kupata mkopo huo wa nje ziachiliwa na kuirejeshea.
Benki hizo katika majibu yake zilipinga madai ya kampuni hiyo, huku nazo zikifungua shauri la madai kinzani dhidi ya kampuni ya ZAS na wakurugenzi wa kampuni hiyo waliotoa udhamini binafsi na kinga kwa ajili ya SBLC/LC.
Wadhamini hao ambao ni wakurugenzi wa kampuni hiyo ni Amit Babubhai Ladwa, Muzdalifat Mohamed Ali, Jamal Ali Muslim pamoja na kampuni za Masasi Construction Company Limited na Bahati Apartment.
Katika madai yake, benki hizo zilidai zilitekeleza masharti ya mikataba hiyo kwa kuwa zilitoa SBLC/LC iliyoiwezeaha kampuni hiyo kupata mkopo huo kutoka kwa Lamar/Numero.
Zilidai kampuni hiyo ndio iliyokiuka masharti ya mkataba, kwani haijarejesha mkopo huo kwa mkopeshaji na zenyewe ndio zikawajibika kuulipa.
Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo iliyosikilizwa na Jaji Butamo Phillip, kampuni ya ZAS iliyowakilishwa na Wakili Frank Mwalongo, ilimuita shahidi mmoja na kuwasilisha jumla ya vielelezo 18.
Benki za Equity ambazo ziliwakikishwa na Wakili Timon Vitalis ziliwaita mashahidi wanne, huku zikiwasilisha kupitia mashahidi hao jumla ya vielelezo 95.
Mahakama baada ya kusikiliza na kupitia ushahidi wa pande zote, vielelezo vilivyowasilishwa pamoja na hoja za mwisho za mawakili wa pande zote katika uamuzi wake ilioutoa juzi, Jumanne Alhamisi Julai 23, 2024, imetupilia mbali shauri la msingi lililofunguliwa na ZAS.
Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa madai na hoja za kampuni hiyo hazina mashiko, kwani ilishindwa kuyathibitisha madai yake.
Badala yake imekubaliana na madai ya benki hizo na hoja za wakili wake, Vitalis, ikisema zimethibitisha madai yake kwa kiwango kinachohitajika kisheria.
Pamoja na mambo mengine, msingi wa kesi ya upande wa mdai (ZAS) katika kesi hiyo ilikuwa ni mkopo ilioupata kutoka Lamar/Numora si tu haukuwa na dhamana ya SBLC/LC kutoka kwa Benki ya Equity Kenya (EBK), bali pia haukuwa na dhamana hiyo kutoka mahali popote.
Katika hoja zake wakili wa ZAs, Mwalongo ameieleza Mahakama kuwa swali kwamba iliwezekanaje mkopeshaji Lamar/Numora akatoa mkopo huo bila ya dhamana ya SBLC/LC kama mkataba wa mkopo huo unavyoeleza, haikuwa hoja inayohusika katika kesi hiyo.
Wakili Mwalongo amedai pande husika katika mkopo huo ndizo zinajua sababu hiyo, hivyo Mahakama haikupaswa kujishugulisha nayo.
Hoja hiyo ilipingwa vikali na Wakili wa EBT na EBK, Vitalis aliyeirejesha Mahakama katika kielelezo cha 64 cha upande wa utetezi (benki hizo), yaani barua ya dhamana ya EBK (LC) ni sharti muhimu lililopaswa kutekelezwa kwanza ndipo mkopeshaji atoe mkopo huo.
Lakini Jaji Phillip amesema hakubaliani na wakili Mwalongo kuwa mkopo huo uliotolewa bila SBLC/LC, kinyume cha kielelezo cha sita cha upande wa mdai (ZAS), mkataba baina yake na mkopeshaji Lamar/Numora, kuwa hoja hiyo si sehemu ya kesi hiyo.
Jaji Phillip amesema hata shahidi wa kwanza wa mdai, ZAS alisema kuwa hoja hiyo inahusika katika kesi hiyo, Ili kuamua mgogoro wa utolewaji wa hiyo SBLC/CL.
“ZAS inadai kuna ukiukwaji wa makubaliano ya SBLC/LC na wakati huohuo imedai ilipokea mkopo huo kiasi kikichooneshwa kwenye SBLC/LC bila kuwepo kwa SBLC/LC hiyo,” amesema Jaji Phillip na kuongeza:
“Hivyo, ilikuwa muhimu ZAS kuelezea iliwezaje kupata mkopo uliopaswa kuwa na dhamana ya SBLC/LC, bila kuwepo hiyo SBLC/LC.”
Jaji Phillip amesema hawezi kusisitiza umuhimu wa maelezo ya mkopo unaodajwa kutolewa na Numora bila dhamana katika kesi hiyo.
“Itoshe tu kusema kwa kuwa EBT na EBK walidai LC ilitolewa na kuwezesha utolewaji wa mkopo kwa ZAS kutoka Lamar/Numora, ZAS ina dhima ya kuthibitisha madai yake kuwa mkopo huo haukuwa na dhamana ya SBLC/LC iliyotolewa na EBK,” amesema Jaji Phillip.
Amesisitiza madai ya wakili Mwalongo kuwa mkopo huo haukuwa na dhamana hayana msingi na kwamba ushahidi uliotolewa unathibitisha mkopo huo ulitolewa kwa ZAS baada ya kutolewa kwa LC.
Pia amesema ushahidi unaonyesha EBK ilipaswa kulipa kiasi cha mkopo huo chini ya masharti ya LC na kwamba ZAS haikuweza kutoa ushahidi kuthibitisha kuwa iliilipa EBK kiasi cha mkopo huo ambao EBK iliulipa (kwa Lamar/Numora).
Hivyo, Jaji Phillip baada ya kuchambua na kujadili ushahidi wa pande zote, vielelezo na hoja za mawakili, amehitimisha kuwa SBLC/LC na EBK kwa ajili ya mkopo huo uliotolewa kwa ZAS kutoka Lamar/ Numora.
Pia amesema mikataba ya mikopo hiyo baina ya ZAS na EBT na EBK Septemba 28, 2020 na Oktoba 5, 2021 si batili, kwani ilitekelezwa na kwamba ZAS ilikiuka mikataba hiyo kwa kushindwa kurejesha mkopo huo ndani ya muda uliokubaliwa.
“Kwa nyongeza ushahidi uliotolewa na EBT na EBK ulithibitisha kwa kiwango kinachotakiwa kisheria kwamba ZAS inadaiwa na EBT na EBK,” amesema Jaji Phillip.
Pia amesema ushahidi huo uliotolewa umethibitisha wadaiwa wa pili mpaka wa sita katika madai kinzani (ya EBT na EBK) wanawajibika kulipa mkopo uliotolewa kwa ZAS katika nafasi yao ya udhamini.
“Kutokana na hayo (yaliyoelezwa) ni uamuzi wa Mahakama hii kwamba ZAS imeshindwa kuthibitisha madai yake dhidi ya EBT na EBK, kwa kiwango kinachotakiwa kisheria, wakati EBT na EBK zimethibitisha madai yake dhidi ya wadaiwa katika madai kinzani kwa kiwango kinachotakiwa kisheria,” amesema Jaji na kuhitimisha:
“Hivyo, ninafuta kesi ya msingi kwa gharama (mdai, ZAS kulipa gharama gharama za kesi) na natoa hukumu dhidi ya wadaiwa katika madai kinzani (ZAS na wadhamini wake) kama ifuatavyo,” amesema Jaji Phillip na kutoa amri mbalimbali.
Kesi hii ni moja kati ya kesi kadhaa zilizofunguliwa na kampuni mbalimbali zinazodaiwa kukopeshwa au kudhaminiwa na benki hizo kupata mikopo kutoka kwa wakopeshaji wa nje, lakini zikagoma kulipa na kisha kuzishtaki benki hizo baada ya kuzidai, zikipinga kudaiwa.
Kampuni hizo zinawakilishwa na wakili mmoja, Mwalongo, ziko katika maeneo tofauti na zilikopa kwa nyakati tofauti, lakini msingi wa mgogoro wao dhidi ya benki hizo katika ulipaji wa mikopo hiyo unafanana na karibu zote zinapinga kudhaminiwa na benki hizo.