“Natumia lipa namba kufanya malipo ya huduma nyingi ninazozipata, kwa muda sasa nimepunguza matumizi ya pesa taslimu, nikiwa na simu yangu nina kila kitu,” anasema Jesca Jackson.
Jackson anasema mtandao wa simu anaoutumia unampa fursa ya kufanya mambo mengi bila kuhitaji kutafuta huduma sehemu nyingine, hususan za kifedha.
“Kubeba pesa taslimu ni hatari kwa usalama wa mbebaji na pesa zenyewe, huduma za fedha kidijitali zinapunguza hatari hiyo,” anasema Jackson, ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam.
Jackson ni miongoni mwa mamilioni ya watu waliojiunga na huduma za fedha kwa simu ya mkononi ambao kwa sasa idadi yao imekuwa ikiongezeka kila siku.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), hadi kufikia Juni 2024, kulikuwa na akaunti milioni 55.7 za pesa mtandaoni ambazo zimetumika walau mara moja ndani ya kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa akaunti za pesa mtandao ziliongezeka kwa wastani wa asilimia 1.9 kwa mwezi katika robo mwaka iliyoishia Juni 2024, huku idadi ya watoa huduma wakiwa sita (M-pesa, Tigopesa, Airtel Money, T-pesa, Halopesa na Azam Pesa).
M-Pesa ndiyo yenye akaunti nyingi zaidi (milioni 20.67), ikifuatiwa na Tigo-pesa akaunti milioni 17.82, Airtel Money akaunti milioni 11.02, Halopesa akaunti milioni 4.56, T-Pesa akaunti milioni 1.42 na Azam Pesa akaunti 187,691.
Idadi ya miamala nayo imeongezeka katika kipindi husika hadi kufikia wastani wa miamala milioni 295.9 kwa mwezi, sawa na walau miamala milioni 10 kila siku.
Kwa miaka mitano iliyopita, miamala ya pesa mtandao iliongezeka kutoka bilioni 3 mwaka 2019 hadi bilioni 5.3 kwa mwaka 2023, sawa na asilimia 19 ya ukuaji kwa kila mwaka. Katika kipindi hicho, wastani wa miamala kwa kila mteja ulipungua kutoka miamala 117 mwaka 2019 hadi 100 mwaka 2023
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari anatafsiri ukuaji huo kama nguzo muhimu ya uchumi wa kidijiti Tanzania, ambao umekuwa ukipigiwa chapuo kwa miaka mingi.
Anasema mwaka 2016 Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza barani Afrika na Ulimwenguni kuwa na mfumo kamili uliowezesha mwingiliano wa mitandao ya fedha kupitia simu za mkononi.
Dk Bakari amefafanua kuwa mwingiliano huu unawezesha huduma kutolewa miongoni mwa watoa huduma za simu za mkononi na miongoni mwa watoa huduma hawa na mabenki.
“Mtumiaji wa mtandao wowote wa simu za mkononi anaweza kutuma pesa kwenye mtandao mwingine, lakini pia kufanya malipo na miamala mingi ya kibenki kupitia simu zao za mkononi,” anasema.
Akirejea takwimu za mamlaka anayoiongoza, Dk Bakari anasema akaunti za pesa kwa simu zimeongezeka kwa karibu mara mbili ndani ya miaka mitano, huku kukiwa na ukuaji wa asilimia tano kati ya Aprili na Juni mwaka huu, takwimu zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCFA) zinaonesha.
Dk Bakari amesema akaunti za pesa kwa simu ziliongezeka kutoka milioni 25.86 mwaka 2019 hadi milioni 52.87 mwaka 2023 na kufikia milioni 55.52 Juni 2024. Akaunti hizi zilifanya jumla ya miamala bilioni 5.27 Juni 2024, ikilinganishwa na miamala bilioni 3.02 mwaka 2019.
Anaeleza kuwa TCRA inashirikiana na Benki Kuu ya Tanzania kuendeleza matumizi ya simu za mkononi kufanya miamala ya kifedha mtandaoni.
“TCRA inatoa leseni kwa watoa huduma za simu za mkononi ambao wanatoa huduma za pesa mtandaoni. Inawapa namba za mawasiliano na misimbo, au namba fupi za kuwezesha miamala hiyo. Benki Kuu ya Tanzania inasimamia sekta ya fedha kwa ujumla na inatoa leseni za huduma za fedha mitandaoni.”
Hata hivyo, mtumiaji wa huduma za miamala ya simu, Johari Samson anasema kama gharama katika huduma hizo zingekuwa chini, watu wengi zaidi wangekuwa sehemu ya huduma hiyo.
“Ni muhimu sana kuwa na utamaduni wa kutumia huduma za miamala kidijitali, kwani naweza kununua na kulipa mahali popote bila usumbufu, changamoto iliyopo sasa ni gharama, maana ukilipa mara 10 unajikuta karibu Sh15,000 imeondoka,” alisema Samson.
Kuhusu mwenendo huo wa sekta ya matumizi ya huduma za fedha kidijitali, Mchambuzi wa Uchumi, Dk Mwinuka Lutengano anasema ukuaji wa huduma za miamala ya simu unatokana na ukuaji wa huduma nyingine za kiuchumi.
“Huduma za miamala zinategemea sana huduma nyingine na kwa jiografia ya nchi yetu yenye maeneo mengi ya vijijini, huduma hizi zinakuwa ni muhimu sana kwa kuwa huduma za kibenki hazipatikani huko,” amesema Dk Lutengano.
Dk Lutengano, ambaye ni mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu Dodoma, anasema sababu nyingine ya ongezeko hilo ni kukua kwa matumizi ya Tehama miongoni mwa wananchi.
“Watu wengi wanatumia huduma za simu lakini huduma za kibenki hazijafika maeneo mengi, lakini mawakala wa miamala ya simu wako kila kona na leseni zake ni rahisi kuzipata,” anasema Dk Lutengano.
Kuhusu gharama kubwa zinazozungumziwa na baadhi ya watumiaji, Dk Lutengano anasema kadiri watumiaji wanavyozidi kuwa wengi ushindani utaongezeka, ikizingatiwa kuwa watoa huduma ni wengi, hivyo gharama zitapungua.