Mashujaa vita vya Kagera wasimulia waliyopitia hadi kushinda

Bukoba. Wakati Tanzania ikiadhimisha Siku ya Mashujaa leo Julai 25, 2024, mashujaa waliopigana vita vya Kagera dhidi ya utawala wa Idd Amin wa Uganda, wamesimulia walivyolipigania Taifa, huku wakiwahimiza vijana waliopo jeshini kufuata nyayo zao katika kulinda amani ya nchi.

Vita kati ya Tanzania na Uganda ilipigana mwaka 1978 hadi 1979 ikianzia katika Mkoa wa Kagera ambapo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kushirikiana majeshi ya waasi wa Uganda, walimuondoa kiongozi wa kijeshi wa Uganda wakati huo, Idd Amin.

Maofisa wanne wastaafu wa JWTZ waliopigana kwenye vita hiyo wamesimulia ujumbe waliopewa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere wakielekea vitani na namna walivyopigania amani na ushindi dhidi ya Amin.

Gabriel Mduta, amesimulia alishuhudia gari la kijeshi lililokuwa limebeba askari lilivyolipuliwa na maadui wao wa Uganda.

Amesema yeye alikuwa kwenye gari dogo eneo la Kabwoba lililopo mpakani mwa Tanzania na Uganda, wakiwa wameegesha kupokea maelekezo ya viongozi wao, waliona gari lililobeba vifaa vya kijeshi na askari linalipuliwa.

“Kitendo hicho kilitushtua sana kuona askari wenzetu na vifaa tulivyokuwa navyo vimelipuliwa,” amesema shujaa huyo.

Amewasihi vijana waliopo jeshini kuwa na uchungu wa kulinda amani ya Taifa, pale linapotokea jambo lolote la kuhatarisha usalama wa nchi kama wao walivyofanya.

Kwa upande wake, mstaafu wa JWTZ, Meja Dominikius Kauta amesema alishiriki vita hiyo kuanzia mwaka 1971, 1974 hadi Julai 25, 1979 na kwamba kitu ambacho hatasahau ni adui yao alipovunja daraja la Mto Kagera na kusababisha uchungu kwa askari wa Tanzania, hivyo wakaanza kumshambulia.

“Zilianza chokochoko mwaka 1971 hadi vita yenyewe 1979, tuliumia sana kuona daraja alilotengeneza kiongozi wetu Mwalimu Nyerere linavunjwa na adui Idd Amin. Mwalimu alisema huyu si wa kuacha, tuhakikishe tunapigana hadi kumtoa.

“Tulianza polepole hadi tukavuka mpaka wa Mtukula, Mbarara, Masaka, chokochoko zikazidi tukampiga hadi Jinja na Kampala mpaka kwake Koboko na historia ya vita ikawa imeishia hapo,” amesema Kauta.

Kauta ametaja maeneo yaliyowapa shida kwenye vita hiyo kuwa ni sehemu za Rukaya na Kajansi ambazo zilikuwa ngome za wanajeshi wa Uganda na wale waliokuwa wamechukuliwa kutoka Libya, lakini walifanikiwa kuwapiga hadi kuwanyang’anya silaha zote.

Kwa upande wake, kapteni mstaafu, Moses Mgendwa amesema vita hiyo iliyoanzia Kagera inamkumbusha alivyolazimishwa kuingia kwenye vita baada ya Amin na vikosi vyake kuvamia eneo la Mkoa wa Kagera hasa Mto Kagera.

“Tuliingia vitani na kuanza kusonga mbele hadi Amin alipotolewa kwenye mipaka yetu na ilikuwa turudie Masaka na Mbarara, lakini Mwalimu Nyerere aliposikia Amin anataka majeshi yatakaporudi atawachinja wote waliokuwa wanaisaidia Tanzania, basi Mwalimu akatoa amri nyingine kwamba tusonge mbele hadi tutakapomtoa,” amesema Mgendwa.

Ameongeza kwamba kitu kinachomuuma hadi sasa ni namna alivyoshuhudia maiti za watu zilivyokuwa zimezagaa kila eneo kutokana na mashambulizi ya vikosi vya Amin dhidi ya Watanzania.

Kwa upande wake, Wadari Issa amewasihi vijana kuiga uzalendo wao na kujali kazi kwa kila hali na wale walio jeshini amewataka wafanye kazi ya Taifa.

“Vita ilikuwa ngumu, lakini Mungu alikuwa upande wetu na niwaombe tulinde Taifa letu, tuangalie kinachotokea kwenye mataifa ya wenzetu, ni mifano tosha, siyo mambo mazuri, la msingi ni kulinda Taifa na kupiga kazi,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, aliyeongoza kumbukizi ya Siku ya Mashujaa mkoani Kagera, amewataka wananchi kuwapongeza mashujaa wote waliorejesha amani na furaha ya Taifa miaka hiyo na hadi sasa Tanzania ni nchi ya mfano kwa amani duniani.

Mwassa amewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu na wenye amani na uchungu wa kulinda Taifa lao pale zinapotokea changamoto kwenye mataifa jirani, ili waepuke kushawishika kufanya vitendo vya kuondoa amani ya Taifa.

Sherehe za maadhimisho ya Siku ya Mashujaa kimkoa zimefanyika Uwanja wa Mayunga uliopo Manispaa ya Bukoba.

Related Posts