Dar es Salaam. Mkazi wa Goba-Matosa, jijini Dar es Salaam, Musa Sasi (32) anashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake, Lucy Haule (29), naye kunusurika kujiua.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limethibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Alhamisi Julai 25, 2025 maeneo ya Goba Matosa, Kinondoni huku likieleza uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo cha mauaji hayo kinatokana na ugomvi uliozuka baina yao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Jumanne Muliro, mtuhumiwa amekamatwa na hali yake ni mbaya, yupo Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala akipatiwa matibabu.
“Baada ya kumuua mpenzi wake, mtuhumiwa naye alijaribu kujiua kwa kutumia kisu kwa kujichoma shingoni. Mtuhumiwa amekamatwa na hali yake ni mbaya na yupo Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala,” amesema Kamanda Muliro.
Amesema taarifa za tukio hilo walizipata saa 3:20 asubuhi, baada ya kufika eneo la tukio na kubaini kuwepo kwa mwili wa mtu aliyefariki dunia.
“Tulipofika tulikuta mwili wa mtu, alishapoteza maisha. Alifahamika kwa jina la Lucy Stevin Haule (29), mfanyakazi wa kiwanda cha pombe kali iitwayo Nguvu Banana Wine.
“Uchunguzi wa awali umeonyesha aliuawa na mpenzi wake aliyefahamika kwa jina la Musa Sasi (32), anayefanya kazi ya kibarua katika kiwanda cha pombe ya banana na mkazi wa Goba Matosa,” amesema.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa jamii, pindi watu wanapokuwa na migogoro au matatizo ya kijamii wazishirikishe taasisi mbalimbali za kisheria, za kiserikali na zisizo za kiserikali, ili zisaidie kutatua matatizo yanayowasumbua.
“Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola na wananchi wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali za kuzuia vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na watu wengine,” amesema.
Jeshi hilo limesema vitendo vya ukatili ni pamoja na vya kubaka, kulawiti, kunajisi, mauaji na ukiukwaji mwingine wowote wa sheria unaohusisha haki za watoto.
“Tangu jana Julai 2024 kupitia mitandao ya kijamii kumekuwa na taarifa zilizojaa sintofahamu kuhusu kipande cha picha ya video ikionyesha kijana mmoja wa kiume kutoka eneo la Ilala -Bungoni akihojiwa na wananchi kuhusiana jaribio la wizi wa mtoto.
“Baada ya kupata taarifa hizo Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lilizifuatilia taarifa hizo na kubaini tukio la kipande hicho cha video sio mwaka huu au mwaka jana,” imesema.
Jeshi hilo limesema tukio hilo lilitokea Julai, 2022 eneo la Ilala Sharifu Shamba na kuripotiwa kituo cha Polisi Ilala/Pangani kwa madai ya mama moja kumtuhumu Frank Moi Chacha (18), mkazi wa Vingunguti kutaka kuiba mtoto wake. Baadaye shauri hilo lilifikishwa mahakamani kwa CC.165/2022.