KOCHA wa Yanga, Miguel Gamondi ni kama amefunga mjadala juu ya dili la Maxi Nzengeli anayetajwa kutakiwa na Kaizer Chiefs akisema hakuna mchezaji yeyote wa kikosi hicho atakayeondoka, huku akichekelea ushindani wa namba ulivyo mkali ndani ya timu hiyo iliyokuwa uwanjani jana jioni kucheza na TS Galaxy.
Hapo awali kupita Mwanaspoti liliandika kuhusu nyota huyo kiraka kutakiwa na Kaizer ya Afrika Kusini iliyogonga hodi kwa Yanga kutaka kumsajili licha ya kuwa bado ana mkataba na kikosi hicho.
Hata hivyo, akizungumza na Mwanaspoti jana, Gamondi alisema kwa sasa hakuna uwezekano wa kumuuza mchezaji yeyote wa kikosi hicho, kwani hesabu alizonazo kwa msimu ujao zimekwisha kumalizika.
Gamondi alisema hakuna hatua kama hiyo na hawezi kuiruhusu kwa sasa na sio kwa Maxi tu, ila yeyote ambaye wameshamsajili na tayari yupo katika kikosi hicho na ameshaanza maandalizi ya msimu ujao.
“Sitakubali kumkosa mchezaji ambaye yuko katika kikosi kwa sasa, ruhusa pekee nitakayotoa ni pale atakapokosekana kwa sababu za majeraha na sio kumuuza,” alisema Gamondi na kuongeza;
“Kikosi tulichosajili ni kwa malengo yetu ya msimu ujao kwa ajili ya mashindano ya kimataifa na ya ndani, hivyo haiwezekani kumpunguza hata mmoja, ijapokuwa nafahamu zinakuja ofa nyingi kwa wachezaji wetu nyota, lakini hatukuruhusu waondoke na badala yake tulipambana kuwabakiza ili kulinda hesabu za msimu ujao.”
Gamondi alieleza ushindani wa namba umeongeza kitu kikubwa kwa wachezaji na kuwafanya wawe na hari ya kupambana, kwani hakuna anaejiamini atapata nafasi kutokana na ubora wa kila mmoja wapo.
“Ninafurahia ushindani wa namba unavyoendelea kwenye kikosi changu kwani umewafanya wachezaji kujituma na kutafuta nafasi na hizo ni sifa za mchezaji anayecheza kwa malengo ambao ndio wapo sasa kwenye kikosi changu,” alisema kocha huyo raia wa Argentina.
Maxi ambaye msimu uliopita ndio ulikuwa wa kwanza kucheza Ligi Kuu bara akimaliza kwa mabao 11, huku akiwa na uwezo wa kucheza kama winga au beki akifahamika kwa utaalamu wake wa kukaba, kuanzisha mashambulizi na kufunga pia, jambo lililozidisha thamani yake ndani ya kikosi na hata kwa timu zingine kama Kaizer Chief.