Mkurugenzi wa zamani TPA, wenzake wataka upelelezi dhidi yao uharakishwe

Dar es Salaam. Washtakiwa sita katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA), Madeni Kipande na wenzake, wameiomba Mahakama ielekeze upande wa mashtaka ukamilishe upelelezi kwa kesi hiyo haraka kwa kuwa ni ya muda mrefu.

Kipande na wenzake, wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya Dola milioni 1.85 za Marekani (sawa na Sh 4.2bilioni).

Washtakiwa hao kupitia wakili wao, Peter Kibatala wamewasilisha ombi hilo leo Alhamisi, Julai 25, 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Kibatala ametoa ombi hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu, muda mfupi baada ya upande wa mashtaka kudai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.

“Mheshimiwa hakimu, naomba upande wa mashtaka wawe serious na kesi hii kwa sababu ni ya muda mrefu na mwaka jana walituambia wapo katika hatua za mwisho kusajili taarifa muhimu Mahakama Kuu, lakini mpaka sasa upelelezi bado haujakamlika,” amedai Kibatala.

Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali, Winiwa Samson amedai kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi unaendelea kwa sababu baada ya kupitiwa ilibainika kuna vitu havijakamilika.

“Ni kweli tulisema tupo kwenye hatua za mwisho kuisajili Mahakama Kuu, lakini nimewasiliana na mpelelezi wa kesi ameniambia jalada lipo Takukuru kwa ajili ya kupitiwa kwa sababu ilibainika kuwa kuna vitu bado havijakamilika,” amedai Samson.

Hata hivyo, kutokana upelelezi wa shauri hilo kutokamilika, ameomba Mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa na kuangalia kama utakiwa umekamilika. Hakimu Magutu ameahirisha kesi hadi Agosti 23, 2024 na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.

Mbali na Kipande, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 38/2022 ni Peter Gawile, aliyekuwa Ofisa Rasilimali Watu wa TPA na mkazi wa Mianzini, Casmily Lujegi, mkazi wa Mbezi Juu na Mwenyekiti wa Bodi ya Manunuzi wa TPA, Mashaka Kisanta, Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi, Kilian Chale, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano pamoja na Andrew John.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, wanadaiwa kati ya Oktoba mosi, 2014 na Oktoba mosi 2020, jijini Dar es Salaam, walikula njama ya kutenda kosa la kuisababishia TPA hasara ya Sh4.2 bilioni.

Pia inadaiwa kati ya Januari mosi, 2015 hadi Februari 17, 2015 wakiwa maofisa wa TPA, walitumia madaraka yao vibaya kwa kutangaza zabuni namba AE/016/2014-15/CTB/G/39 kwa nia ya kujipatia dola 1,857,908.04 za Marekani.

Shtaka la tatu, inadaiwa kati ya Oktoba mosi, 2014 na Oktoba mosi, 2020 eneo la TPA na maeneo mengine ya Dar es Salaam, washtakiwa kwa makusudi walitangaza zabuni ya Enterprises Planning Resources (ERP) bila kupata kibali cha bodi ya zabuni ya mamlaka hiyo na kushindwa kufuata kanuni za zabuni, hivyo kutoa malipo ya awali ya asilimia 40 bila idhini ya bodi hiyo, jambo lililosababisha TPA hasara ya Dola milioni 1.8 za Marekani ambazo ni sawa na Sh 4.2bilioni.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Juni 30, 2022 na kusomewa mashtaka.

Related Posts