DROO ya makundi ya michuano kwa Klabu Bingwa kwa Nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati(CECAFA) imefanyika juzi, huku wawakilishi wa Tanzania, Simba Queens ikipangwa kundi linaloonekana mchekea linaloipa nafasi kubwa ya kutinga nusu fainali ya kusaka tiketi ya kushiriki Klabu Bingwa Afrika kwa mara ya pili.
Michuano hiyo kwa msimu huu itafanyika Addis Ababa, Ethiopia kuanzia Agosti 17 hadi Septemba 4, 2024 na bingwa atakata tiketi ya kushiriki fainali hizo za CAF na Simba ilishiriki mara ya kwanza 2022 na kumaliza nafasi ya nne, huku msimu uliopita ilienda JKT Tanzania ambayo ilitolewa hatua ya makundi.
Simba Queens imekata tiketi ya kushiriki michuano hiyo ya Cecafa kwa mara nyingine baada ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake uliokuwa ukishikiliwa na maafande wa JKT Queens.
Kwenye droo ya kupanga makundi hayo iliyofanyika juzi jijin Cairo, Misri Simba imeangukia Kundi B ikiwa pamoja na timu za PVP Buyenzi ya Burundi, Kawempe Muslim Ladies ya Uganda na FAD ya Djibouti.
Simba sio mgeni wa mashindano hayo kwani msimu wa 2022 ilichukua ubingwa wa Cecafa iliyowapa tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Msimu wa kwanza kushiriki Klabu Bingwa CAF iliishia nusu fainali na kumalizia nafasi ya nne kwa kufungwa kwa bao 1-0 dhidi ya Bayelsa Queens ya Nigeria.
Huu ni msimu wa nne wa CECAFA baada ya mwaka 2021 ubingwa ukienda kwa Vihiga Queens (Kenya), Simba Queens (2022) na JKT Queens msimu uliopita.
Michuano hiyo ya Cecafa, timu tisa zimegawanywa katika makundi mawili ikicheza michezo mitatu ya makundi kisha kuvuka nusu fainali na kisha fainali.
Kundi A lina timu za Kenya Police Bullets ya Kenya, Commercial Bank of Ethiopia (wenyeji), Yei Joint FC (Sudan Kusini), Warriors Queens (Zanzibar), Rayon Sport Womens (Rwanda).
Kwa makundi yalivyo na uzoefu wa Simba kwenye michuano hiyo ni wazi ikikaza inaweza kuchukua ubingwa wa Cecafa na kukata tiketi ya kucheza Klabu Bingwa Afrika.
Hadi sasa mpinzani mkubwa wa Simba ni C.B.E na ni wenyeji wa michuano hiyo msimu huu ikionekana ni timu tishio baada ya msimu uliopita kutolewa fainali na JKT Queens kwa mikwaju ya penati 5-4 dakika 90 zikiisha kwa suluhu.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo iliyofanyika Misri, Agosti 18, Simba itaanza kumenyana na FAD Djibouti ambao ndio msimu wao wa kwanza kushiriki michuano hiyo.
Baada ya mechi hiyo watavaana na Kawempe Muslim Ladies inayoshiriki Ligi ya wanawake Uganda, Agosti 21, kisha Agosti 24 kufunga hesabu dhidi ya PVP Buyenzi.
Kwa kuangalia timu shiriki za kundi hilo ni Simba imepata mchekea kwa kupewa timu zisizo na uzoefu wa kimataifa na kutokana na ushindani ulionyesha wana Msimbazi hao inaweza kuwa njia rahisi kwao kufika fainali na kuwa mabingwa.
Mamelodi Sundown Ladies ya Afrika Kusini ndiyo iliyobeba ubingwa mara nyingi zaidi ikifanya hivyo mara mbili msimu wa 2021 na 2023 na 2022 ikitolewa kwenye fainali na AS FAR ya Morocco kwa mabao 4-0.
Hivyo kutokana na mafanikio hayo, Mamelodi na tayari wamefuzu kwa hatua ya mwisho ya mashindano na wanatarajia kushinda taji la tatu kwa ukanda wa COSAFA.
Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Juma Mgunda alisema baada ya kuona makundi hayo wamejipanga kuhakikisha wanashinda na kurudi na kombe.
“Hatuangalii ni kundi jepesi kiasi gani kwa sababu hadi wana shiriki walikuwa mabingwa hivyo hatuchukulii kawaida,” alisema Mgunda na kuongeza;
“Tupo tunajiandaa kwenda kushindana na wote washindani wetu na hatuchagui nani bora hivyo tutapambana vilivyo.”
Winga wa timu hiyo, Mrundi Asha Djafar kwa sasa wamekuja kivingine baada ya kutoshiriki kwa msimu mmoja sasa.
“Mwanzo tulishiriki lakini hapa kati tulipotea, tumerudi tena na tunaamini kwa maandalizi haya tutafanya vizuri na kwenye kundi letu kuna Buyenzi ya nyumbani Burundi naamini sio wapinzani wagumu lakini tutawaheshimu.”