TAASISI YA NELSON MANDELA KUJENGA CHUJIO LA MAJI NGARENANYUKI KUPUNGUZA ATHARI ZA MADINI YA FLORIDE

Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti na Ubunifu kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Prof. Revocatus Machunda akiongea na wanakijiji wa Ngarenanyuki wakati wa maonyesho ya awali ya Nanenane.

Wanafunzi , wakulima na Wananchi wa Kata ya Ngarenanyuki wakiangalia bidhaa mbalimbali za kilimo katika maonesho ya awali ya Nanenane.

Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti na Ubunifu kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Prof. Revocatus Machunda ( wa pili kushoto) akiangalia kilimo cha mbogamboga kinachofanywa na wakazi wa kata ya Ngarenanyuki kwa kutumia mbolea iliyochujwa magadi , wa kwanza kushoto ni Mhadhiri Prof. Thomas Kivevele na wa Kwanza kulia ni Afisa Kilimo Kata ya Ngarenanyuki Bw. Solomoni Mzirai na wa pili kulia ni Msimamizi wa kitengo cha Kilimo Halmashauri ya Wilaya ya Meru Bi. Digna Masawe.

Wakazi wa Kata ya Ngarenanyuki wakiguatilia matukio katika
maonesho ya maandalizi ya awali ya Nanenane na ni ya kwanza kufanyika katika kata hiyo, ambayo yamejumuisha wadau wa kilimo, wakulima na wanafunzi 

……..

Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela imeahidi kujenga chujio kubwa la maji katika Kata ya Ngarenanyuki ili kupunguza athari zinazotokana na madini ya floride kwenye maji ya eneo hilo.

Hayo yamesemwa Julai 23, 2024 na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti na Ubunifu Prof. Revocatus Machunda ambaye pia ni Msimamizi wa Mradi wa kuondoa Madini ya Floride, wakati wa maonesho ya wakulima ngazi ya Kata, katika Kata ya Ngarenanyuki iliyopo Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

“Baada ya kubuni mtambo wa kuondoa madini ya Floride kwenye mbolea itokanayo na kinyesi cha wanyama sasa Nelson Mandela inajipanga kuleta chujio kubwa la maji ambalo litachuja maji na kuondoa madini hayo ili maji yafae kwa matumizi ya wakazi wa kata hiyo bila ya kuleta athari za kiafya.” alisema Prof.Machunda

Naye Bi. Digna Masawe Msimamizi wa kitengo cha Kilimo Halmashauri ya Wilaya ya Meru, ameeleza kuwa, Halmashauri hiyo inatambua mchango mkubwa wa Taasisi ya Nelson Mandela kwa kukuza kilimo kupitia tafiti zake na kuahidi kushirikiana nao bega kwa bega katika kufanikisha juhudi za watafiti za kuendeleza kilimo wilayani humo.

Kwa upande wa Afisa kilimo wa Kata ya Ngarenanyuki Bw. Solomoni Mzirai ameishukuru Taasisi ya Nelson Mandela kupitia kwa kuichagua kata hiyo kama eneo la kufanyia tafiti ya kuondoa madini katika kinyesi cha wanyama ambacho hutumika katika kilimo hususani kilimo hai (kilimo kisicho tumia mbolea zenye kemikali) na kuwafanya wakulima wa eneo hilo kuwa wakulima wa mfano katika wilaya hiyo kwa kilimo chenye tija.

Maonesho hayo ni maandalizi ya awali ya Nanenane na ni ya kwanza kufanyika katika kata ya Ngarenanyuki ambayo yamejumuisha wadau wa kilimo, wakulima na wanafunzi lengo ikiwa ni kuwakutanisha wakulima na wadau mbalimbali wa kilimo ili kufanya kilimo cha biashara na kujipatia mazao bora ya biashara na yenye kujenga afya ya mlaji.

Related Posts