Afisa Tawala wa Chama cha Wataalamu wa Barabara (TARA), Anna Nkoma, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Julai 24,2024 kuhusu kongamano la tisa kuhusu usafiri endelevu litakaloanza Jumatatu ijayo jijini Arusha.
Na Mwandishi Wetu
TANZANIA inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Kongamano la tisala Kimataifa la Usafiri Endelevu na Ubunifu Bora ambao umeandaliwa na Chama cha Wataalamu wa Barabara (TARA).
Mkutano huo utakaofanyika jijini Arusha wiki ijayo utafunguliwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa na utahudhuriwa na washiriki zaidi ya 300 kutoka ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi Mkuu wa TARA, Eliamlisi Joseph, amesema kuwa mada kuu ya kongamano hilo itakuwa Usalama, Umakini na Uendelevu wa Mifumo ya Usafiri kwa Ukuaji wa Uchumi Duniani.
Amesema madhumuni ya mkutano huo wa Kimataifa wa usafiri endelevu na ubunifu bora ni kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya usafiri kuhusu usafiri salama, mahiri na endelevu na mifumo ya ukuaji wa uchumi ulimwenguni kupitia kubadilishana maarifa, uzoefu na mbinu bora.
Amesema lengo ni kuwawezesha wadau katika sekta ya uchukuzi, kuchangia ipasavyo katika maendeleo, utekelezaji na usimamizi wa mifumo endelevu na bora ya usafiri na kutoa jukwaa la kina kwa wadau ili kuelewa changamoto na fursa za sasa.
“Washiriki watapata maarifa kuhusu mitindo, changamoto na fursa za hivi punde katika sekta ya usafiri, ikijumuisha maendeleo ya teknolojia, mabadiliko ya udhibiti na masuala ya mazingira huku pia wakipata zana muhimu, mbinu, na mbinu bora za kuboresha uwezo wao wa kitaaluma na michakato ya kufanya maamuzi katika mipango ya usafiri, uendeshaji na usimamizi” amesema Joseph.
“Hili ni tukio kubwa na la kimataifa ambalo litafunguliwa na Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa na wadau mbalimbali wa nje na ndani ya nchi watashiriki na wakuu wa taasisi mbalimbali kama Wakala wa Barabara TANROADS, Wakala wa Barabara Vijijini TARURA na Mfuko wa Barabara,” alisema
Naye, Afisa Tawala wa TARA, Anne Nkoma amesema watu watakaoshiriki mkutano huo watapaswa kulipia kiingilio cha 750,000 kwa ajili ya maandalizi ya mkutano huo na wale wenye kampuni watakaokwenda kuonyesha bidhaa zao watakipia sh miliombi mbili.
“Mtu akitaka kudhamini mkutano huu kwa kuleta vifaa mbalimbali kwenye mkutano wetu atapata unafuu wa gharama za kushiriki,” amesema