KIKOSI cha Azam FC kinaendelea kujifua mjini Morocco na kesho Jumamosi kitashuka tena uwanjani kucheza mechi ya pili ya kirafiki ya kimataifa baada ya awali kuifunga Us Yacoub Mansour mabao 3-0.
Azam iliyoweka kambi hiyo ya kujiandaa na msimu mpya wa mashindano itacheza mechi kesho saa 2 usiku dhidi ya Union Touarga kabla ya Jumatatu kuvana na mabingwa wa zamani wa Afrika, Wydad Casablanca mechi itakayopigwa kuanzia saa 1 usiku.
Lakini wakati kikosi kikiendelea kujifua, mabosi wa klabu hiyo wameamua kumpa nafasi nyingine winga chipukizi, aliyetabiriwa makubwa na familia ya wapenda soka hapa nchini, Tepsie Evans Theonasy kwa kumsainisha mkataba wa nyongeza wa mwaka mmoja.
Tepsie maarufu kama Tepsinho au kichwa bongo miguu Brazil akifananishwa uchezaji wake na vipaji vinavyozaliwa Brazil, amekulia katika kituo cha kulelea vipaji cha Chamazi alichojiunga nacho tangu mwaka 2016.
Mwaka 2019 alipandishwa timu kubwa na kocha Etienne Ndayiragije na baadaye kutolewa kwa mkopo kwenda Ihefu ya Mbalali mkoani Mbeya.
Huko akaungana na Zubery Katwila, kocha wake wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 20 aliyeshinda naye ubingwa wa CECAFA mwaka 2019 yaliyofanyika jijini Jinja, Uganda.
Kina Tepsie walishinda ubingwa kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Kenya iliyoundwa na kina Benson Omalla, ambaye ni straika hatari kwenye Ligi Kuu ya Kenya akiitumikia Gor Mahia.
Tepsie aliibuka mchezaji bora wa mashindano hayo na kuashiria kesho kubwa kwa kijana huyo kutokea Morogoro, kwenye asili ya vipaji vingi na vikubwa tangu na tangu.
Baada ya mashindano haya ndipo Kocha Ndayiragije akampandisha timu ya wakubwa kwa ajili ya msimu wa 2019/20.
Bahati mbaya kwake ni Ndayiragije hakudumu sana Azam, na kocha alıyeritihi mikoba, Aristica Cioaba, hakumuweka kwenye mipango yake, hivyo dogo akarudi timu ya vijana.
Mapema mwaka 2020 kuna majaribio yalifanyika Uwanja wa Uhuru yakiendeshwa na watu kutoka Ulaya kwa ushirikiano na kituo cha Cambiaso Sports Academy cha Tanzania.
Tepsie kwa ruhusa ya klabu ya Azam, akaenda kushiriki na kuchaguliwa kwenda Ufaransa kwa majaribio zaidi.
Alienda kwenye klabu ya Nantes na kukutana na kina Randal Kolo Mwani wakati huo nao wakiwa akademi.
Tepsie akafanya majaribio na akafaulu na kuanza mazoezi na kina Kolo Mwani.
Bahati mbaya ndiyo ukaja mlipuko wa UVIKO 19 na Nantes ikawa moja ya klabu za kwanza kabisa kufunga ofisi zao ili kila mtu arudi nyumbani hadi hali itakapotulia.
Wakala aliyempeleka Tepsie klabuni hapo akataka kujaribu tena nafasi katika klabu zingine, ndipo akampeleka Poland na baadaye Uholanzi.
Lakini akili ya Tepsie ilishachagua kubaki Nantes kwa hiyo, huko kwingine ni kama alilazimishwa hivyo hakufanya jitihada kutoka moyoni.
Hii haikumfurahisha yule wakala ambaye akımlalamikia Tepsie kwamba anataka kucheza Nantes wakati wao hawataki kutoa hela…yeye kama wakala anataka hela.
Hapo ndipo mapishano ya Tepsie na huyo wakala yakaanza na wakati akiendelea kumzungusha Ulaya, hati yake ya kuishi huko ikaisha na akatakiwa kurudi nyumbani kuomba upya.
Na aliporudi ndiyo UVIKO 19 ikawa imechanganya kiasi kwamba hakuna watu walioruhusiwa kusafiri nchi yoyote.
Lakini baadaye hali ikatulia na dunia ikafunguka tena, Ila sio kwa Tepsie kwani yule wakala hakumpata tena hadi leo.
Msimu mpya wa 2020/21 ulipoanza ndipo Azam ikamtoa kwa mkopo kwenda Ihefu na baadaye kurudi msimu wa 2021/22 ulioanza chini ya George Lwandamina na baadaye Abdihamid Moallin.
Ni chini ya raia huyo wa Marekani mwenye asılı ya Somalia ndipo Tepsie alipoanza kufurahia tena maisha ya soka.
Mechi dhidi ya Simba, Januari Mosi 2022 pale kwa Mkapa, Tepsie akitokea benchi huku timu yake ikiwa nyuma 2-0, alibadili upepo huku alitengeneza bao pekee la timu yake lililofungwa na Rodgers Kola.
Baada ya hapo wakaenda kwenye Kombe la Mapinduzi na Tepsie alicheza mpira wa hali ya juu sana akiisaidia timu yake kufika fainali ikiwemo kuitoa Yanga kwenye nusu fainali.
Moto wa Tepsie ukawaka na aliporudi bara kwenye ligi hali ikawa balaa.
Kumbuka ushindi wa 4-0 wa Azam FC dhidi ya Tanzania Prisons kule Sumbawanga.
Sio tu kwamba Tepsie ndiyo alifunga bao la kwanza bali alichangia kwa kiasi kikubwa sana kuisambaratisha ngoma ngumu ya Wajelajela hao.
Msimu wa 2022/23 pia ulianza vyema sana kwa Tepsie alifunga mabao mawili na kutoa pası moja ya bao katika mechi mbili za kwanza.
Bahati mbaya nyingine kwake ikaja hapo, kwani kocha wake aliyempatia, Abdulhamid Moallin, akaondoka.
Akaja Mfaransa Denis Lavagne ambaye alimuona Tepsie kama namba 10 badala ya winga.
Hapo ndipo anguko la Tepsie lilipokuja. Mabadiliko ya nafasi yakamchanganya na akashindwa kurudi kwenye kiwango chake kile alichokuwa nacho chini ya Moallin.
Lavagne naye hakudumu, akaja Kali Ongala ambaye hakuona kabisa pa kumuweka. Hapo ndipo Tepsie akapotea jumla.
Msimu ukaisha na Azam ikaleta makocha wapya chini ya Yousouph Dabo ambaye naye akamuona bado ana utoto mwingi, hivyo akamtoa kwa mkopo akakue.
Tepsie akaenda KMC kwa mkopo kuungana na kocha Moallin ambaye chini yake mambo yalienda poa sana.
Lakini safari hii haikuwa hivyo, mambo yakakataa na Tepsie hakuwa yule tena wa zamani.
Msimu ukaisha na akarudi katika klabu ya Azam alikobakisha mwaka mmoja kwenye mkataba wa kuitumikia.
Azam wana imani sana na kijana huyo na sasa wakampa nafasi nyingine ya kujaribu bahati yake. Wamesainisha mwaka mwingine. Safari hii hawamtoi kwa mkopo, wanataka apate nafasi ya kufundishwa na Dabo huenda akambadilisha kama Yahya Zayd.
Kwa hiyo Tepsie ambaye mkataba wake ulikuwa uishe mwishoni mwa msimu huu wa 2024/25, sasa atakuwepo Azam hadi mwishoni mwa msimu wa 2025/26.
Kazi ni kwake sasa kuamua awe mchezaji mkubwa au shughuli yake iishie hapo.