UJIRANI MWEMA HIFADHI YA SAADANI WAZIDI KUZAA MATUNDA

Na Catherine Mbena /Saadani.

Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ikiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Jenerali (Mstaafu) George Marwa Waitara, jana Julai 24, 2024 ilitembelea Hifadhi ya Taifa Saadani kwa ajili ya kukagua utendaji kazi ambapo ilipata fursa ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya hifadhi hiyo.

Akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wajumbe wa bodi, Mkuu wa Hifadhi hiyo Afisa Uhifadhi Mkuu, Simon Aweda alisema ushirikiano kati ya Hifadhi ya Taifa Saadani na wawekezaji umewezesha kupiga hatua kubwa kimaendeleo ambapo wadau mbalimbali wamejitokeza kuunga mkono juhudi za uhifadhi na kuchagiza maendeleo ya utalii.

“Wadau wanaozunguka Hifadhi ya Taifa Saadani wamekuwa mstari wa mbele kuunga juhudi za uhifadhi na utalii ambapo kampuni ya sukari ya Bagamoyo sugar ilijitolea kugharamia vifaa pamoja na zoezi la ufungaji wa visukuma mawimbi “collar ” ambapo zaidi ya shillingi milioni 180 zilitolewa na wadau ikiwa ni gharama ya vifaa, wataalam walioshiriki zoezi hilo pamoja na helkopta iliyotumika katika zoezi hilo” alisema Mhifadhi Aweda.

Mhifadhi Aweda, aliongeza kuwa Bagamoyo sugar walienda mbali zaidi na kufanya matengenezo ya gari moja ambalo linatumika katika kufanya doria za kuzuia Wanyama waharibifu kabla hawajaingia mashambani na kuharibu mazao.

Aidha, Mhifadhi Aweda alibainisha kuwa Saadani Safari Lodge ambaye ni mwekezaji ndani ya hifadhi pia ilitoa kiasi cha shilingi milioni 39 kwa ajili ya ukarabati mkubwa wa uwanja wa ndege wa Saadani ambao kwa kiasi kikubwa uliharibiwa na mvua ambazo zilinyesha mwaka jana na mwaka huu 2024.

Uwanja huo umekuwa kwenye kiwango kizuri kuwezesha ndege zinazofanya safari katika hifadhi hiyo kutua wakati wote hata wakati wa mvua kubwa.

“ Kampuni ya Mount Kilimanjaro Safari Club pia wametusaidia kutatua tatizo la umeme kwa kuingiza umeme wa gridi ya Taifa katika geti la Madete ambapo hapo awali tulilazimika kutumia umeme unaotokana na nguvu ya jua pamoja na umeme wa jenereta ili kuendesha shughuli zote katika geti hili “

Mwenyekiti wa Bodi, Jenerali Waitara, alipongeza ushirikiano baina ya hifadhi na wawakezaji na kubainisha kuwa migogoro inarudisha nyuma maendeleo,

“Ninafurahi kuona mahusiano mazuri ya Saadani na wawekezaji hawa, niwapongeze sana kwa huu ushirikiano mzuri na majirani pale ambapo kuna jambo linawatatiza msisite kubisha hodi kwa majirani zenu ili tuone namna nzuri ya kutatua changamoto hizo. Sehemu yenye migogoro hutengana na maendeleo” alisema Waitara.

Aaron Kasasa, Meneja wa Shamba Bagamoyo sugar aliieleza Bodi ya Wadhamini namna ambavyo mwekezaji huyo anashirikiana na Hifadhi ya Taifa Saadani ili kuleta maendeleo ya pamoja

“Bagamoyo sugar na Saadani tuna mahusiano mazuri sana tunaamini maendeleo tuliyonayo ya haraka katika uzalishaji kiwandani kwetu msingi wake ni ushirikiano mzuri na majirani, tangu tunaanza mpaka sasa hatuna migogoro na hifadhi”.

Bodi ya Wadhamini TANAPA imepongeza utendaji kazi katika Hifadhi ya Taifa Saadani hususani juhudi zinazofanywa katika kuongeza idadi ya watalii ambapo
imeutaka uongozi wa hifadhi kuongeza jitihada katika kutangaza zaidi vivutio vya kipekee vilivyopo katika hifadhi ya Saadani ili kuongeza idadi ya watalii na kuunga mkono adhma ya serikali ya watalii milioni tano ifikapo 2025.

Mapema, bodi iliweza kutembelea miradi ya kimkakati inayotekelezwa na hifadhi hiyo ikiwemo ujenzi wa hosteli mpya kwa ajili ya wanafunzi, bwalo la chakula, pamoja na kukagua shughuli za matumizi bora ya maji baina ya mwekezaji Bagamoyo sugar na Hifadhi ya Saadani.

    

Related Posts