Watoto wawili wa familia moja wapotea Arusha

Arusha. Watoto wawili wa familia moja wamepotea katika mazingira ya kutatanisha mkoani Arusha, baada ya kuaga wanakwenda shule jana Julai 24, 2024, lakini hawakurudi nyumbani na mpaka leo hawajaonekana popote.

Watoto hao wanaosoma Shule ya Msingi Olosiva, wilayani Arumeru, wamedaiwa kupotea baada ya kupandishwa kwenye daladala wakielekea shuleni, lakini hawakufika shule na wala hawakurudi nyumbani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo amethibitisha kupokea taarifa hiyo leo Julai 25, 2025 asubuhi na wameanza kuifanyia kazi.

“Tumepata taarifa hiyo leo asubuhi na tunaifanyia kazi, tutakapopata chochote cha kuwaeleza tutawaambia kesho,” amesema SACP Masejo.

Akisimulia tukio hilo leo Alhamisi Julai 25, 2024, mama mzazi wa watoto hao, Elizabeth Modesta (31), amewataja watoto hao kuwa ni Mordekai Maiko (7) anayesoma darasa la tatu na Masiai Maiko (9) anayesoma darasa la tano.

Amesema jana aliwaandaa kwenda shule kama kawaida na kwenda barabarani kuwapakia kwenye daladala kuelekea shuleni.

“Kawaida saa 9:30 hadi au saa 9:45 jioni wanakuwa wamefika, lakini jana hadi saa 10 walikuwa hawajafika. Niliamua kwenda shule saa 11 jioni kuulizia nikaambiwa tangu asubuhi watoto hao hawajaonekana shule. Nikachanganyikiwa na kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi Ngaramtoni,” amesema mama wa watoto hao.

Amesema alipofika polisi walimtaka arudi nyumbani na kusubiri hadi saa 24 kama wasipoonekana ndio arudi kwa ajili ya kukata ripoti namba (RB Namba) na kuanza kutafutwa.

“Nilirudi nyumbani kulala na asubuhi nilikwenda tena shule kuulizia wakasema hawajawaona, ndipo nikarudi tena Polisi, nikapewa RB namba NGT/RB/1265/2024, wakataka picha za watoto, ili wasambaze mitandaoni na namba yangu, nikawapa, sasa nasubiri majibu,” amesema Elizabeth.

Mama huyo ametumia nafasi hiyo kuiomba Serikali na wananchi kumsaidia kuwapata watoto wake popote watakapoonekana.

“Kwa sasa napiga tu simu kwa marafiki wanisaidie kusambaza picha za wanangu, maana nimetembea kila mahala siwaoni. Naomba walimwengu wanisaidie, popote watakapowaona wanangu wanisaidie kuwapeleka polisi, maana nafsi yangu kwa sasa imeinama kwa kweli, namwomba tu Mungu wasidhurike huko walipo hadi niwapatikane,” amesema huku akilia kwa uchungu.

Mkuu wa shule ya msingi Olosiva, Mwenzine Msuya amesema tangu jana watoto hao wanajaonekana shuleni na leo wameuliza wanafunzi kwenye halaiki ya asubuhi (paredi), lakini wamesema hawajawaona.

“Hawa watoto hawana tabia ya kutofika shule kabisa na hata jana mama yao alipokuja kuuliza tukashangaa na leo asubuhi pia amekuja, hawapo. Tunaendelea kusambaza picha kwa ajili ya kutoa taarifa za kupotea kwao, yoyote atakayewaona awasiliane na mama yao au kituo chochote cha Polisi,” amesema mwalimu huyo.

Endelea kufuatilia Mwananchi kupata taarifa zaidi kuhusu tukio hili.

Related Posts