Dar es Salaam. Ni saa kadhaa za maswali, majibu, mapendekezo, maoni na uwasilishwaji wa changamoto kati ya wawekezaji wa ndani ya nchi na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kikiwa na washirika wake katika mkutano uliofanyika leo Julai 25, 2024 jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo wawekezaji wa ndani wamezitaja changamoto zinazowakabili ikiwemo kodi pindi wanapoagiza vipuri kutoka nje, kukosa uhakika wa kuaminika wa mikopo kutoka taasisi za kifedha, huku wakilinganisha na wageni kuaminiwa haraka wanapofika.
Aidha wamelia na utitiri wa kodi, sambamba na rundo la wakusanyaji wa kodi hizo kiasi cha kuwapa mawazo wanapokuwa wakiendelea na majukumu yao. Wametaka uwepo wa mkusanyaji mmoja.
Mmoja wa wawekezaji hao kutoka mkoani Kagera, Amir Hamza ambaye amewekeza katika kiwanda cha kahawa amedai benki za ndani, zinawaamini wawekezaji wa nje huku zikishindwa kuwapa uhakika wa mikopo wao wazawa.
“Kingine hatuna benki ya viwanda hapa Tanzania na jambo hili linatuumiza hususani sisi wazawa katika kuwekeza. Pia naomba bodi ya TIC ishauri Serikali kusiwe na mabadiliko ya mara kwa mara ya sera, kanuni, sheria za mazao na mfanyabiashara isibadilishwe mara kwa mara,” amesema Hamza.
Aidha, ameomba unafuu wa mafuta yanayotumika viwandani kwa ajili ya uzalishaji ili wawekezaji wa ndani waweze kushindana.
Aristarick Ndeliananga mwekezaji kutoka Woiso Original Products hapa jijini Dar es Salaam, amesema kuna utitiri wa wadai kodi jambo ambalo linafanya watumie muda mwingi kushughulika nao badala ya kujikita katika uzalishaji.
“Taasisi za Serikali ziko nyingi mfano, TRA, manispaa, mabango nafikiri kungekuwa na mkusanyaji mmoja ili kuepusha ushumbufu,” amesema Ndeliananga.
Akijibu hayo Ofisa Forodha kutoka TRA, Gift John amesema upo msamaha wa kodi kwa wawekezaji wanaoingiza vipuri vya mashine zao za uzalishaji.
“Kodi nyingine zote ikiwemo ya Ongezeko la Thamani (VAT), na nyingine ndogondogo mwekezaji huyu atazilipa kama kawaida,” amebainisha.
Amesema utaratibu uliopo hapa Tanzania ikifanyika uingizwaji wa kitu chochote kuna kodi ikiwemo RDL (kodi ya Maendeleo ya Reli) Import Duty, CPF. Hivyo wawekezaji wenye viwanda wanaoagiza vipuri wanasamehewa kodi ya Import Duty lakini zilizobaki zote atazilipa.
“Pia, ieleweke kwamba hakuna utitiri wa kodi bali zote zilizopo ziko kwa mujibu kisheria lakini pale panapohitaji maboresho tutazidi kuboresha kwa kadri muda unavyoruhusu,” amesema.
Kingine amepokea pendekezo la wawekezaji walio wengi waliogusia suala la ulipaji wa kodi zote kwa pamoja na utaratibu ulipo sasa wa kila mtu kukusanya kivyake, uondolewe amesema ni suala la kisera na linafanyiwa kazi.
Aidha, katika kutatua changamoto hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri amesema Kituo cha Uwekezaji kwa sasa kimeamua kufanya kazi kwa pamoja na taasisi nyingine za Serikali ili kuokoa muda na mzunguko kwa wawekezaji hao.
Amesema TIC inalo dirisha la pamoja ‘One Stop Centre’ ikiwa na taasisi za TRA, Brela, Wizara ya Kilimo, Madini, Baraza la Mazingira Nemc, Nida, Idara ya Uhamiaji, Shirika la Viwango TBS, zote zikiwa na dhumuni la kuimarisha uwekezaji.
“Kwa sasa kuna ongezeko la wawekezaji wa ndani na takwimu zinasema kuna Watanzania waliosajili miradi yao ni asilimia 58 katika mwaka wa fedha 2023/24.
“Pia, kituo kimesajili miradi ya uwekezaji 707 ikiwa ni ongezeko la asimia 91 kutoka miradi 360 mwaka uliotangulia wa 2022/23.
Amesema uwekezaji unaongoza katika sekta kuu tano huku ya kwanza ikiwa ni viwanda, uchukuzi pamoja na usafirishaji, majengo ya kibiashara, utalii na mwisho ikiwa ni kilimo.
Amesema kitendo cha kubadilishwa kwa sheria ya uwekezaji mwaka 2022 baada ya kufutwa ile ya mwaka 1997 imeipa nguvu sekta ya uwekezaji nchini, huku malengo yakiwa ni kumsaidia Mtanzania anayetaka kuwekeza kwa pesa kidogo aliyokuwa nayo.