Wawili waliohukumiwa kunyongwa kwa kuua waachiwa huru

Arusha. Mahakama ya Rufani imewaachia huru Simon Gabriel na Sagenda Bugalama, waliokuwa wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya kumuua William Musa.

Simon na Sagenda, walihukumiwa adhabu hiyo na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza Agosti 14, 2020 katika kesi ya mauaji iliyokuwa ikiwakabili.

Katika kesi hiyo, Simon, Sagenda na mwenzao Manyumba Magiki aliyefariki dunia kabla ya kusikilizwa Mahakama Kuu, walidaiwa kumvamia William aliyekuwa amemtembelea mjomba wake, Gabriel Fung’ho (shahidi wa tatu), wilayani Kwimba, Juni 26, 2010. Walivamia nyumba aliyokuwa amefikia na kumpiga kwa kutumia chuma.

Walidaiwa baada ya kutenda kosa hilo waliuweka mwili wa marehemu kwenye mfuko ‘kiroba’ na kuondoka nao. Ulipatikana Juni 30, 2010 katika Mto Ndagwasa.

Hukumu ya rufaa iliyowaachia huru imetolewa Julai 23, 2024 na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani wakiongozwa na Jaji Lugano Mwandambo, Lilian Mashaka na Gerson Mdemu.

Majaji hao walifikia uamuzi huo baada ya kupitia mwenendo wa kesi na kusikiliza hoja za pande zote mbili na kubaini upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kosa bila kuacha shaka.

Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani kwa kesi ya mauaji ya Willliam, Juni 26, 2010 katika Kijiji cha Lunele, Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.

Ilidaiwa kabla ya kifo hicho, William alikuwa mkazi wa Ngudu wilayani Kwimba, na siku ya tukio alikuwa amelala katika nyumba hiyo, wengine wakiwa kwenye kikao katika chumba kilichokuwa kimetandikwa magunia matupu kama mikeka.

Ilidaiwa nyumba hiyo ilikuwa na mlango uliokuwa na pazia lililotengenezwa kwa mwanzi, watu wawili waliwavamia na kumshambulia William kwa kumpiga na chuma.

Shahidi wa kwanza, alidai akiwa na wenzake waliokuwa sebuleni walikimbilia chumbani na kujificha nyuma ya magunia ya mchele, lakini walichungulia kwenye mlango uliokuwa wazi na kushuhudia kilichokuwa kinaendelea sebuleni.

Shahidi huyo ambaye ni Emanuel Simon (mtoto wa Simon), alimtaja baba yake na Mayunga kuwa ndio walimvamia William na kuwa aliwatambua kwa kupitia mwanga wa mbalamwezi na kudai baada ya kutenda kosa hilo walitishiwa kuuawa endapo wangemueleza yoyote hukusu tukio hilo.

Alidai mahakamani kuwa baada ya kutenda kosa hilo waliuweka mwili huo kwenye kiroba na kuondoka kwenda kusikojulikana kabla ya mwili huo kupatikana katika Mto Ndagwasa.

Kabla ya watuhumiwa hao kumvamia marehemu, shahidi wa tatu alidaiwa kukutana nao na kumtishia na kudai kuwa walimweleza kuhusu dhamira yao ya kumuua William aliyekuwa na ugomvi na mdogo wake, Sabuni Fang’ho.

 Shahidi alidai kuwa kwa kuogopa tishio la kuuawa, alikimbilia nyumbani kwake kwa ajili ya usalama wake.

Siku iliyofuata baada ya tukio, shahidi wa pili alidai kumuarifu shahidi wa tatu kutoweka kwa William akiwa na baiskeli yake kabla ya shahidi wa tatu kuripoti kupotea kwa mpwa wake aliyefariki.

Mtaalamu wa afya aliyeuchunguza mwili wa marehemu William alibaini ulianza kuoza, huku ukiwa na majeraha mgongoni na kwamba chanzo cha kifo kilikuwa ni kuvuja damu nyingi kutokana na majeraha.

Mahakama hiyo baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, iliwahukumu kunyongwa hadi kufa na ilitegemea ushahidi wa shahidi wa kwanza na pili waliodai kuwatambua na ushahidi wa mdomo wa shahidi wa kwanza hadi wa tatu kuhusu mazingira ya mauaji.

Katika hoja za rufaa, Simon na mwenzake waliwasilisha hoja nane ambazo baadaye kupitia mawakili wao zilipungua na kubaki hoja tatu.

Hoja hizo ni ushahidi dhaifu wa utambulisho uliomtia Simon hatiani, kosa katika kuthibitisha hatia kwenye maelezo ya onyo yaliyorekodiwa kinyume na sheria, kwani mshtakiwa hakuwa na shahidi huru na hoja ya tatu ni kesi dhidi yao ilitungwa haikuthibitishwa bila shaka yoyote.

Mawakili wao walieleza Mahakama kuwa mkanganyiko wa ushahidi wa mashahidi waliodai kushuhudia tukio hilo (shahidi wa kwanza na pili).

Kwa upande wao, mawakili wa mjibu rufaa walieleza Mahakama ya awali iliridhika kuwa ushahidi wa mashahidi hao wa utambuzi ulitosha kumtambua mhusika, kwani walikuwa wanamfahamu.

Kuhusu kukinzana kwa ushahidi wa mashahidi hao, alieleza mashahidi hao walikuwa wa kuaminika na walikwenda siku iliyofuata kwa mwenyekiti wa kijiji kutoa taarifa na kuomba majaji hao kutulipia mbali hoja hiyo.

Jaji Mwambando alieleza baada ya kusikiliza hoja zinazokinzana, hakuna ubishi kuwa shahidi wa tano alirekodi maelezo ya onyo kwa zaidi ya saa nne.

Alieleza katika mahojiano na mtuhumiwa na kisheria alipaswa kuomba kuongezewa muda, lakini hawakufanya hivyo.

Jaji alisema kushindwa kumhoji mtuhumiwa wa uhalifu ndani ya muda uliowekwa kunafanya taarifa hiyo isikubalike katika ushahidi, hivyo kufuta kwenye kumbukumbu kielelezo cha pili ambacho ni maelezo ya onyo ya mshtakiwa.

“Baada ya kufuta kielelezo hicho hakutakuwa na ushahidi wa kumhusisha Sagenda na mauaji ya William, hivyo tunaruhusu sababu hii ya pili ya rufaa,” alisema.

Jaji Mwandambo alieleza wanaona uhalali wa sababu zote za kukata rufaa na kufuta matokeo ya Mahakama ya awali kwa Simon na mwenzake na kuwa hawana hatia baada ya kuridhika ushahidi wa mashtaka haukuthibitisha kesi dhidi yao.

“Baada ya kueleza hayo tunabatilisha hukumu na kuweka kando hukumu za kifo zinazotolewa juu yao, tunaruhusu rufaa na kuamuru waachiliwe huru mara moja kutoka kizuizini,” alieleza.

Related Posts