AFARIKI AKIOTA MOTO NDANI YA GARI – MWANAHARAKATI MZALENDO

 

Thadei Mbawala (48) mkazi wa mtaa wa mji Mwema halmashauri ya mji wa Njombe ambaye ni dereva wa gari ya kampuni ya maji anadaiwa kufariki dunia ndani ya gari aliyokuwa amepaki nyumbani kwake pembeni kukiwa na jiko la mkaa (kigai) huku milango ya gari ikiwa imefungwa.

Catherine Haule ni mke wa marehemu ambaye amesema mumewe ana kawaida ya kuchaji redio pamoja na simu ndani ya gari kila anaporejea nyumbani kwa kuwa nyumba yake haina umeme lakini sio kwenda na ‘kigai’ pamoja na blanketi.

“Aliporudi jana saa tatu akawa anaendelea na shughuli zake na hapa ndani kuna kigai chake huwa anaota moto akirudi nikajua kipo kumbe mwenzangu alishachukua pamoja na shuka la watoto huko ndani,sina hili wala lile akaniambia mimi nachaji redio na kile cha kunyolea ndevu nikamwambia sawa mimi naenda kulala akasema tangulia ila milango usifunge”

Amesema mara baada ya kushtuka majira ya saa kumi na mbili asubuhi kutokana na kupitiwa na usingizi alishangaa kuona mume wake hayupo ndani lakini alipokwenda kwenye gari alifika na kuanza kumuita mume wake lakini milango ilikuwa imefungwa jambo lililomfanya aanze kuomba msaada kwa majirani waweze kumsaidia.

Aidha kwa upande wake Teophil Mwinuka ambaye ni Mtendaji wa kata ya mji mwema amesema mara baada ya viongozi kupata taarifa walifika eneo la tukio na kuwapigia simu kampuni ya maji ambao walifika na ufunguo mwingine wa gari walioutumia kufungua mlango na kukuta Mbawala akiwa ameshafariki.

Hata hivyo wakati tukio hili likitokea,kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe Mahamoud Banga alitoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Njombe wakati huu wa majira ya baridi kuchukua tahadhari kwenye matumizi ya jiko la mkaa katika maeneo yasiyo na hewa ya kutosha.

 

Related Posts