Dybala, Lukaku namba zilivyopishana | Mwanaspoti

ROMA, ITALIA: Supastaa Paulo Dybala, nyota wa kimataifa wa Argentina na Roma ya Italia anaujua mpira. Ndiye straika tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Wataliano hao, ingawa linapokuja suala la timu ya taifa anasugua sana benchi.

Kwa Roma, mastaa kibao wanakaa benchi wakisikilizia mwamba amalize kazi yake uwanjani ndipo waingie au anapokuwa majeruhi. Na hata Romelu Lukaku alipotua msimu uliopita kwa mkopo kikosini hapo alianza kusugua mbele ya mwamba huyo.

Lukaku alitua Roma akitokea Chelsea kwa mkopo ikiwa ni baada ya kuishi msimu mzima wa mwingine akiwa na Inter Milan. Hata hivyo, Dybala na Lukaku kuna mahala namba zao zinapishana sana tu kuanzia katika vikosi vya timu za taifa.

Kwa Ubelgiji, Lukaku ndiye straika tegemeo pale mbele akianza kikosini na kuwasugulisha benchi mastaa kibao wanaocheza katika ligi kubwakubwa Ulaya, lakini walipokuwa pamoja na Dybala Roma mambo yalikuwa tofauti, ingawa Dybala mara nyingi alikuwa majeruhi.

Katika msimu uliopita Dybala alicheza mechi 28 za Ligi Kuu Italia (Serie A) na kufunga mabao 13 akiwa na asisti tisa huku akiondoka na kadi zake tatu za njano, ilhali uliotangulia alicheza michezo 25, akafunga mabao 12 akiondoka na asisti sita na kadi za njano tano.

Ni Dybala huyohuyo aliyecheza mechi tisa za Europa League na kufunga mara mbili akitoa asisti moja msimu uliopita, lakini katika kile kinachoweza kukushangaza ni kwamba supastaa wa Kibelgiji, Romelu Lukaku ilibidi alalamike kusugua benchi mpaka jamaa apumzishwe.

Kutokana na malalamiko ya Lukaku, aliyekuwa kocha wa Roma, Jose Mourinho alilazimika kuanza kumpanga nyota huyo sambamba na Dybala, lakini kwa namba Mbelgiji huyo hakumfikia Muargentina huyo, hususan ushiriki wake uwanjani.

Katika hilo msimu uliopita Lukaku alicheza mechi 32 – nne zaidi ya Dybala ambaye alikuwa majeruhi, lakini alifunga mabao 13 na asisti tatu katika kikosi hicho cha ‘Watakatifu’ wa Roma.

Hii ina maana kwamba licha ya kucheza mechi nyingi walilingana mabao, lakini katika asisti Dybala alikuwa nazo tatu zaidi. Lukaku pia alimzidi straika huyo kwa kadi mbili zaidi za njano akiwa nazo tano. Katika Europa League, Lukaku alicheza mechi 13 akifunga mabao saba na asisti moja

Wakati Lukaku alicheza kwa msimu mmoja uliokuwa wa mkopo, pia aliifungia Roma bao moja katika mechi mbili za Kombe la Ligi (Coppa Italia), huku Dybala pia akitupia bao moja na asisti moja kama ilivyokuwa msimu wa 2022-23.

Namba za wakali hao haziishi hapo, kwani Lukaku anayetarajiwa kutua Napoli katika dirisha hili, iwapo mipango itakwenda vyema alikuwa na ‘dribolingi’ mara 56 katika msimu mzima, huku Dybala akifanya hivyo mara 62. Pia alimzidi Lukaku kwa mipira 16 zaidi aliyoingia nayo ndani ya boksi la penalti la adui akifanya hivyo mara 79 katika mechi 28. Namba za Lukaku pia zilikuwa tamu katika umiliki wa mpira ambapo alifanya hivyo kwa asilimia 73 dhidi ya 69.5 za Dybala.

Washambuliaji hao hawakuishia hapo, kwani walizidiana pia katika upokonyaji wa mipira, Lukaku akipokonya mara 201, lakini akipokonywa mara 87 huku Dybala akipora mipira mara 322 na kuporwa mara 77. Wote wawili waliporwa mipira kirahisi ndani ya eneo la 18 la adui mara 51. 

Related Posts