Dar es Salaam. Masoko ni miongoni mwa maeneo yanayozalisha taka kwa wingi maeneo ya mijini. Mfano, soko la Mabibo lililopo Manispaa ya Ubungo linakadiriwa kuzalisha tani 50 kila siku.
Kutokana na wingi huo, gari la taka hulazimika kwenda pale hadi mara nne kila siku, kwa mujibu wa Lawi Bernard, mkuu wa kitengo cha udhibiti wa taka ngumu na usafirishaji wa manispaa hiyo.
Hilo ni soko moja katika jiji lenye masoko 87 yanayosimamiwa na manispaa, likiwa pia na taka zinazozalishwa kwenye maeneo mengine.
Meneja wa Dampo la Pugu Kinyamwezi lililopo katika Manispaa ya Ilala, Richard Kishere anasema magari mengi wanayopokea pale hubeba tani sita hadi 25 za taka kila moja.
Sera ya Urejelezaji Taka Ngumu ya 2017 ya Dar es Salaam ilisema mkoa unakadiriwa kuzalisha zaidi ya tani 4,252 za taka kwa siku, kati ya hizo, ni asilimia 45 hadi 50 pekee zinazopokelewa katika dampo, sawa na tani 1,200 – 2,000 na zinazobaki huishia kwenye maeneo ya wazi, mitaro ya maji, barabara na makazi.
Ingawa hakuna takwimu za sasa, tovuti ya Tamisemi mwaka 2020 ilinukuu ripoti ya Benki ya Dunia (WB) ikionyesha Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa unakadiriwa kuzalisha zaidi ya tani 4,600 za taka kwa siku. Kati ya hizo, asilimia 45 hadi 50 ndizo zilizokuwa zinafikishwa kwenye dampo, sawa na wastani wa tani 2,000 tu hufika dampo.
Kwa mujibu wa Meneja wa dampo, wanapokea wastani wa tani 900 kwa siku za wikiendi na wastani wa tani 1,500 siku nyingine. “Kuna siku zinafika hadi tani 2,500 kama magari yakiwa mengi,” anaongeza.
“Tunapokea tripu (idadi ya magari) 100 hadi 120, lakini Jumapili yanaweza kuwa magari 65 hadi 75. Gari hizi zina ujazo wa tani sita hadi kubwa zaidi ambazo zipo chache ni tani 25,” anasema.
Hata hivyo, Kishere anasema taka zinazopelekwa dampo zimepungua miaka ya karibuni. “Miaka ya 2015 au kabla ya 2018 tulikuwa tunapokea hadi tripu 200,” anasema.
Dampo hili lina ukubwa wa hekta 65. Linaendeshwa kwa mtindo wa kupokea taka na kushindilia (controlled dumping), si dampo la kitaalamu (sanitary landfill), hali ambayo imesababisha milima ya taka hadi urefu wa mita 2-3 katika eneo la karibu hekta 45, hii ni kwa mujibu wa sera ya 2017.
Hali ya sasa ni tofauti. Mei 15, 2024 Mwananchi lilifika kwenye dampo. Siku hiyo kulikuwa na msururu wa zaidi ya magari 20 yanayotaka kuingia dampo. Harufu ya taka kali sana, lakini kulikuwa na harufu ya dawa fulani.
Licha ya kwamba mvua haikunyesha, kwenye barabara ya kuingia kwenye lango kuu la dampo usingeweza kupita bila kuvaa viatu maalumu (rain boot).
Ilimlazimu mwandishi kuzunguka njia ya pembeni inayopita kwenye makazi ya watu mpaka kwenda kuona yaliyomo ndani.
Alitaka kufahamu kwa nini kuna foleni na ndani kulionekana kuna utengenezaji wa mtambo wa kubebea taka. Pia milima ya taka ilionekana mpaka nje ya lango.
Kuhusu hali hiyo, Kishere anafafanua kwamba mashine za kushusha taka zilipata hitilafu. “Inapotokea kama hivyo huwa tunakodisha mashine na kukarabati zile zinazowezekana kufanyiwa matengenezo ya haraka.”
Akifafanua kuhusu foleni, anasema hakuna magari yanayokaa hapo kwa zaidi ya saa 8 hadi 12 na mashine zikiwa zinafanya kazi magari yanatoka ndani baada ya saa moja.
“Yapo magari yanarudi hadi tripu tatu. Sasa piga hesabu yanasubiri muda gani. Sehemu kama Kariakoo, panazalisha tani nyingi za taka, pale ukiacha usiku mmoja tu, nchi itasimama. Sasa gari yake ikija unafikiri itakaa muda gani?” anaeleza.
Kuhusu taka kujaa mpaka nje anasema, “Unaona hali ya dampo? Kipindi kama cha mvua njia za kuingia ndani hazipitiki. Je, tuzuie magari? Huwezi kuzuia, kwa hiyo eneo lile tumeweka ili magari (yashushe pale) yasikae, kipindi cha mvua kikiisha tutapeleka kwenye maeneo ya ndani zaidi.”
Kwa jumla huko dampo taka zinazopelekwa zinakuwa mchanganyiko, kinyume na sera na sheria.
Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya 2004 (114) inasema miongoni mwa wajibu wa Mamlaka za Serikali za Mtaa kwenye kusimamia na kupunguza taka ngumu, ni kuhakikisha taka zinachambuliwa na kutenganishwa kwenye chanzo chake.
Sheria hiyo inazitaka mamlaka za serikali za mtaa kufanya tafiti za mara kwa mara, ili kubaini aina za taka zinazozalishwa kwenye masoko, maeneo ya biashara na kutoa mbinu mwafaka za kutenganisha, kuhifadhi au kutupa taka hizo.
Hata hivyo, hali hii haipo dampo wala kwenye masoko mengi Dar es Salaam, jambo linalopoteza thamani ya taka nyingi zinazozalishwa.
Uchunguzi wa Mwananchi kwenye masoko 11 jijini Dar es Salaam umebaini ni soko moja tu la Tegeta Nyuki ndilo linafanya hivyo na hata hilo bado kiasi kingi cha taka hakipo kwenye mpango sahihi.
Soko hilo lina vizimba viwili vya kukusanya taka kwenye eneo la wazi pembezoni mwa barabara inayozunguka soko.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko hilo, Juma Hamza anasema maeneo hayo yamewekwa kwa lengo la kutenganisha taka.
“Zipo taka zinazopelekwa kwenye kiwanda cha kutengeneza mbolea cha Mabwepande na nyingine hupelekwa dampo,” anasema na kuongeza kuwa taka hizo hukusanywa na kuchukuliwa kila siku na magari ya manispaa.
Hata hivyo, licha ya kuwepo maeneo ya kutenganisha taka, hakukuwa na taka zilizotenganishwa kwa sababu sehemu zote mbili zilionekana kuwa na taka zinazooza na hivyo zote zinawezekana kupelekwa kiwandani.
Kwenye masoko mengine ya Temeke Sterio, Tazara Veterinary, Buguruni, Ilala -Boma, Mabibo, Kawe, Magomeni, Kisutu, Ungindoni na Kigamboni Ferry vilikuwepo vizimba vya taka, lakini hakuna sehemu za kuzitenganisha.
Utaratibu tofauti wa kukusanya taka ulikuwa kwenye soko la Kigamboni Ferry ambapo hakuna kizimba cha taka, badala yake kila mwenye biashara alifanya usafi na kuhifadhi taka mpaka gari litakapopita. Ratiba ya gari ni mara tatu kwa wiki, kwa mujibu wa katibu wa soko hilo, Ernest Makambala.
“Tulikuwa na kizimba cha muda, lakini kwa aina ya soko na ufinyu kilileta adha ya harufu na kuzagaa maji machafu,” anasema.
Akionyesha alipohifadhi taka kwenye mfuko maarufu wa salfeti, mama lishe kwenye soko hilo, Mwamvita Hamisi anasema njia hiyo imesaidia, kwani zamani kulikuwa na harufu ambayo anaamini iliwakimbiza wateja.
Hata hivyo, tofauti nyingine inaonekana kwenye masoko yenye vizimba hamishika (kontena) kama Soko la Magomeni, Kisutu na Tazara Veterinary.
Taka pia zinaweza kuzalisha nishati kwa mujibu wa Shirika la Ulinzi wa Mazingira la Marekani (EPA) na vyanzo vingine vya mamlaka ya ubadilishaji wa nishati. EPA inasema kiasi cha taka kinachohitajika kuzalisha nishati kinatofautiana kulingana na aina ya taka na teknolojia ya ubadilishaji.
Taka za mijini zinazalisha kWh 550-700 za umeme kwa tani katika mitambo ya kuzalisha nishati kutoka kwa malighafi hiyo. Biomasi, kama vipande vya mbao, inazalisha kWh 1,000-1,500 kwa tani. Gesi ya taka kutoka kwenye dampo inaweza kutoa takriban kWh 5-7 kwa tani kila mwaka.
Hii inamaanisha kwenye tani 1,000 zinazozalishwa kuna uwezekano wa kuzalisha megawatt 5 hadi 7 za umeme.
Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Taka na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Temeka, Mkana Mkana anasema wameweka taratibu za kutenganisha taka kwenye masoko, ila tatizo lipo kwa wanaozikusanya na kuziweka.
Mkana anasema, “unajua wanaopeleka taka ni wafanyabiashara au vijana waliowekwa na wafanyabiashara, sasa inategemea mtu, badala ya kuwekwa kwenye kontena anaweke chini.”
Mkana anasema kila mwezi wanafanya semina na wafanyabiashara na viongozi wao, angalau mara moja kwenye masoko yote kutoa elimu ya jambo hilo. Kutokana na ukubwa wa tatizo, Mkana anasema sasa wanatoa elimu kwa wanafunzi shuleni, akitaja shule ya Kibasila kuwa ya mfano.
“Kuwafundisha watoto tunaamini nao watafundisha wazazi, walezi na jamii,” alifafanua.
Kuhusu hilo, Lawi Bernard wa Manispaa ya Ubungo anahoji, “Mwandishi, pale (Soko la Mabibo) umeona taka ya plastiki?” Hapa tumerusuhu watu kukusanya taka za aina hiyo.”
Kwenye Soko la Kawe, kizimba cha taka nacho kipo karibu na barabara katika jengo moja linaloonekana kama fremu ambayo haijakamilika, na pembeni kuna fremu iliyokamilika na inafanya kazi.
Pamoja na hayo, Meneja wa Dampo, Charles Kichere anasema taka zinatakiwa kutenganishwa kabla hazijafika dampo.
“Zikifika pale zinashushwa magari yanaendelea na shughuli nyingine… yanakuja magari mengi yakiwa na taka zilizochanganywa,” anasema.
Kichere anaongeza kuwa baada ya kuona kuna taka nyingi zinazoweza kurejelezwa, wameweka utaratibu wa kuwaandikisha watu wote wanaokusanya taka zinazorejelezwa kutoka kwenye dampo, ili kuwafahamu na anasema wapo zaidi ya 1,500.
Haya yanafanyika licha ya sheria ya mazingira kutaka utenganishaji taka ufanyike kuanzia kwa mzalishaji wa taka husika.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Hudefo, Sarah Pima anasema mzalishaji wa kwanza ana jukumu la kutenganisha taka na hili litarahisisha kwa watumiaji wa bidhaa hiyo.
“… mfano kama tunatumia taka hizo kuzalisha mbolea, tutapunguza pia taka zinazokwenda dampo ambalo tunajua limezidiwa.
“Licha ya kwamba inasaidia kuweka mazingira vizuri, lakini inapunguza uzalishaji wa hewajoto ambayo inapatikana katika taka zinapooza na ni hatari kwa mabadiliko ya tabianchi,” anasema.
Anashauri wadau na Serikali kusimamia sheria ya mazingira, kwani ikitekelezwa tatizo litapungua.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917