Tanga. Mahakama Kuu, Kanda ya Tanga Agosti mosi, 2024 itatoa uamuzi wa ama kumpa dhamana Kombo Twaha Mbwana au kuamua iwapo shauri alilofungua mahakamani hapo kupitia mawakili wake dhidi ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) na wenzake lina uhalali au la.
Uamuzi huo utatolewa na Jaji Happiness Ndesamburo baada ya leo Januari 26, 2024 kusikiliza hoja za mawakili katika shauri lililofunguliwa na Kombo anayewakilishwa na mawakili tisa dhidi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, IGP, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Kabla ya uamuzi huo wa mahakama, mawakili wa mleta maombi, Peter Madeleka na Kamunyu Solomoni wakiwawakilisha wenzao walihoji ni kwa nini mteja wao ameshikiliwa na amenyimwa uhuru kinyume cha sheria.
Pia, mawakili hao wanataka Mahakama itoe amri ya kuzuia washitakiwa hao kuendelea kumshikilia mteja wao kwa muda mrefu kinyume cha sheria.
Madeleka alidai iwapo mteja wao anashikiliwa kinyume cha sheria mahakama itoe amri aachiwe na itoe amri ya nafuu yoyote itakayoona inafaa.
Wakili wa wajibu maombi Rashid Mohamed, alidai shauri hilo lililowasilishwa mahakamani chini ya hati ya usikilizaji wa dharura halina dharura kubwa, na haijaonyeshwa kama lilivyo neno lenyewe.
Ameieleza mahakama kesi ilishafunguliwa na mshitakiwa alishafikishwa katika mahakama ya Wilaya ya Tanga.
Ameieleza mahakama kuwa kesi ya jinai namba 19759 ya mwaka 2024 imefunguliwa na Jamhuri dhidi ya Kombo Mbwana Jumanne kwa jina lingine Kombo Twaha Mbwana.
“Julai 16, 2024 kwa mara ya kwanza mshtakiwa alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya Tanga, yupo mahabusu kwa sababu hakukidhi vigezo vya dhamana, tena mahabusu ya Maweni Tanga,” wakili huyo ameieleza mahakama.
Amedai uwepo wa kesi hiyo unalifanya shauri la maombi hayo (ya Kombo) kupitwa na muda na hata kilichoombwa kimeshafanyika.
Wakili Mohamed amedai, “Tunafahamu mahakama hii inaweza kuingilia utoaji dhamana ila inaweza kutolewa endapo mstakiwa atakidhi masharti ambayo yataweza kukubaliana na mahakama ya chini. Upande wa wajibu maombi tunaona yamepitwa na muda.”
Mbali ya hilo, ameiomba mahakama kuwapa wajibu maombi muda wa siku 14 ili kuwasilisha kiapo kinzani ili kujibu hoja za mleta maombi.
Wakili Madeleka akijibu hoja hizo, amedai kesi ya jinai iliyopo Mahakama ya Wilaya Tanga haimuhusu mteja wao Kombo Twaha Mbwana, bali Kombo Mbwana Jumanne.
Amedai hata kama ingemuhusu mteja wao, wanaomba apatiwe dhamana.
Baada ya Jaji Ndesamburo kusikiliza hoja za pande zote mbili amesema atatoa uamuzi Agosti mosi, 2024.
Awali shauri hilo lilipangwa kusikilizwa mahakamani hapo Julai 23, 2024 lakini liliahirishwa hadi Julai 26, kutokana na jaji kutokuwapo. Iliahirishwa mbele ya Naibu Msajili wa mahakama hiyo, B.R. Nyaki.
Kombo alitoweka Juni 15, 2024 baada ya watu wasiojulikana kudaiwa kumteka akiwa nyumbani kwake Kijiji cha Kwamsala wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga.
Julai 14, 2024 Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Zacharia Bernard alitangaza kuwa wanamshikilia kwa tuhuma za kutumia vifaa vya kielektroniki na laini za simu za mitandao mbalimbali zisizo na usajili, kutekeleza uhalifu huo kinyume cha sheria za nchi.
Kombo baada ya kufikishwa mahakamani Julai 16, alisomewa mashtaka kwa makosa matatu likiwamo kushindwa kutoa taarifa za kutosha za akaunti ya kadi yake ya simu, kinyume cha kifungu cha 126 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta. Anadaiwa kutenda kosa hilo Juni 9, 2024 katika Mtaa wa Hassan Ngwilizi ndani ya wilaya na Mkoa wa Tanga.
Anadaiwa alikutwa akimiliki laini ya Tigo ikiwa na namba (ICCID), 8925502042093621824 iliyosajiliwa kwa jina la Shukuru Kahawa na kushindwa kutoa maelezo ya kutosha kuhusu umilikiwa wa laini hiyo.
Pia anadaiwa kushindwa kusajili laini ya simu ambayo awali ilikuwa ikimilikiwa na mtu mwingine.
Pia kushindwa kuripoti mabadiliko ya umiliki wa laini ya simu.
Baada ya kusomewa mashtaka alipewa masharti ya dhamana akitakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh2 milioni kila mmoja, wenye barua ya mtendaji wa mtaa na vitambulisho vya Taifa (Nida). Alishindwa kutumiza masharti ya dhanama akapelekwa mahabusu.