JANUARI 26, 2022 Simba ilimtangaza Imani Kajula kuwa ofisa mtendaji mkuu (CEO) wa klabu alikichukua nafasi ya Barbara Gonzalez aliyejiuzulu Desemba 10, 2021.
Hadi Agosti Mosi, mwaka huu, siku ambayo ataachia ngazi katika nafasi hiyo atakuwa ametimiza siku 913 tangu ashike nafasi iliyoachwa na Barbara, huku akishindwa kufikia mafanikio yaliyofikiwa na mtangulizi wake.
Tangu aingie madarakani Kajula ameonja furaha mara mbili, ikiwa ni kutwaa Ngao ya Jamii na Kombe la Muungano lililoibuka ghafla katikati ya msimu, huku Simba ikishindwa kutetea mataji matatu ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho. Simba ambayo ipo Misri kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa 2024/25 imepoteza mataji matatu mfululizo mbele ya Yanga ikiwakilisha nchi Ligi ya Mabingwa Afrika misimu miwili mfululizo na msimu huu ikiangukia Kombe la Shirikisho.
Hapa chini ni baadhi ya mambo matamu na machungu aliyopitia Kajula chini ya utawala wake ndani ya Simba.
Simba mara ya mwisho kutwaa taji la ligi ni chini ya Barbara ambaye aliipa mataji manne mfululizo. lakini baada ya kuamua kuachia ngazi timu hiyo imekuwa ikipata shida mbele ya Yanga.
Ndani ya misimu mitatu chini ya Kajula, Simba imeshinda taji moja la Ngao ya jamii mbele ya watani zao, Yanga ikiwa chini ya Nasreddine Nabi anayeino Kaizer Chiefs ya Sauzi.
Misimu miwili ya mwanzo aliiongozi timu hiyo ikimaliza nafasi ya pili kwenye msimamo na kuipeleka Ligi ya Mabingwa Afrika ikiishia robo fainali, lakini msimu ulioisha amekwaa kisiki akiisaidia kumaliza nafasi ya tatu na itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Tangu atue Simba ushindi alioupata mbele ya Yanga ni kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii ikiwa chini ya Nabi mchezo uliochezwa Agosti 13, 2023.
Simba ilitwaa taji hilo mbele ya Yanga kwa penalti 3-1 baada ya dakika 90 kumalizika timu hizo bila kufungana.
Baada ya hapo Simba wamekuwa wanyonge mbele ya Yanga kwani msimu ulioisha mechi zote mbili wamekubali vichapo wakifungwa mabao 5-1 mzunguko wa kwanza na mabao 2-1 mzunguko wa pili.
Simba ndani ya misimu mitatu iliyokosa mataji imefanya usajili mbalimbali, lakini imeshindwa kupata mafanikio katika usajili huo ingawa kuna ambao ulikuwa na mafanikio.
Katika usajili wwa hivi karibuni uliofanikiwa zaidi ni wa beki wa kati wa timu hiyo, Che Malone, Henock Inonga na kipa Ayoub Lakred na ndio zaidi kwa Simba katika misimu mitatu iliyopita.
Kati ya wachezaji hao, Inonga ambaye ameuzwa na timu hiyo kwenda FAR Rabat amehudumu Simba kwa misimu miwili, Malone pia ameitumikia timu hiyo kwa misimu miwili huku Ayoub akiwa na msimu mmoja ambapo wameonyesha uwezo mkubwa.
Kwenye mambo mazuri huwezi kukosa pia upungufu na hii ni kwa upande wa usajili mbovu Simba ambao imeufanya, mwingi ambao haukuwalipa na wachezaji hao waliishia kuwa watalii ndani ya kikosi hicho.
Dejan Georgijevic, Victor Akpan, Mohamed Ouattra, Babacar Sarr na Pa Omar Jobe ni baadhi ya majina ya wachezaji wa kigeni ambao walitajwa kuja kufanya mambo makubwa ndani ya kikosi cha Simba, lakini imekuwa tofauti na baadaye wakajikuta wanatimuliwa.
Licha ya Simba kutajwa kuwa miongoni mwa timu bora Afrika kutokana na mafanikio ya hivi karibuni hasa kwenye michuano ya kimataifa, ndiyo timu ambayo imenolewa na makocha tisa ndani ya misimu sita.
Chini ya Kajula imefukuza makocha watano ikiwa ni wageni wanne na mzawa mmoja ambaye walimuondoa timu ya wakubwa na kumpeleka timu ya vijana.
Makocha hao ni Pablo Franco alitua kuinoa Simba akahudumu miezi sita ndani ya kikosi hicho baada ya Mei 2022 kutimka na nafasi yake kuchukuliwa na Zoran Maki Juni 22 na kuondoka Septemba 22 ikiwa ni kocha aliyedumu kwa muda mfupi zaidi.
Septemba 2022, mzawa Juma Mgunda alipata nafasi ya kuifundisha Simba akihudumu kwa miezi mitano na kujiwekea rekodi ya kuiongoza timu hiyo katika michezo 18 na kati ya hiyo alifungwa moja, akaachana nayo Januari 2023.
Ilipofika Januari 2023 Simba ilimtangaza Roberto Olivieira ‘Robertinho’ ambaye aliiongoza kwenye mechi 12 akishinda michezo saba, akifungwa mmoja dhidi ya watani wao Yanga kwa mabao 5-1 na hapo ndipo ikawa safari yake imeishia.
Baadaye Abdelhak Benchikha alitua na kudumu kwa siku 157 tangu alipoajiriwa Novemba 24 alipotambulishwa siku nne baadaye akichukua nafasi ya Robertinho.
Benchikha aliiongoza timu hiyo katika michezo 21 ya mashindano yote ikiwemo Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ligi ya Muungano iliyorejea mwaka huu.
Katika Ligi Kuu Bara aliiongoza katika michezo 11 na kati ya hiyo alishinda sita, sare tatu na kuchezea vichapo mara mbili huku akifunga mabao 18 na kuruhusu nyavu za kikosi hicho kutikiswa mara nane.
Ni michezo miwili ya Ligi Kuu Bara ambayo Benchikha hakuiongoza Simba ikiwa ni Machi 9, 2024 dhidi ya Coastal Union ambapo timu hiyo ilishinda kwa mabao 2-1 na ushindi wa 3-1 mbele ya Singida Fountain Gate katika mchezo uliopigwa Machi 12, mwaka huu ambapo aliomba kuondoka na nafasi yake kuchukuliwa na Mgunda ambaye alimalizia msimu na msimu ujao Simba itakuwa chini ya kocha mpya Fadlu Davids.
Kajula ambaye ni mwanachama wa muda mrefu wa Simba na mbobezi katika masuala ya benki na masoko akiwa na uzoefu wa kutosha aliouvuna baada ya kuhudumu katika taasisi mbalimbali. Pia ni mzoefu kwenye masuala ya uongozi wa mpira kwani aliwahi kuwa kwenye Kamati ya Maandalizi ya Michuano ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (Afcon U17) iliyofanyika nchini 2019.
Akiwa mkurugenzi wa kampuni ya mawasiliano na masoko ya EAG Group, Kajula alikuwa sehemu ya maandalizi ya Wiki ya Simba mpaka kilele chake (Simba Day), mwaka jana na kampuni hiyo ndiyo ilitengeneza mitandao ya kijamii ya klabu hiyo.
Mwaka 1999 hadi 2003 alikuwa meneja masoko wa Benki ya CRDB, na kati ya 2003 hadi 2006 akawa mkurugenzi wa masoko na biashara wa Benki ya Posta Tanzania (TPB) na 2006 hadi 2013 alikuwa mkuu wa masoko na mawasiliano wa NMB. Hadi wakati Simba inamteua kuwa mtendaji mkuu wake alikuwa mkurugenzimMtendaji wa EAG Group aliyoingoza tangu 2013.