Kaeni kwa kutulia sasa! | Mwanaspoti

WAKATI timu za Ligi Kuu Bara zikiendelea kujifua kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano, wawakilishi wanne wa Tanzania katika michuano ya kimataifa Simba, Yanga, Azam na Coastal Union zinajiandaa kufunga hesabu za maandalizi kabla ya kuanza mchakamchaka wa mashindano ya msimu mpya.

Yanga iliyopo Afrika Kusini na Azam iliyoweka kambi Morocco zitashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Simba iliyojichimbia Misri na Coastal iliyopo Pemba zitacheza Kombe la Shirikisho Afrika baada ya wababe hao wanne kumaliza nafasi nne za juu za Ligi Kuu iliyopita.

Kama hujui timu hizo ndizo zitakazoumana kwenye mechi za Ngao ya Jamii kati ya Agosti 8-11, Simba na Yanga zikipepetuana kuanzia Saa 1:00 usiku Kwa Mkapa, huku Azam na Coastal zikiumana Saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar.

Washindi wa mechi hizo za Agosti 8 ndizo zitakazocheza fainali kupata bingwa wa michuano hiyo kwa msimu huu na kuzindua rasmi Ligi Kuu Bara 2024-2025, wakati zitakazopoteza itavaana kusaka mshindi wa tatu, mechi zote zikipigwa Kwa Mkapa jijijini Dar es Salaa siku ya Agosti 11.

Kambi za timu hizo zilizopo nje ya maskani zao, zinatarajiwa kuvunjwa kuanzia Julai 31 na Agosti Mosi kabla ya timu zote kujiandaa na mechi hizo za Ngao sambamba na nyingine za matamasha ya kutambulisha vikosi vipya hasa kwa vigogo, Simba itakayofanya Agosti 3 na Yanga italiamsha siku inayofuata (Agosti 4).

Mwanaspoti kupitia makala haya linakuletea mwanzo mwisho wa maandalizi ya timu hizo na namna zinavyomalizia maandalizi yake ‘Final Touch’ kabla ya kazi kuanza kwa msimu mpya wa 2024-2025, kwani kila moja inacheza mechi wikiendi hii na kumalizika mwanzoni mwa wiki kabla ya kujipanga kwa mengine.

Mabingwa hao wa misimu mitatu mfululizo wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho kwa sasa wapo Saudi walikoenda kumalizia kambi iliyoanzwa wiki tatu nyuma katika viunga vya Avic Kigamboni, Dar es Salaam.

Baada ya kujifua vyema Kigamboni, Julai 18 Yanga ilisafiri hadi Sauzi kuendelea kujifua, ikicheza mechi mbili zakirafiki za kimataifa za michuano ya Kombe la Kimataifa la Mpumalanga.

Yanga ilicheza mechi ya kwanza Julai 20 dhidi ya FC Augsburg ya Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga) na kulala mabao 2-1, bao pekee la Yanga lilifungwa na mshambuliaji mpya Jean Baleke.

Mchezo uliofuata ulipigwa Julai 24 ikiumana na wenyeji TS Galaxy iliyopo Ligi Kuu Afrika Kusini (PSL) na kushinda 1-0, bao pekee la nyota mpya kikosini Prince Dube.

Na kesho timu hiyo itamalizia mechi ya mwisho kwa kambi ya Sauzi kwa kucheza na Kaizer Chiefs kuwania ubingwam wa Kombe la Toyota na baada ya hapo Wananchi wataanza taratibu za kurejea nchini Julai 31 ili kujiandaa na maandalizi ya Kilele cha Wiki ya Mwananchi itakayofanyika Agosti 4 na kufuatia na Ngao.

Baada ya mechi hizo mbili za awali, kocha mkuu wa Yanga Miguel Gamondi alisema michezo hiyo imempa kitu alichokihitaji na anaamini timu yake inazidi kuimarika.

“Mchezo wa kwanza tulicheza vizuri lakini tukafanya baadhi ya makosa yaliyotunyima ushindi. Mchezo wa pili tumeshinda na tumecheza vizuri. Tunaendelea kuandaa timu na ninaimani tutakuwa bora zaidi,” alisema Gamondi.

Nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto alisema; “Timu iko vizuri na muunganiko ni bora kati ya wachezaji wapya na waliokuwepo. Nawaomba mashabiki zetu wajitokeze kwa wingi kwenye kilele cha wiki ya Wananchi waione timu yao.”

Kikosi hicho kimeongeza nguvu kwa kuwasajili kipa Abubakar Khomeiny, beki Chadrack Boka na viungo Aziz Andambwile, Duke Abuya na Clatous Chama sambamba na washambuliaji wawili, Baleke na Dube.

Matajiri hawa wa Chamazi nao hawalazi damu, walianzia kambi ya msimu mpya viunga vya Azam Complex kisha kwenda Zanzibar na kucheza mechi dhidi ya Zimamoto na kushinda 4-0 kabla ya kupaa hadi Morocco ilipo hadi sasa.

Ikiwa huko Morocco imekuwa ikijifua na kujenga kikosi chake ikiwemo kucheza mechi ya kirafiki moja iliposhinda 3-0 dhidi ya US Yacoub Mansour ya huko kwa mabao ya Blanco, Cheikhe Sidibe na Djibrill Sylla na leo Jumamosi  itacheza tena mchezo mwingine dhidi ya Union Touarga na itamalizia kazi keshokutwa Jumatatu kwa kuumana na mabingwa wa zamani wa Morocco na Afrika, Wydad Casablanca.

Baada ya hapo Azam itapita Kigali, Rwanda kucheza mchezo mmoja Agosti 3 na Rayon Sport inayonolewa na kocha wa zamani wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, wakiitumia kutambulisha kikosi kipya cha Azam (Azamka in Rwanda) kabla ya kurejea nchini tayari kwa kuanza kuliamsha.

Katika dirisha la usajili, Azam imeongeza nyota wanane katika kikosi hicho akiwamo; Nassor Saadun, Adam Adam, Jhonier Blanco, Ever Meza, Frank Tiesse, Yoro Diaby, Cheikna Diakite na Mamadou Samake.

Kocha wa Azam Bruno Ferry alisema maandalizi ya msimu mpya yanaendelea vyema na sasa anasubiri ligi ianze timu ikapige kazi.

“Tumekuwa na maandalizi bora tangu siku ya kwanza, tunaendelea kujifua kabla ya ligi kuanza ila kiufupi tupo tayari kuanza msimu mpya,” alisema Ferry.

Beki kiraka wa Azam, Nathaniel Chilambo alisema msimu ujao utakuwa bora zaidi kwao kutokana na walivyojiandaa.

“Tunatarajia kuwa na msimu mzuri. Tumejipanga kama timu kufanya hivyo lakini pia maboresho yaliyofanyika yana tija kwa klabu,” alisema Chilambo.

Wekundu wa Msimbazi baada ya kuboronga misimu mitatu iliyopita sasa wamefanya mabadiliko yatakayowapa heshima msimu ujao.

Ukiachana na mabadiliko ya benchi la ufundi linaloongozwa na Msauzi, Fadlu Davids, Simba pia imefanya usajili wa wachezaji kibao kwaajili ya msimu mpya.

Simba imeweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya katika mji wa Ismailia, Misri na huko imekuwa ikijifua ili kurejesha ufalme wa Msimbazi.

Ikiwa huko Simba tayari imecheza mechi moja ya kirafiki na kushinda 3-0 dhidi ya Canal SC kwa mabao ya Augustine Okejepha na Charles Ahoua aliyefunga mawili.

Katika siku tano zilizobaki, Simba itacheza mechi nyingine mbili za kirafiki na baada ya hapo itafunga hesabu na kurejea nchini kuanza kazi kwenye Simba Day Agosti 3.

Mastaa wapya ndani ya Simba ni Valenteno Nouma, Abdulrazak Hamza, Karaboue Chamou, Kelvin Kijiri, Yusuph Kagoma, Deborah Fernandez, Augustine Okejepha, Omary Omary, Awesu Awesu, Ahoua, Joshua Mutale, Steven Mukwala na Valentine Mashaka.

Kocha Fadlu  alikaririwa akisema amefurahia kwa jinsi kikosi hicho kipya, huku akisema hadi ligi inaanza kila kitu kitakuwa sawa.

“Nafurahia kuwa na hii timu. Kila mmoja yupo tayari kufanya kazi na tumepata muda wa kuzoeana na kuwa kitu kimoja. Tunaimarika kadri siku zinavyosonga na naamini hadi mashindano rasmi yanaanza tutakuwa imara,” alisema Fadlu.

Nahodha wa timu hiyo, Mohamed Hussein ‘Zimbwe JR’ alisema kikosi kimebadilika na ushindani umeongezeka huku akiwataka mashabiki wa chama hilo kuwa na subra mambo mazuri yanakuja.

“Kikosi kimebadilika sana. Ila tunaendelea kusomana na kuzoeana zaidi. Ushindani umeongezeka na kila mtu anatimiza vyema majukumu yake hivyo masubiri wakae mkao wa kula,” alisema Zimbwe.

Wagosi wa Kaya, hata wao nao hawapoi. Baada ya kuanza maandalizi ya msimu mpya jijini Tanga, kisha kushiriki michuano ya Kagame Cup iliyopigwa Dar es Salaam baadae ilivuka maji hadi Zanzibar ili kujifua zaidi katika kisiwa cha Pemba.

Mabosi wa klabu hiyo walisema wameenda huko kwa vile mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam itapigwa kwenye Uwanja wa Amaan, hivyo wameenda kuzoea mazingira kabla ya kucheza mchezo huo, hivyo ile mipango ya kuweka kambi mjini Mombasa, Kenya ilifutwa.

Kikosi hicho kimepanga kufanya vizuri zaidi msimu ujao na inaelezwa kipo mbioni kushusha kocha mpya atakayesaidiana na Mkenya David Ouma.

Timu hiyo iliyomaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu msimu uliopita imefanya usajili wa nyota kadhaa wakiwemo Athuman Msekeni, Haroub Mohamed, Mukrimu Issa, Ramadhan Mwenda, Mbaraka Yusuph, Abdallah Hassan na Anguti Luis.

Coastal ikiwa humo imepanga kucheza mechi kadhaa za kirafiki kabla ya kuvaana na Azam katika Ngao ya Jamii kisha kurejea Bara kwa mechi inayofuata ya michuano hiyo na baadae kuliamsha katika Ligi Kuu Bara itakayoanza Agosti 16.

Kiungo wa klabu hiyo, Lucas Kikoti alisema maandalizi yao yanalenga kufanya vizuri zaidi msimu ujao na wachezaji wako tayari.

“Tunaendelea vizuri na tumepata mechi za kutosha za kirafiki kuweza kujua muenendo wa kikosi chetu kwani malengo ni kufanya vizuri zaidi ya tulichofanya msimu uliopita,” alisema Kikoti.

Straight mpya wa timu hiyo, Mbaraka Yusuph alisema kila mchezaji ndani ya kikosi anapambania namba hivyo itakuwa timu shidani zaidi.

“Kila mtu ndani ya kikosi hiki anapambania nafasi, kwa wale wapya na hata waliokuwepo. Hilo linafanya ushindani uongezeke na kuimarisha timu zaidi,” alisema.

Kiungo wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Amri Kiemba alisema kila timu itavuna ilichopanga kutoka kwenye usajili na maandalizi ya msimu mpya.

“Karibu kila timu imesajili na baada ya hapo zimepata muda wa kwenda pre season hivyo tusubiri kuona matokeo na hapo ndipo tutajua uwezo wa kila timu,” alisema.

Kocha wa zamani wa Yanga Kenny Mwaisabula alisema: “Kutakuwa na mabadiliko kwa kila timu na hilo litazua mitazamo tofauti baada ya ligi kuanza. Mashabiki watatoa maoni baada ya kuziona timu vivyo hivyo kwa wadau jambo ambalo kila kocha na mchezaji anatakiwa kulipokea na kulifanyia kazi.

Kocha wa zamani wa Coastal na Simba, Juma Mgunda alisema licha ya kuwa na pre season lakini matokeo yake yanaweza yasionekane katika mechi za kwanza.

“Sidhani kama mechi za mwanzo ni kipimo sahihi cha kuwapima walimu na wachezaji wa timu flani. Wakati mwingine mambo huchanganya katikati hivyo tisiwe na presha tusubiri mechi zichezwe na hapo tutapata la kusema,” alisema Mgunda.

Related Posts