Sengerema. Kaya 315 kati ya 1,305 katika kata ya Igulumuki iliyopo Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza hazina vyoo na wakazi wake wanajisaidia kwenye vichaka na milimani.
Kata ya Igulumuki ni miongoni mwa kata 26 zinazounda wilaya ya Sengerema, ina kaya 1,305, watu 13,705 ambapo kaya zenye vyoo bora ni 254, zenye vyoo vya asili 254, zenye vyoo vya mabanzi 151 na 351 hazina vyoo kabisa.
Hayo yamebainishwa na Ofisa Afya wa Kata ya Igulumuki, Alice Mwanisawa alipokuwa akisoma taarifa ya kata hiyo kwenye mkutano wa mbunge wa Sengerema (CCM), Hamis Tabasamu, wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwenye jimbo lake.
Amesema ukosefu wa vyoo kwenye kaya hizo, unahatarisha maisha ya wakazi wake na huenda wakakumbwa na magonjwa ya mlipuko hasa kipindupindu.
Alice amesema waliamua kufanya sensa katika kata hizo ili kubaini kaya zilizo na changamoto ya kutokuwa na vyoo, lengo likiwa ni kutoa elimu ambayo itahamasisha kaya hizo kuchimba vyoo bora.
“Licha ya kutoa elimu kuhusu umuhimu wa choo, kila kaya imepeleka majina ya wakuu wa kaya kwenye ofisi ya mtendaji wa kata ya Igulumuki kwa hatua zaidi za kisheria,” amesema Mwanisawa.
Baadhi ya wananchi wamesema watu ambao hawana vyoo ni asili ya wafugaji, kutokana na asili yao, huwa hawaoni umuhimu wa kuwa na vyoo, hivyo elimu inatakiwa kutolewa kwenye jamii hiyo.
Mkazi wa Kitongoji cha Ijinga C, Amos John, amesema kaya kutokuwa na choo ni uzembe wa mkuu wake ambaye anatakiwa achukuliwe hatua za kisheria kwa kutojua umuhimu wa kuwa na choo bora.
“Tunahamasishwa kila mara kaya kuwa na vyoo, kinachotushangaza ni hizo kaya kutokuwa na vyoo hadi sasa. Serikali inatakiwa kuwachukulia hatua wakuu wa kaya ambazo hazina vyoo,” amesema John.
Kwa upande wake, Anastazia Sylvester amesema watu wanaoathirika na kata kukosa vyoo ni akina mama na watoto ambao muda wote wanakuwa mazingira ya nyumbani wakifanya shughuli mbalimbali na hawapati muda wa kwenda porini au mashambani ili wakatimize haja hiyo.
Amewaomba viongozi wa kata hiyo kuendelea kuhamisha wananchi wa kata hiyo kuwa na vyoo bora, ambavyo vitawasaidia kujikinga na magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Ijinga C, Dotto Mwandagwa amesema kitongoji chake kina baadhi ya kaya zisizo na vyoo, amekuwa akitoa elimu mara kwa mara kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuwa na vyoo. “Baadhi wa wananchi ni wagumu kupokea elimu ya uchimbaji wa vyoo, tunaomba Serikali iingilie kati kuwachukulia hatua watu ambao hawana vyoo kwenye kaya zao,” amesema Mwandagwa.
Kufuatia hali hiyo, Tabasamu amesema ni aibu kwa familia hizo kutokuwa na sehemu maalumu ya kupata huduma ya faragha, hivyo amemwagiza mtendaji wa kata hiyo, Renatus Mkama, atumie sheria ndogondogo kuzibana kaya hizo zichimbe vyoo na kuacha kujisaidia vichakani.
Amesema kazi ya mbunge ni kutunga sheria na kuwaletea maendeleo wananchi, lakini suala la kuhamasisha uchimbaji wa vyoo ni la mwananchi mwenyewe.
“Ni aibu kaya 315 hazina vyoo katika kata nzima ya Igulumuki, mtendaji wa kata upo, jitathmini utendaji kazi wako,” amesema Tabasamu.
Akizungumzia jambo hilo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Igulumuki, Renatus Mkama, amesema amefanya mikutano kadhaa na wananchi kuwahamasisha kuchimba vyoo ili kuepuka kujisaidia vichakani au milimani.
“Baada ya kutoa elimu, nimetoa siku 14 kila kaya ambayo haina choo, iwe imekamilisha kujenga choo, baada ya hapo tutachukua hatua za kisheria. Tuna sheria ndogondogo ndani ya halmashauri yetu, kaya isiyo na choo itatozwa faini ya Sh50, 000, hivyo sheria hiyo tunakwenda kuitekeleza,” amesema.
Hata hivyo, Ofisa Afya Wilaya ya Sengerema, Ester Maginya, amesema ni kosa kisheria kaya kutokuwa na choo, na kosa hilo likithibitika mahakamani, mkuu wa kaya atalipa faini ya Sh200,000 huku faini ndogo ya halmashauri ikiwa Sh50,000.
“Tunatakiwa tuendane na sera ya Serikali yetu ya kila mtu kuwa na choo bora ili kuboresha maisha,” amesema Maginya.