Geita. Mtoto mchanga anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi miwili amekutwa ameuawa kwa kunyongwa kisha kukatwa mkono na mguu, vyote vya upande wa kulia, kutupwa shambani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Saphia Jongo, amesema tukio hilo lilitokea Julai 22, 2024 katika Kitongoji cha Myenze, Kata ya Katome, Bukombe mkoani Geita.
Kwa mujibu wa Kamanda Jongo, Jeshi la Polisi lilipata taarifa Julai 24, 2024 ya kukutwa kwa mwili wa mtoto anayekadiriwa kuwa na miezi miwili, ukiwa umetelekezwa shambani huku ukiwa umekatwa viungo ambavyo havijapatikana.
“Baada ya kupata taarifa, Jeshi la Polisi lilianza ufuatiliaji wa kina wa tukio hilo ambalo lilizua taharuki kwa wananchi na Julai 25, 2024, tulipata taarifa ya mwanamke aliyekuwa mjamzito, alijifungua watoto pacha lakini sasa ana mtoto mmoja na tumeanza uchunguzi,” amesema.
Kamanda Jongo amesema katika uchunguzi huo wamebaini Flora Mapolu (33), alijifungua watoto pacha, wa kike na kiume, lakini ndugu zake walishangaa kumuona hana mtoto mmoja na walipomhoji, hakuwa na majibu.
Ameeleza kwamba Julai 25, 2024, polisi walimkamata Flora akiwa nyumbani kwake Lwamgasa akiwa na mmoja wa kiume na walipomhoji, alikiri kujifungua pacha akiwa Mienze Ushirombo na kuwa wakati wa kujifungua alipata shida kwa kuwa alikuwa mwenyewe, hivyo alikosa msaada wa ndugu zake.
Amedai kwamba akiwa njiani, mtoto mdogo alizidiwa na kuona atakuwa kero kwa kuwa si mtoto wa mume wake anayeenda kuishi naye, hivyo aliamua kumnyonga kwa kipande cha kitenge na kumtupa, kisha akaendelea na safari.
“Mama huyu anakiri kumnyonga na kumtupa mwanaye. Ametuonyesha kipande cha kitenge kilichobaki na uchunguzi unaendelea kujua kama yeye alimnyonga na kumtupa, nani alimkata viungo. Pia, tunataka kujua ni wakati gani viungo vilinyofolewa kwenye mwili wa mtoto. Tunaendelea kuchunguza kujua kama viungo vilinyofolewa na mnyama au kuna mtu alivikata na kama ni mtu alijuaje kuna mtoto ametupwa na kwenda kuvikata. Tupo kazini na tutahakikisha tunapata majibu,” amesema Kamanda Jongo.
Kamanda Jongo amesema mama huyo anashikiliwa kwa mahojiano kwa tuhuma za kumuua mtoto wake.
Akizungumzia tukio hilo, Mganga Mfawidhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Deograsia Mkapa, amethibitisha kupokea mwili wa mtoto huyo na kuwa viungo hivyo vilikatwa kuanzia begani na kwenye paja.
“Tumepokea mwili wa mtoto mchanga anayekadiriwa kuwa na miezi minne hadi sita, akiwa amekatwa mkono wa kulia na mguu wa kulia. Aliokotwa akiwa amepoteza maisha na majeraha yapo kwenye bega na paja na inaonekana alikufa kwa kupoteza damu nyingi,” amesema Dk Mkapa.
Katika tukio jingine la Julai 24, 2024, mwanamke aitwaye Rehema Paulo (26), alijeruhiwa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu za kichwani na kukatwa viganja, chanzo kikiwa wivu wa mapenzi.
Inadaiwa mwanamke huyo alikuwa na mgogoro wa kimapenzi na mwanaume aliyefahamika kwa jina la Baba Law na kuwa siku ya tukio, alipigiwa simu na mtu wakaonane na alipofika, alivamiwa na kujeruhiwa.
“Hadi sasa Baba Law na mke wake wametoroka nyumbani na Jeshi la Polisi linaendelea kufuatilia ili kumkamata,” amesema Kamanda Jongo.
Kamanda huyo amesema matukio yanayotokea mkoani humo yanasababishwa na wananchi kulipiziana visasi na kujichukulia sheria mkononi.
Amewaomba wazazi kuwalinda watoto na wanapoona wamekwama ni vizuri wakaomba msaada ustawi wa jamii.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.