PARIS, UFARANSA: Huko Paris ambapo hali ya hewa siyo joto sana, Diaba Konate anaonyesha msisimko huku akiwa na tabasamu pana akielekea mahali alipokubaliana kukutana na mwandishi wa BBC karibu na Louvre. Nyota huyo amevaa jezi yenye nambari 23. Bila shaka hivyo ndivyo ilivyo – mpira wa kikapu ni mapenzi yake.
Mchezaji anayecheza nafasi ya ‘point guard’ mwenye umri wa miaka 23 anayekipiga katika timu ya Idaho, Marekani, hivi karibuni alirejea kwenye jiji lake la nyumbani, Paris, baada ya karibu miaka sita akiwa Marekani na aliishi maisha ya mafanikio akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Idaho.
Chuo hicho kilimnasa nyota huyo kutoka nchini kwake na kumpa ufadhili wa kumsomesha kutokana na uwezo wake mkubwa wa kucheza kikapu. Nyota aliichezea UC Irvine na kuisaidia kufikia mashindano ya juu zaidi ya kikapu kwa vyuo Marekani maarufu kaa NCAA ikiwa ni mara ya kwanza tangu 1995.
Diaba amejitokeza kama nyota mpya katika timu ya vijana ya taifa ya Ufaransa, akishinda medali ikiwemo fedha katika mpira wa kikapu kwenye michezo ya vijana ya Buenos Aires 2018 – uzoefu aliouwekeza akitamani kurudia kwenye michezo ya Olimpiki iliyoanza wiki hii, Paris.
Lakini mchezaji huyo ana hisia mchanganyiko kuhusu kurudi nyumbani kwa sababu amekatazwa kushiriki mashindano Ufaransa na sababu ikitajwa ni uvaaji wake wa vazi la hijabu, kwa mujibu wa imani yake ya Kiislamu.
Hadithi kama ya Konate imekuwa ya kawaida katika madaraja yote ya mpira wa kikapu yanayosimamiwa na Shirikish la Kikapu Ufaransa (FFBB), ikimaanisha wachezaji wanaovaa hijabu wanakutana na vikwazo vya mafunzo na fursa za mashindano – na wakihisi athari kwenye ustawi wao wa kijamii.
Katika uwanja wa mpira wa kikapu uliopo Paris, Salimata Sylla anaandaa moja ya vikao vya wachezaji wa mchezo huo nchini humo akieleza ni nafasi yao kutoa kile wanachoamini kwa sababu wananyamazishwa kuonyesha walichonacho. Kikao hicho kinahudhuriwa na wanawake na wasichana wanaopenda michezo – bila kujali kama wanavaa hijabu au la.
Tangu alipoanza kuendesha vikao hivyo mwaka jana, wanawake zaidi 60 wamekuwa wakihudhuria kwa wakati mmoja na lengo ni kupambania haki yao ya kucheza wakiwa na mavazi watakayo linafanikiwe.
“Niko mbele yenu kwa sababu ya mpira wa kikapu,” anasema Sylla. “Mpira wa kikapu ni kila kitu kwangu. Si neno tu; umeokoa maisha yangu. Nilikuwa naishi katika eneo lililoshamiri kwa dawa za kulevya. Mpira wa kikapu umenisaidia kuwa mtu bora, kuwa na nidhamu katika maisha na kuwa bora zaidi.”
Sylla alikuwa kwenye timu ya ligi ya Ufaransa, Aubervilliers, lakini hajacheza kwa zaidi ya mwaka mmoja. Januari 2023, kabla ya kuwa nyota wa timu hiyo akicheza kama point guard, kocha wa Sylla alilazimika kutoa habari mwamuzi atamruhusu tu kuingia uwanjani kama atavua hijabu yake.
Kama mwanamke Mwislamu ambaye alikuwa akicheza akiwa na hijabu kwa miaka mitatu hadi wakati huo, ilikuwa vigumu kukubaliana na kauli hiyo. Anakumbuka alimwambia mwamuzi wa mechi: “Unione hivi na hutaniona kwa njia nyingine.”
“Nilidhihakiwa mbele ya kila mtu,” anasema Sylla. “Hii ni nchi nilikozaliwa na siku hiyo waliniweka kando.”
Baada ya safari ya saa tatu kutoka Paris hadi kaskazini mwa Ufaransa, Sylla alikaa kwenye benchi na kuangalia timu ikicheza bila yeye kucheza. Nyota huyo anapinga mitazamo ya kibaguzi kwa njia ya dini akisema: “Wanadhani ukivaa hijabu, uko jikoni tu na hufanyi chochote na maisha yako.
“Lakini mimi ni mfano. Mimi siyo Muislamu tu, siyo mwanamke anayevaa hijabu tu, bali ni mjasiriamali. Nafanya kazi na pia nacheza mpira wa kikapu.”
Helene Ba, mwanzilishi mwenza wa Basket Pour Toutes (Mpira wa Kikapu Kwa Wote), anasema sera ya kuzuia uvaaji hijabu katika michezo Ufaransa imepitwa na wakati na ni ubaguzi wa wazi kwa binadamu katika nchi huru. Sheria hiyo inawahusu siyo wachezaji tu, bali pia makocha na waamuzi. Na huwatoa wachezaji wanaovaa hijabu za michezo kutoka kwenye eneo la mashindano.
Lakini wakati Michezo ya Olimpiki Paris inaandika historia kuwa ya kwanza kufanikisha uwiano wa kijinsia uwanjani, wanawake wa Kiislamu nchini humo wanaendelea kukumbana na vikwazo kwenye viwanja vya nyumbani – jambo ambalo wanaharakati wanasema ni uvunjaji wa haki za binadamu wenye athari mbaya zaidi katika jamii.
“Ni janga kwa michezo ya Ufaransa – kwa michezo ya wanawake,” anasema Helene Ba, ambaye baada ya kupitia uzoefu kama wa Sylla alianzisha Basket Pour Toutes, ukiwa ni umoja uliojikita kupambana na ubaguzi katika mpira wa kikapu.
“Inaonekana kana ni sawa au haki, ilhali si hivyo. Hawataki tuwe na chaguo, wanataka tu tusahau utambulisho wetu na imani. “Sitakubali kamwe imani au maadili yangu viingiliwe na kuzuiwa hasa kwa sababu najua hii ni sheria siyo ya haki,” anasema.
Septemba, mwaka jana, Waziri wa Michezo wa Ufaransa, Amelie Oudea-Castera alithibitisha kwamba hijabu ilikuwa imepigwa marufuku kwa timu zote za Ufaransa kwenye Olimpiki. Uamuzi huo ulipingwa na Umoja wa Mataifa kupitia idara ya haki za binadamu pamoja na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC), lakini baadaye hijabu zikakubalika ndani ya kijiji cha wanamichezo wa michezo hiyo.
Wakati huohuo, Diaba bado anapima kama aendelee kujifua kwa mazoezi binafsi, lakini kwenye michezo hii ya Olimpiki hatashiriki. “Nalenga kujikubali na kukubali kinachoendelea,” anasema. “Najiambia kuwa nimekuwa na kazi ya ajabu – hasa kucheza na timu ya taifa ya Ufaransa. Nadhani ni ndoto ya kila mchezaji kuwakilisha nchi. Mara hii ningefanya maajabu nyumbani.”
Pia amejiunga na Basket Pour Toutes kuunga mkono wachezaji wanaovaa hijabu, lakini akiwa na hisia mchanganyiko.
“ Ni jambo la kijinga (kututenga). Hawapaswi kufanya hivi; hatupaswi kufanya hivi,” anasema Diaba.
“Ni jambo la huzuni kwangu kuanza kupigania hili. Nachofanya (kuvaa hijabu) nitaendelea kufanya, lakini ni huzuni kwa sababu serikali ina masuala muhimu zaidi inapaswa kulenga (kufanya) kuliko wanawake Waislamu wanaovaa hijabu uwanjani.”