Nyuma ya raha ya bodaboda kuna hatari hizi kiafya…

Dar es Salaam. Pamoja na uhakika wa kufika haraka, kupenya kwenye msongamano na gharama nafuu za usafiri wa bodaboda, unajua madhara ya kiafya yaliyojificha nyuma ya raha hizo?

Sikutishi uache kupanda au kuendesha bodaboda, muktadha wa andiko hili ni mtazamo wa wataalamu wa afya, wanaoeleza madhara ya kiafya yanayowakabili watumiaji na madereva wa usafiri huo, hasa wasipotumia vifaa kinga, ikiwemo kofia ngumu.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, pengine hutayaona matokeo sasa, lakini kwa kadiri siku zinavyokwenda ndivyo unavyokaribia kukabiliwa na madhara hayo, ikiwemo upungufu wa nguvu za kiume kwa wanaume.

Msingi wa kauli za wataalamu hao ni kile kilicholalamikiwa na baadhi ya madereva wa bodaboda, kuhusu kukabiliwa na magonjwa ya vifua na mapafu mara kwa mara.

Sambamba na magonjwa hayo, madereva hao wa bodaboda wametaja kusumbuliwa pia na migongo na viuno, huku baadhi wakikumbwa na magonjwa ya ajabu yanayosababishwa na mitikisiko inayochochewa na ubovu wa barabara.

Hata hivyo, magonjwa ya mapafu yanajumuishwa katika magonjwa ya mfumo wa hewa. Takwimu zilizotolewa Februari mwaka huu na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu zinaonyesha kuwa maambukizi ya mfumo wa hewa yaliongoza.

“Kwa mwaka 2023, maambukizi ya mfumo wa hewa yaliwaathiri Watanzania milioni 4,901,844, sawa na asilimia 18.9, huku matatizo ya njia ya mkojo (UTI) ikiathiri Watanzania milioni 4,095,104 sawa na asilimia 15.8,” anasema Waziri Ummy.

Maumivu ya kifua na mapafu kujaa maji ni miongoni mwa magonjwa yanayomsumbua Daniel William, anayefanya kazi ya udereva bodaboda jijini Dar es Salaam.

“Kama huvai kofia ngumu, unahisi kabisa baridi inapita puani moja kwa moja kwa sababu upepo ni mkubwa, ugonjwa wa macho pia tunapata, hasa mtu asipovaa kofia ngumu yenye kioo,” anasema.

Magonjwa hayo kwa mtazamo wa William, yanasababishwa na vumbi na mchanga unaorushwa na magari au bodaboda zinazowatangulia barabarani.

“Wakati mwingine mnaona macho yanatoka machozi au yanakuwa na rangi nyekundu, pia tunaumwa sana kichwa kwa sababu unakuta muda wote macho yanatoka machozi,” anasema.

Hashim Bariki, anayefanya shughuli hiyo pia, anasema changamoto kubwa kwake ni maumivu ya mgongo na kiuno, yanayosababishwa na mashimo yaliyopo katika baadhi ya barabara.

“Barabara mbovu mtu ukienda kulala mwili wote hauna hali, hasa kwenye mgongo na kiuno tunapata maumivu sana, kutokana na kurushwa kwenye mashimo ya barabara,” anaeleza.

Kinachomkabili Hashim ni tofauti na Hamza Juma, anayeendesha bodaboda katika jiji hilo, anayesema kuwashwa mikono ndilo tatizo sugu kwake, hasa nyakati za usiku.

“Yaani kwa hizi njia zetu zenye mashimo, kila ikifika usiku nikiwa nimetulia nasikia viganja vya mikono vinawasha, yaani kama mtu ananichoma na sindano.

“Hii inanitokea kila siku, hasa nikiendesha pikipiki kwenye njia mbovu, baada ya muda inatulia,” anasema.

Bodaboda na nguvu za kiume

Upo uhusiano wa matatizo ya afya ya uzazi kwa wanaume na uendeshaji wa bodaboda katika barabara mbovu, kama inavyoelezwa na mtaalamu wa mfumo wa uzazi kwa wanaume wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Deogratius Mahenda.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, uendeshaji wa bodaboda katika barabara hizo unasababisha maumivu ya mgongo na kiuno, viungo ambavyo ndiyo maeneo muhimu kwa nguvu, hasa za kiume.

“Maumivu hayo yakitokea inaweza kusababisha athari kwenye viungo vya uzazi na pengine nguvu za kiume. Nguvu za kiume zinategemea mfumo wa fahamu na damu iende ya kutosha kwenye uume,” alisema.

Kama ulidhani muziki wa sauti ya juu unaopigwa kwenye bodaboda ni starehe unakosea, kelele hizo zinahatarisha mfumo wako wa kusikia, kwa mujibu wa Mtaalamu wa Masikio, Pua na Koo, Dk Edwin Lyombo.

“Sauti ya kiwango cha juu bila ya kuwa na kitu cha kuzuia inapunguza usikivu. Athari hizo zinaenda taratibu, hata akiendesha bodaboda leo, matatizo atayagundua baadaye, mwanzoni anaweza asione shida,” anasema Dk Lyombo.

Kuna hatari ya kupata madhara ya muda mfupi na mrefu iwapo utaendesha bodaboda bila kuzingatia matumizi ya mavazi maalumu, ikiwemo kofia ngumu, kama inavyofafanuliwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa yatokanayo na kazi, Hussein Mwanga.

Dk Mwanga, ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya ya Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), anayataja miongoni mwa madhara ya muda mfupi ni maambukizi ya kifua.

Kwa upande wa madhara ya muda mrefu, anasema ni athari katika mapafu inayosababishwa na vumbi, moshi na uchafu mwingine unaotokana na moshi.

“Hii inaweza kuleta madhara ya muda mrefu na inaathiri zaidi mapafu kwa sababu tunavuta zaidi hewa na vumbi likifika kwenye mapafu linajibadilisha kama mtu aliyevuta sigara, madhara yake ni kama ugonjwa wa COPD,” anasema.

Madhara mengine ya muda mrefu kwa mujibu wa Dk Mwanga, ni ugonjwa wa shambulio la pumu na magonjwa mengine ya kifua ambayo aghalabu ni hatari kwa binadamu.

Saratani na magonjwa ya moyo ni madhara mengine ya kudumu yanayoweza kumkabili mtu anayeendesha bodaboda bila kuvaa vifaa maalumu.

“Ukiachana na mapafu, kuna magonjwa mengine ambayo yana uhusiano na magonjwa ya moyo hadi saratani ya mapafu.

“Wanaoathirika zaidi ni watoto, lakini pia watu wazima na inaathiri hadi ukuaji wa mapafu, kama watoto ni abiria wa mara kwa mara au wanaishi karibu na barabara mapafu yanaweza yasikue vizuri,” anasema.

Ili kuepuka magonjwa hayo, Dk Mwanga anasema madereva bodaboda wanapaswa kuvaa vifaa vya kujikinga kama maski na uzingatiwaji wa hilo ufanywe nchi nzima.

“Ni vizuri hatua zikaanza kuchukuliwa juu, kama nchi iamue kupunguza hilo, kila mtu apunguze uchafuzi wa hali ya hewa kama vile kupunguza magari na ndiyo maana kwenye nchi zilizoendelea zinatumika sana baiskeli.

“Tunapaswa kuwa na lami zitakazosafishwa kila wakati kwa ajili ya kupunguza vumbi,” anaeleza.

Related Posts