Mirerani. Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara limeeleza chanzo cha vifo vya wanafunzi wawili wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (Must) kuwa ni kuvuta hewa chafu wakiwa mgodini Mirerani, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.
Wanafunzi hao wa Must wamefariki dunia kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite walikokwenda kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu vifo hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, George Katabazi amesema tukio hilo limetokea saa 12 jioni Julai 24, 2024.
Kamanda Katabazi amesema wanafunzi hao wamefariki dunia kwenye machimbo ya kitalu D kwenye mgodi unaomilikiwa na kampuni ya Franone Mining and Company walikokuwa wakipata elimu ya miamba ya Tanzanite kwa vitendo.
Amewataja marehemu hao kuwa ni Maulid Omary (23) ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili na Given Machunde (25), mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa chuo hicho.
Kamanda huyo amesema chanzo cha vifo vya wanafunzi hao ni baada ya kuvuta hewa chafu wakiwa umbali wa zaidi ya mita 250 kutoka eneo salama walilopaswa kuwepo.
Ameongeza kuwa miili yao imehifadhiwa katika Kituo cha Afya cha Mirerani kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Mmoja kati ya jamaa wa marehemu hao, John Ezekiel amesema Machunde ni mwenyeji wa Bunda mkoani Mara na Omary ni mwenyeji wa Arumeru mkoani Arusha.
“Wamefariki wakiwa wadogo, tunamshukuru Mungu kwa kila jambo kwani siku hiyo walienda eneo ambalo hawakupaswa kwenda na kumefariki dunia kwa kuvuta hewa chafu,” amesema.
Awali, uongozi wa Must ulikiri vijana hao kuwa wanafunzi wake na kuwa walikwenda Mirerani kwenye mafunzo kwa vitendo.
Hata hivyo haukueleza zaidi kuhusu tukio hilo wala chanzo chake.